Idara ya Habari-MAELEZO ipo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ikiwa na jukumu la kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera, Mipango na Miradi ya Maendeleo vinavyotekelezwa na Serikali kwa wananchi, kusimamia vyombo vya habari hasa magazeti na machapisho na kuishauri Serikali juu ya sera na sheria za habari.
Idara iliundwa mwaka 1945 wakati wa Vita ya Pili ya Dunia. Wajibu wa Idara kwa wakati huo kwa kushirikiana na magazeti mbalimbali yakiwemo Mambo Leo na Habari za Leo ilikuwa ni kuwajulisha wananchi kuhusu maendeleo ya vita. Aidha kwa wakati huo, Idara ilikuwa na jukumu la kupiga picha mbalimbali za matukio ya Serikali yanayotokea ndani na nje ya nchi.
Kati ya mwaka 1961-1962 majukumu ya Idara ya Habari yaliwekwa chini ya Wizara ya Elimu na Habari. Baadaye mwaka 1962-1964 yalibadilishwa na kuhamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kabla ya kurejeshwa katika Wizara ya Habari na Utalii mwaka 1964-1971.
Kuanzia mwaka 1979-1984, Idara iliwekwa chini ya Wizara ya Habari na Utangazaji na baadae Wizara ya Habari na Utamaduni. Mwaka 1991 Idara ilirejeshwa tena katika Ofisi ya Makamu wa Rais na baadaye kuhamishiwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu kati ya mwaka 2005-2008.
Kwa sasa Idara ya Habari ipo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuihamisha Idara ya Habari kwenda kwenye Wizara iliyokuwa ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Idara ina sehemu kuu tatu ambazo ni sehemu ya Habari na Huduma za Picha, sehemu ya Uratibu na Usajili na sehemu ya Uratibu wa Mawasiliano Serikalini.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO