Wasifu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar. Alisomea shule za msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) kati ya 1966 na 1972 na kisha alisoma masomo ya upili Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976).
Alisoma kozi mbalimbali hadi akafikia kupata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.
Kazi
Aliajiriwa kama mchapishaji katika serikali ya Zanzibar mwaka 1977 na akapanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango serikalini kati ya 1987 na 1988.
Alihudumu pia kama meneja wa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama meneja mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGO 1998 hadi 1999.
Familia
Aliolewa mwaka wa 1978, kwa Bw Hafidh Ameir, ambaye wakati huo alikuwa Afisa Kilimo na walijaliwa watoto wanne.
Siasa
Alijiunga na siasa mwaka wa 2000, Wakati huo alijiunga na Baraza la wawakilishi la Zanzibar kama mjumbe maalum.
Haikuchukua muda mrefu nyota yake ikaanza kung'aa na akateuliwa kuwa waziri na rais Amani Karume, akipewa wadhifa wa Waziri wa Kazi, Jinsia na Watoto.
Alitumikia taifa hadi mwaka wa 2005 alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri, wakati huu akipewa Wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji katika serikali ya visiwani.
Mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi.Baada ya hapo akateuliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.
Machi mwaka 2014, aliwania na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma. Mama Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Amina Abdalla Amour ambaye alipata kura 126 sawa na 24%.
Julai mwaka 2015, Dkt John Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza.
Wale wanaomjua Mama Samia wanasema kuwa ni mchache wa maneno.
Hakimiliki ©2022 Habari MAELEZO