Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Agosti, 2018 aliposalimiana na wananchi waliokusanyika katika njiapanda ya Bugando Jijini Mwanza na Mjini Sengerema akiwa njiani kuelekea Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Mhe. Rais Magufuli amesema utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano unakwenda vizuri ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi 8 kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 3,060, Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) limefufuliwa, miundombinu ya barabara na madaraja inajengwa, watoto wanapata elimu bure na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua uwigo wa ajira na kukuza uchumi wa nchi.
“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu tunakwenda vizuri, juhudi zetu za kujenga Tanzania mpya zinapata mafanikio makubwa, tumejenga viwanda vingi, nataka tuirudishe Tanzania ya Nyerere ambapo hapa Mwanza kulikuwa na viwanda vingi na vijana wengi walipata ajira” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa Sengerema Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi ambapo amepiga marufuku viongozi wa halmashauri kuwanyang’anya bidhaa zao wafanyabiashara wadogo na badala yake ameagiza viongozi wote nchini kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa soko la mazao yao.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa Sengerema kudai Halmashauri ya Wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza matunda yao mjini hapo.
Amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.
“Nilishasema viongozi wote niliowateua mimi msisherehekee uteuzi, mtasherehekea siku mkimaliza uongozi, nataka mchape kazi, tatueni kero za wananchi na waleteeni maendeleo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kukutana na wananchi wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) ya hospitali ya Bugando Jijini Mwanza akiwemo dada yake Bi. Monica Joseph Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuwatibu wagonjwa, na amesema Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amesafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha shirika hilo, na akiwa ndani ya ndege abiria waliosafiri nae kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza wamemshangilia na kumpongeza kwa juhudi zake za kuifufua ATCL na wamemuombea dua.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Agosti, 2018.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO