Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Baraka Messa – MAELEZO Serikali imesema Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili litakalofanyika jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Julai 4 hadi 7, 2026, litakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika kwa ujumla kupitia lugha ya Kiswahili, huku likitarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya kongamano hilo, akieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati katika kuchochea maendeleo ya uchumi. Jitihada za Serikali ni kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati ili kiwe chachu ya kukuza biashara, kutangaza utalii na kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani,” amesema Msigwa. Amesema Kiswahili kwa sasa si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni rasilimali yenye fursa nyingi za kiuchumi, kielimu na kidiplomasia ambazo zinaendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya lugha hiyo duniani. Msigwa amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Cuba yameongeza hadhi ya Kiswahili kimataifa, ambapo kwa sasa baadhi ya taasisi za elimu nchini Urusi na Ufaransa zimeanza kufundisha lugha hiyo. Pia amesema Kiswahili kimeanza kuingizwa katika mifumo ya kidijitali ikiwemo mitandao ya Kijamii, jambo linaloonyesha namna lugha hiyo inavyozidi kupata nafasi katika maendeleo ya teknolojia na ubunifu duniani. Kwa mujibu wa Msigwa, kongamano la Paris litahusisha tamasha kubwa la maonyesho ya Kiswahili, midahalo kuhusu tafiti na makala mbalimbali zinazohusu lugha hiyo pamoja na shughuli za kubadilishana uzoefu kati ya wadau kutoka mataifa mbalimbali. Takribani washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki kongamano hilo, wakiwemo mabalozi, wawakilishi wa UNESCO, wataalamu kutoka vyuo vikuu, wafanyabiashara pamoja na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Amesema Serikali inaamini kuwa kupitia kongamano hilo, Kiswahili kitaendelea kujijengea heshima duniani na kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukuza biashara, utalii na uwekezaji kwa manufaa ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mwisho

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kujitegemea katika kugharamia shughuli za maendeleo kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani huku akieleza kuwa mchango wa makampuni, mashirika na taasisi za umma unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo. Rais Samia amesema hayo Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, Ikulu jijini Dar Es Salaam. Rais Samia ameeleza kuwa mafanikio hayo yatachangia kupunguza pengo la kujitegemea katika bajeti ya mwaka huu na kwa miaka miwili ijayo jambo linaloonyesha kuwa mikakati ya kuongeza mapato ya ndani imeanza kuzaa matunda. “Gawio na mchango uliotolewa na makampuni, taasisi na mashirika yetu ni sehemu ya lengo letu la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharamia shughuli za maendeleo” amesema Rais Samia Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa matumaini yataongezeka endapo kasi ya ukusanyaji wa mapato na ufanisi wa taasisi utaendelea kuimarika ndani ya miaka miwili ijayo, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kugharamia maendeleo yake kwa kutegemea vyanzo vya ndani pekee. Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amewaelekeza viongozi na watendaji wote kutoridhika na pongezi wanazopata, bali amewasisitiza kuwa, pongezi hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii, ubunifu na maarifa ili kufikia matokeo makubwa zaidi katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa mapato. Kadhalika, ameeleza kuwa maendeleo ya uchumi wa Taifa yanahitaji uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa rasilimali na juhudi endelevu kutoka kwa taasisi zote za umma ili kuhakikisha mchango wao unaendelea kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amevigiza vituo vya utafiti wa afya nchini kushirikiana na wabobezi wa tafitri duniani, kutafuta sababu za ongezeko la saratani na moyo kwa watoto wadogo ili kupata sababu zinazosababisha ongezeko la maradhi hayo na kutoa elimu kwa Watanzania ili kuepuka mambo yanayosababisha saratani kwa watoto. Rais Samia ametoa maagizo hayo Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa huduma za tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC mjini Moshi,  na kueleza kuwa uwepo wa tiba mionzi katika Kanda ya Kaskazini, utasaidia kupunguza changamoto kwa wagonjwa wa saratani ambao awali walilazimika kwenda maeneo mengine yakiwemo Dar es Salaam kupata matibabu. Hili ni suala la kuangalia kwa kina hasa watafiti wetu. Vituo vyetu vya watafiti wa afya kwa kushirikiana na waliotuzidi ujuzi duniani, tuzame kutafuta sababu zinazoleta ongezeko la maradhi hayo kwa watoto wetu na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ya Watanzania ili kuepuka yale yote yanayofanya tulete watoto wenye maradhi hayo duniani”, ameelekeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema ili kuimarisha huduma za afya nchini zikiwemo kinga, uchunguzi, na matibabu, Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika huduma hizo, ambapo imetoa shilingi bilioni 5.5 kusaidia kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi. “Hospitali ya rufaa ya KCMC ina heshima kubwa hapa nchini na hata jirani kwa huduma bobezi na za kibingwa zinazotolewa hapa. Uzinduzi wa jengo hili la tiba mionzi ni hatua nyingine muhimu katika kusogeza huduma hizo karibu na wananchi”, ameeleza Rais Samia. Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma kubwa za afya ikiwemo matibabu ya saratani na magonjwa ya moyo katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma karibu na wanapoishi na kwamba uwepo wa hospitali hiyo ya rufaa KCMC ni faraja kubwa kwa familia nyingi zilizokuwa zikibeba gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata matibabu. Rais Samia amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za afya, taasisi za dini na mashirika ya maendeleo yaliyoshiriki katika kufanikisha mradi huo, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini. Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kituo hicho kwa sasa kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka na kikikamilika kitaweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 3,900 kwa mwaka. Mhe. Mchengerwa amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama kwa familia, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini umeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya. Mwisho

Na Baraka Messa – MAELEZO Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya Wabunge wengi kuunga mkono mapendekezo ya matumizi na makusanyo ya Serikali yaliyowasilishwa bungeni. Akitoa matokeo ya kura zilizopigwa Juni 23, 2026, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema jumla ya wabunge 395 walihudhuria kikao hicho huku wabunge wanane wakikosekana. Mhe. Zungu amesema kati ya wabunge waliohudhuria, wabunge 385 walipiga kura za ndiyo, sawa na asilimia 97.26 ya kura zote zilizopigwa, huku wabunge wanane wakipiga kura za hapana. Matokeo hayo yamedhihirisha uungwaji mkono mkubwa wa bajeti hiyo kutoka kwa wajumbe wa Bunge. Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatoa idhini kwa Serikali kuendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo pamoja na shughuli za kawaida za kiutawala katika mwaka mpya wa fedha. Bajeti hiyo imelenga kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kuendeleza miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mipango ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza ustawi wa wananchi. Amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Prof. Mkumbo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochangia kuongezeka kwa uzalishaji na mapato ya taifa. Aidha, ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango na miradi iliyopangwa, ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania katika miaka ijayo.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi, ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi kwenye afya hasa upande wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwani afya haijawahi kuwa gharama na ni uwekezaji ambao nchi inaweza kuona faida yake. Ametoa rai hiyo Juni 23, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika (ICPPA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam. Prof. Janabi amesema kuwa nchi inaweza kufanya magonjwa yasiyoambukiza kuwa kipaumbele cha maendeleo ya kitaifa kwa kutumia sera za kifedha zinazoweza kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na kodi kwenye tumbaku, pombe na bidhaa zote zenye sukari, kupanua ulinzi wa kifedha ili ugonjwa usimaanishe umaskini, kuongeza kiwango cha mpango wa Pen na Pen-Plus kitaifa pamoja na kuwalinda watoto kwa kutengeneza mazingira yenye afya bora. Tunaweza kuwa na vipaumbele vingi lakini tunasahau kuwa vipaumbele vinahitaji vitendo. Magonjwa yasiyoambukiza si tishio la baadaye tena katika bara letu bali ni ukweli wa sasa kwani yanasababisha asilimia 37 ya vifo. Magonjwa kamwe hayapaswi kuamua hatma ya mtu kwa sababu kila maisha ya Mwafrika yana thamani na utu sawa”, amesema Prof. Janabi. Akizungumzia kuhusu Pen-Plus, amesema kuwa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 20 na imeweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya 100,000 huku akisisitiza kuwa si miradi ya majaribio tu bali ina ushahidi kwani kupitia kuimarisha afya, watoto wanarudi shuleni, vijana wanaishi maisha marefu na akina mama wanajifungua salama na kuishi.  Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa Maendeleo, Bw. James Reid kutoka Mfuko wa Hisani wa Helmsley Charitable Trust ameeleza kuwa, kwa muda mrefu wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini kwenye ukanda wa Afrika, wanakabiliwa na changamoto zikiwemo za huduma za afya zisizofikika, kukosa wafanyakazi wa afya waliofunzwa na mifumo michache ya kuwahudumia wagonjwa hao pamoja na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, dawa au huduma za ufuatiliaji. “Tunahitaji kuendelea kupanua idadi ya nchi zinazohusika katika mtandao huu ili kufikia malengo ya kikanda ya nchi wanachama wa WHO. Tunahitaji kuendelea kujenga na kuimarisha nguvu kazi inayofanya huduma hii iwezekane, tunahitaji kufanya kazi pamoja na nchi husika ili kuhakikisha kuwa kuna ufadhili endelevu na kuhakikisha kuwa mfumo huu unaweza kuendelea kupanuka”, amemalizia Bw. Reid. PEN-Plus ni mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa NCDI Poverty unaolenga kupanua huduma za afya kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yaliyo sugu na makali. Mpango huu unapanua wigo wa huduma kutoka ngazi za chini ili wagonjwa wapate matibabu katika hospitali za wilaya au rufaa za ngazi ya kwanza bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Na Baraka Messa- MAELEZO  Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema Tanzania itaendelea kuwa sehemu muhimu katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake mkubwa wa kuhifadhi na kusaidia wapigania uhuru waliowezesha taifa hilo kupata uhuru, akieleza kuwa Kongwa ni moja ya maeneo yenye thamani kubwa katika historia ya ukombozi wa Afrika. Dkt. Nandi-Ndaitwah ametoa kauli hiyo Juni 21, 2026 alipotembelea eneo la kihistoria la Kambi ya Wapigania Uhuru wa Namibia wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katika ziara yake ya kwanza ya Kiserikali nchini Tanzania tangu aingie madarakani. Amesema ziara hiyo imekuwa ya kipekee kwake na kwa wananchi wa Namibia kwa kuwa imewapa fursa ya kushuhudia kwa macho yao sehemu ambayo mashujaa wa taifa hilo waliwahi kuishi, kupata mafunzo na kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni. Kongwa ni mahali Patakatifu pa ukombozi kwa sababu nchi nyingi zilizopigania uhuru zilipata hifadhi na mafunzo hapa. Mashujaa wetu wamelala mahali hapa na damu yao ilimwagilia uhuru wetu,”amesema. Amewataka Watanzania na Wanamibia kuendeleza ushirikiano uliowekwa na waasisi wa mataifa hayo kwa kushirikiana katika kukamilisha ukombozi wa kiuchumi wa nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla ili kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi. Akizungumzia umuhimu wa kuhifadhi historia hiyo, Rais Netumbo amesema ni wajibu wa kizazi cha sasa kuhakikisha mchango wa mashujaa wa ukombozi unaenziwa na kulindwa ili maadili, misingi na malengo waliyozipigania visiweze kupotea kwa vizazi vijavyo. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania na Namibia zina historia moja ya ukombozi na zinaendelea kushirikiana katika kutimiza azma ya kukamilisha ukombozi wa Afrika kupitia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuhifadhi maeneo yote ya kihistoria yaliyotumiwa na wapigania uhuru kwa kuyaacha katika hali yake ya asili ili kulinda uhalisia wa historia hiyo, huku ikiendelea kuboresha miundombinu katika maeneo jirani kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye.  

Na Baraka Messa – MAELEZO Serikali imekamilisha hatua muhimu za kisheria zitakazowezesha kuanza kwa malipo ya kifuta jasho kwa askari waliojitolea kushiriki Vita ya Kagera dhidi ya utawala wa Idd Amin mwaka 1978/79 ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kulinda uhuru na usalama wa Taifa. Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akijibu maswali ya papo kwa papo Juni, 18, 2026, bungeni Dodoma, amesema kuwa vikwazo vya kisheria vilivyokuwa vinazuia utekelezaji wa malipo hayo vimeondolewa kufuatia maelekezo ya Rais, hivyo kufungua njia kwa askari hao kupata stahiki zao baada ya kusubiri kwa muda mrefu. Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Njombe, Mhe. Deo Mwanyika, Mhe. Waziri Mkuu, amesema kuwa Serikali inaendelea na zoezi la utambuzi na uhakiki wa askari hao, ambapo takribani askari 7,200 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo mara baada ya taratibu husika kukamilika. Hatua hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuthamini na kutambua mchango wa wananchi walioweka maisha yao rehani katika nyakati muhimu za historia ya Taifa. Mwaka 2025 Serikali ilikamilisha zoezi la kuwatambua baadhi ya washiriki wa vita hii kutoka Uganda waliokuwa na mchango katika harakati za kuikomboa nchi wakati wa Vita vya Kagera, hatua iliyoweka msingi wa kuendelea kuwathamini wote walioshiriki katika mapambano hayo,” amesema Mhe. Waziri Mkuu. Vita ya Kagera ya mwaka 1978/79 inabaki kuwa moja ya matukio muhimu katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki, ambapo majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na wapigania uhuru wa Uganda yaliweza kuondoa utawala wa Idd Amin na kurejesha usalama katika eneo hilo.  

Na. Mwandishi Wetu – Singida Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Waziri wa Maji kwenda Mkoa wa Mwanza kushughulikia mara moja changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi wa mkoa huo na kuhakikisha huduma hiyo inarejea kwa haraka. Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo Juni 14, 2026 alipokuwa akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Kiomboi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Lulumba, Wilaya ya Iramba mkoani Singida. Amesema amepokea taarifa kuhusu changamoto ya maji katika Mkoa wa Mwanza na tayari amemuelekeza Waziri mwenye dhamana ya maji kwenda eneo husika kusimamia upatikanaji wa suluhisho la haraka.  Nimemtuma Waziri aende haraka Mwanza akasimamie jambo lile mpaka maji yapatikane. Sisi watu wa Singida tunataka tupate maji toka Mwanza. Simiyu tunataka tupate maji toka Mwanza. Dodoma tunataka tupate maji toka Mwanza. Tabora, wengine wameshaanza kupata maji toka Mwanza. Leo kuja kuambiwa Mwanza, pale pale lilipo Ziwa Victoria, pana shida ya maji. Hili ni jambo ambalo haliwezi kueleweka, na wala hatuwezi kulielewa,” amesema Dkt. Mwigulu. Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo wakati chanzo cha maji kinajulikana na miundombinu ya mradi ipo.  “Hatutaki ngonjera za maneno. Hawa wanasema si bomba limekuwaje, hawa wanasema si umeme umekuwaje. Chanzo sisi tunajua kiko pale, hatuna shida ya chanzo cha maji, na mradi upo, na maji yapo. Haya mambo mengine ni ya ngonjera, mimi sitaki kuyasikia,” amesema. Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa sekta ya maji pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa haraka. “Mkuu wa Mkoa awatafute wataalamu wake, awatafute TANESCO na wataalamu wa maji. wachimbe kiini cha tatizo na wakeshe mpaka wananchi wapate maji. Kunapopambazuka kesho nipate majawabu kwamba maji yamepatikana,” amesema. Juni 9, 2026, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu upungufu wa huduma ya maji uliosababishwa na hitilafu za umeme zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara. Wakati huohuo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji katika Tarafa ya Kiomboi na maeneo mengine ya Wilaya ya Iramba inapata ufumbuzi wa kudumu kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta hiyo nchini. Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele maalum katika sekta ya maji kwa kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.  Niwahakikishie kwamba hili ni eneo ambalo Mheshimiwa Rais ameliwekea kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu maji ni uhai, maji ni maisha. Tulihangaika kupata chanzo cha uhakika cha maji na sasa kimepatikana, hatua mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika,” amesema. Aidha, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji pamoja na kuimarisha uwezo wa uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabwawa na upimaji wa vyanzo vya maji ili kukabiliana na changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali nchini. Dkt. Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi amesema Serikali inaendelea na usanifu wa barabara ya Kiomboi–Kisiriri–Sibiti kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami na kuboresha mawasiliano kati ya wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani. Aidha, amesema usanifu wa barabara ya Kitusha–Galangala–Kisana–Kinampanda–Kisiriri umekamilika, huku Serikali ikiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi mingine ya barabara katika Wilaya ya Iramba ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi. Pia amesema usanifu wa daraja la kuunganisha eneo la Hospitali ya Kiomboi na maeneo ya Meli pamoja na Iguguno umekamilika na hatua zinazofuata ni kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Chuo Kikuu katika eneo la Kiomboi baada ya eneo lililotengwa kuridhiwa na wataalamu husika.  Hapa Kiomboi tutakuwa na Chuo Kikuu. Eneo limekaguliwa na kuridhiwa na hatua za utekelezaji zinaanza,” amesema. Amesema pindi ujenzi wake utakapokamilika, Chuo Kikuu hicho kinatarajiwa kuanza kwa awamu ya kwanza kwa uwezo wa kuhudumia wanafunzi takribani 10,000.

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeandika historia nyingine baada ya jopo la madaktari bingwa na wataalamu wa afya kufanikisha salama uzazi wa watoto watano kwa wakati mmoja kwa Bi. Victoria Mkwizu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam. Watoto hao ambao watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike, wamezaliwa tarehe 13 Juni 2026 na wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa wataalamu wa hospitali hiyo. Akiwa wodini, Bi. Victoria amesema anafurahia huduma alizopata katika hospitali hiyo tangu alipopokelewa hadi kujifungua. “Nawapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya kwa uangalizi wa karibu walionipatia katika kipindi chote cha matibabu kwani mchango wao umetuwezesha mimi na watoto kuendelea vizuri”, amesema Bi. Victoria. Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville amesema tukio hilo ni la kipekee na limehitaji ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa hospitali hiyo ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto huku akimpongeza Bi. Victoria kwa kujifungua salama na kuwatakia wote afya njema. Tunampongeza sana Bi. Veronica kwa kubarikiwa watoto mapacha watano, hospitali yetu itagharamia gharama zote za matibabu za kwake na watoto wake kuanzia alipolazwa hospitalini tarehe 15 Mei, 2026 hadi watakapomaliza matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani”, ameeleza Dkt. Rachel. Amefafanua kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za hospitali kuhakikisha mama na watoto wanaendelea kupata huduma bora na salama katika kipindi hicho.

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO.  Serikali imebainisha mikakati mipya ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa taifa kujitegemea kiuchumi na kugharamia maendeleo kupitia rasilimali zake. Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Juni 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya juhudi za kujitegemea kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali. “Ni muhimu kuendelea kuimarisha uwezo wa nchi kugharamia maendeleo yake kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mikopo na changamoto zake,” amesema Balozi Omary. Amefafanua kuwa kupitia Mkakati wa Ukusanyaji wa Mapato wa Muda wa Kati wa mwaka 2025/26 hadi 2027/28, Serikali itaanza kutekeleza hatua mbalimbali zitakazopanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya ndani. Miongoni mwa hatua hizo ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza shughuli za kiuchumi, ajira na mapato ya kodi. Serikali pia itaendelea kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kupitia majukwaa ya mazungumzo kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuimarisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD). Aidha, Waziri Omar amesema Serikali itaboresha mifumo ya TEHAMA inayosimamia mapato kwa kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo uchambuzi wa taarifa kubwa (Big Data), sambamba na kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali ili kuongeza uwazi, ufanisi na tija katika ukusanyaji wa mapato. Pia, amesema Serikali itaongeza usimamizi wa taasisi za umma ili ziweze kuchangia zaidi mapato ya Serikali kupitia gawio na michango inayowasilishwa kwa wakati katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Katika hatua nyingine, Serikali itaanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo 284 yaliyotolewa na Tume ya Rais ya Kuboresha Mfumo wa Kodi. Vilevile, bidhaa zote zinazozalishwa nchini zitatakiwa kuwa na misimbo pau (barcode) kwa lengo la kurahisisha ufuatiliaji wa bidhaa na kudhibiti upotevu wa mapato. Balozi Omar ametangaza pia kuanzishwa kwa programu mpya ya “Tuzo za Uzalendo” itakayozinduliwa rasmi Julai ,2026 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari kupitia mfumo wa risiti za kielektroniki na droo za bahati nasibu. Amesema hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa uzalendo katika ulipaji wa kodi, kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda mapato ya taifa na kuimarisha uwajibikaji katika shughuli za biashara pia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kupunguza utegemezi wa mikopo na kuimarisha msingi wa uchumi unaojitegemea, shindani na wenye uwezo mkubwa wa kugharamia maendeleo ya wananchi.