Kongamano la Kiswahili Paris Kufungua Fursa za Biashara, Utalii na Uwekezaji Duniani
Na Baraka Messa – MAELEZO
Serikali imesema Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili litakalofanyika jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Julai 4 hadi 7, 2026, litakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika kwa ujumla kupitia lugha ya Kiswahili, huku likitarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya kongamano hilo, akieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Jitihada za Serikali ni kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati ili kiwe chachu ya kukuza biashara, kutangaza utalii na kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani,” amesema Msigwa.
Amesema Kiswahili kwa sasa si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni rasilimali yenye fursa nyingi za kiuchumi, kielimu na kidiplomasia ambazo zinaendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya lugha hiyo duniani.
Msigwa amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Cuba yameongeza hadhi ya Kiswahili kimataifa, ambapo kwa sasa baadhi ya taasisi za elimu nchini Urusi na Ufaransa zimeanza kufundisha lugha hiyo.
Pia amesema Kiswahili kimeanza kuingizwa katika mifumo ya kidijitali ikiwemo mitandao ya Kijamii, jambo linaloonyesha namna lugha hiyo inavyozidi kupata nafasi katika maendeleo ya teknolojia na ubunifu duniani.
Kwa mujibu wa Msigwa, kongamano la Paris litahusisha tamasha kubwa la maonyesho ya Kiswahili, midahalo kuhusu tafiti na makala mbalimbali zinazohusu lugha hiyo pamoja na shughuli za kubadilishana uzoefu kati ya wadau kutoka mataifa mbalimbali.
Takribani washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki kongamano hilo, wakiwemo mabalozi, wawakilishi wa UNESCO, wataalamu kutoka vyuo vikuu, wafanyabiashara pamoja na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Amesema Serikali inaamini kuwa kupitia kongamano hilo, Kiswahili kitaendelea kujijengea heshima duniani na kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukuza biashara, utalii na uwekezaji kwa manufaa ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Mwisho