Idara ya Habari (MAELEZO) ipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, ikiwa na jukumu la kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera,
Mipango na Miradi ya Maendeleo vinavyotekelezwa na Serikali kwa wananchi,
kusimamia vyombo vya habari hasa magazeti na machapisho na kuishauri
Serikali juu ya sera na sheria za habari.
Idara iliundwa mwaka 1945 wakati wa Vita ya Pili ya Dunia. Wajibu wa Idara
kwa wakati huo kwa kushirikiana na magazeti mbalimbali yakiwemo Mambo Leo
na Habari za Leo ilikuwa ni kuwajulisha wananchi kuhusu maendeleo ya vita.
Aidha kwa wakati huo, Idara ilikuwa na jukumu la kupiga picha mbalimbali za
matukio ya Serikali yanayotokea ndani na nje ya nchi.
Kati ya mwaka 1961-1962 majukumu ya Idara ya Habari yaliwekwa chini ya
Wizara ya Elimu na Habari. Baadaye mwaka 1962-1964 yalibadilishwa na
kuhamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kabla ya kurejeshwa katika
Wizara ya Habari na Utalii mwaka 1964-1971.
Kuanzia mwaka 1979-1984, Idara iliwekwa chini ya Wizara ya Habari na
Utangazaji na baadae Wizara ya Habari na Utamaduni. Mwaka 1991 Idara
ilirejeshwa tena katika Ofisi ya Makamu wa Rais na baadaye kuhamishiwa
katika Ofisi ya Waziri Mkuu kati ya mwaka 2005-2008.
Kutoka 2008 hadi sasa Idara ya Habari ipo chini ya Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Hassan
Abbasi. Kwa sasa Idara ina sehemu kuu tatu ambazo ni Sehemu ya Habari na
Huduma za Picha, Sehemu ya Uratibu na Usajili na Sehemu ya Uratibu wa
Mawasiliano Serikalini.
Hakimiliki ©2019 GWF. Haki zote zimehifadhiwa.