Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Kituo Cha Habari

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Mageuzi ya kidijitali katika sekta ya ununuzi wa umma yanaendelea kuleta matokeo makubwa nchini kupitia mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) ambao umekua mkombozi kwa watoa huduma na Serikali, ukiimarisha uwazi, uwajibikaji na ushindani katika matumizi ya fedha za umma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Dennis Simba anabainisha hayo katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma lililowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi wa ununuzi wa umma na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hilo lililofanyika jijini Arusha lililoogozwa na kaulimbiu isemayo “Kutumia Fursa ya Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani kuelekea Dira ya Taifa 2050,” limeonesha kuwa ununuzi wa umma si shughuli ya kiutawala pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ushindani wa biashara na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija. Mkurugenzi huyo wa PPRA anaeleza kuwa tangu kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huo, Julai 1, 2023, uendeshaji wa shughuli za ununuzi nchini kwa kiasi kikubwa umebadilika kwa kuwa mfumo huo unawezesha usajili wa wazabuni, uchakataji wa zabuni kwa njia ya mtandao, usimamizi wa mikataba, malipo ya mikataba, minada ya kielektroniki pamoja na matumizi ya katalogi ya bidhaa na huduma. Mbali na kurahisisha utoaji wa huduma, Bw. Simba anasema PPRA imeendelea kuuboresha mfumo huo kwa kuanzisha moduli ya kisasa ya ufuatiliaji wa vihatarishi katika michakato ya ununuzi kwa wakati halisi. Teknolojia hiyo inaiwezesha Mamlaka kubaini mapema viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa fedha za umma au kukiukwa kwa taratibu za ununuzi, ikiwemo upangaji wa matokeo ya zabuni, ushindani usioridhisha, kula njama kati ya wazabuni na vitendo vya udanganyifu. Anasema hatua hiyo imeongeza uwezo wa PPRA kuchukua hatua za haraka kabla dosari hazijasababisha hasara kwa Serikali, huku ikiimarisha uadilifu na uwazi katika mnyororo mzima wa ununuzi wa umma. Mafanikio ya matumizi ya NeST yameonekana kupitia ongezeko la ushiriki wa wadau ambapo hadi Juni 30, 2026, zaidi ya wazabuni 45,270 walikuwa wamesajiliwa katika mfumo huo, huku asilimia 95 wakiwa wazabuni wa ndani. Aidha, zaidi ya taasisi nunuzi 62,847 na watumiaji zaidi ya 161,704 walikuwa wakitumia mfumo huo. Anasema katika kipindi hicho, zabuni 286,903 zilitangazwa kupitia NeST na zaidi ya tuzo za zabuni 181,057 zenye thamani ya shilingi trilioni 14.5 zikatolewa kwa njia ya mfumo huo, hatua inayoonesha kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika kusimamia fedha za umma. Aidha, ameeleza kuwa PPRA imeendelea kuwezesha ushiriki wa makundi maalumu katika fursa za zabuni. Kupitia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, Taasisi Nunuzi zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Matokeo ya utekelezaji huo yanaonekana ambapo hadi Julai 28, 2026 zaidi ya makundi maalumu 23,590 yalikuwa yamesajiliwa katika NeST na tuzo 745 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 53.68 zilitolewa kwa makundi maalumu. Hii inaonesha kuwa mageuzi ya kidijitali hayajaboresha tu ufanisi wa Serikali, bali pia yamepanua fursa za kiuchumi kwa makundi yaliyokuwa hayashiriki kwa kiwango kikubwa hapo awali. Mbali na manufaa ya kiuchumi, matumizi ya NeST yamechangia pia utunzaji wa mazingira. Utafiti wa PPRA unaonesha kuwa matumizi ya mfumo huo yalipunguza uzalishaji wa metariki tani 64,028 za hewa ya ukaa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kutokana na kupungua kwa matumizi ya karatasi. Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambulika kimataifa. Mfumo wa NeST umepata tuzo mbalimbali za ubunifu na mazingira, ikiwemo kutajwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali duniani katika tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026 zilizofanyika Geneva, Uswizi. Sambamba na mafanikio hayo, PPRA imeendelea kuimarisha ukaguzi wa ukidhi na thamani halisi ya fedha ili kuhakikisha taasisi zote zinazingatia sheria na taratibu za ununuzi wa umma. Jitihada hizo zinaenda sambamba na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza uwajibikaji, kudhibiti mianya ya ubadhirifu na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi. Kadhalika, Mamlaka hiyo imeendelea kupanua ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi kupitia kubadilishana uzoefu katika ununuzi endelevu, huku nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Benki ya Dunia zikiendelea kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kujenga na kutumia Mfumo wa NeST. Kwa ujumla, mafanikio ya PPRA yanaonesha kuwa uwekezaji katika mifumo ya kidijitali si tu umeongeza uwazi na ufanisi wa ununuzi wa umma, bali pia umeifanya sekta hiyo kuwa chombo muhimu cha kukuza uchumi shindani, jumuishi na endelevu. Kadiri matumizi ya NeST yanavyoendelea kuongezeka, ndivyo nafasi ya ununuzi wa umma katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inavyozidi kuimarika.

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Mkoa wa Kigoma umekuwa na nafasi ya kimkakati katika biashara ya kikanda kutokana na mwambao wake katika Ziwa Tanganyika na ukaribu wake na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia. Hata hivyo, changamoto za miundombinu ya usafirishaji zimekuwa zikizuia mkoa huo kutumia kikamilifu fursa hiyo, huku gharama za usafirishaji zikiwa kubwa na safari za mizigo kuchukua muda mrefu. Sasa hali hiyo imeanza kubadilika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora–Kigoma, uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na maboresho ya Bandari ya Kigoma. Miradi hiyo inatarajiwa kuibadili Kigoma kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari. Katika kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uchukuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua meli nne mpya za mizigo, akaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Tabora–Kigoma na kukagua maendeleo ya maboresho ya Bandari ya Kigoma. Hatua hizo zinaakisi mkakati wa Serikali wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara. Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, anasema Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia kutokana na nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika. Anasema kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. “Kwa nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika, Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia. Miradi hii ya SGR na meli mpya za mizigo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema Prof. Mbarawa. Meli hizo nne mpya, ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo, zinatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Kigoma kuhudumia zaidi ya tani 832,000 za mizigo kwa mwaka. Mbali na kuongeza ufanisi wa usafirishaji, uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea biashara na kuzalisha takribani ajira 600 za moja kwa moja katika sekta mbalimbali. Kwa wakazi wa Kigoma, uwekezaji huo una maana zaidi ya kujengwa kwa miundombinu. Ni mwanzo wa zama mpya za fursa za kiuchumi, ajira na uwekezaji. Kuimarika kwa usafiri wa reli na majini kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupanua masoko na kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi. Bi. Asha Mussa, mkazi wa Kibirizi, anasema wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu maendeleo ya aina hiyo. “Tunaamini meli mpya na reli ya kisasa zitafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi. Kuimarika kwa miundombinu ya usafiri kutasaidia wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali kupata nafasi zaidi za kujikwamua kiuchumi.” Hisia kama hizo zinaungwa mkono na wananchi wengi wanaoamini kuwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya usafirishaji kwa miaka mingi. Bw. John Mwakalinga, mkazi wa Kigoma Mjini, anasema gharama kubwa za usafirishaji zimekuwa zikikwamisha biashara na kupunguza ushindani wa bidhaa katika masoko. “Kwa miaka mingi usafirishaji wa bidhaa ulikuwa na changamoto nyingi na gharama kubwa. Tunaamini SGR pamoja na maboresho ya bandari utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda masoko ya ndani na nchi jirani, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara na kuinua kipato cha wananchi.” Mradi wa Reli ya Kisasa wa Tabora–Kigoma wenye urefu wa kilometa 506 unajengwa kwa gharama ya takribani dola za Marekani bilioni 2.7. Mradi huo utaunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa unaofika Dar es Salaam, hivyo kuimarisha Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Zambia. Faida za miradi hiyo hazitaishia katika kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria pekee. Pia zinatarajiwa kuongeza ushindani wa biashara za kikanda, kuvutia uwekezaji, kuchochea uzalishaji wa bidhaa na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kadri miradi hiyo inavyoendelea kukamilika, Kigoma inaelekea kujidhihirisha kama kitovu kipya cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati. Uwekezaji wa Serikali katika reli, bandari na usafiri wa majini unaweka msingi imara wa maendeleo endelevu, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi. Kwa hakika, kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, kuanza kwa huduma za meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi. Kigoma itaimarika kama lango kuu la biashara katika ukanda huu, huku Tanzania ikiendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara Afrika Mashariki na Kati.

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Kwa miaka mingi, wakazi wa Chamwino na maeneo jirani mkoani Dodoma wameishi na simulizi moja inayofanana; kuamka alfajiri kutafuta maji, kusubiri kwa saa nyingi kwenye foleni au kuishi kwa mgao wa maji usiotabirika. Leo, simulizi hiyo inaelekea kuwa historia kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji miji 28 Chamwino, unaotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika huduma ya maji. Mradi huu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17 unatekelezwa katika Wilaya ya Chamwino na unatarajiwa kuhudumia wakazi wa kata za Chamwino, Msanga, Buigiri, Chinangali pamoja na maeneo ya karibu ikiwemo Mtumba na Ihumwa. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kutekeleza miradi ya maji katika miji 28 Tanzania Bara, ukiwa na lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika. Ujenzi wa mradi ulianza Aprili mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Agosti, 2026 ambapo hadi sasa, utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 74, huku baadhi ya maeneo tayari yakiwa yameanza kupata huduma ya maji. Kwa wakazi wa Chamwino, mradi huu si tu ujenzi wa miundombinu, bali ni ukombozi wa maisha yao ya kila siku. “Kiukweli, hapo nyuma maji hayakuwa yanatosha. Serikali imetukumbuka. Mradi mkubwa wa namna hii kwa sisi tuliopitia ugumu wa maji kwa muda mrefu ni jambo la kujivunia na la kushukuru sana,” anasema Bi. Maila Nyembela, mkazi wa Chamwino Ikulu. Licha ya mradi kutokamilika, tayari umeanza kuonesha matokeo chanya. Huduma ya maji sasa inapatikana kwa wastani wa saa 22 kwa siku, hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa mgao wa maji uliokuwa ukiwasumbua wakazi kwa miaka mingi. Kwa wanawake, ambao kwa muda mrefu walibeba jukumu kubwa la kutafuta maji, mradi huu umeleta matumaini mapya. “Awali tulilazimika kuamka alfajiri kutafuta maji au kununua kwa gharama kubwa. Ilikuwa tabu sana, hasa kwa wanawake. Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha maisha ya familia zetu na kutupa muda zaidi wa kushiriki shughuli za maendeleo,” anasema Bi. Mluka Michael, mkazi wa Chamwino. Mratibu Msaidizi wa Mradi huu kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Titho Alex, anaeleza kuwa mradi huo umejumuisha ujenzi wa visima virefu nane, matenki mawili ya kuhifadhi maji pamoja na miundombinu ya kutibu, kusukuma na kusambaza maji. Anasema tanki moja lililopo Chamwino Ikulu lina uwezo wa kuhifadhi maji lita 500,000 , huku lingine lililopo Msanga likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 200,000. “Mkakati huu utawezesha mradi kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku, kiwango kitakachohakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa saa 22 hadi 24 kila siku na kuondoa kabisa changamoto ya mgao wa maji Chamwino pamoja na kuimarisha huduma katika maeneo ya jirani,” anasema Mhandisi Alex. Kwa wananchi walioishi muda mrefu Chamwino, mradi huu ni ushahidi wa mabadiliko makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika Makao Makuu ya Nchi. “Nimeishi Dodoma tangu mwaka 1971. Wakati huo hatukuwa na maji kabisa. Baadaye yakaanza kupatikana lakini hayakutosha. Sasa karibu kila kitongoji kina maji, ingawa baadhi ya maeneo bado hupata kwa mgao. Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu ukikamilika tutapata maji kila siku. Hili ni jambo la kufurahisha sana,” anasema Mchungaji Anderson Ndoloji wa Mtaa wa Muungano. Meneja wa DUWASA Kanda ya Chamwino, Mhandisi Gray Mbalikila, anasema mradi huo utaongeza uwezo wa mamlaka hiyo kupanua huduma katika maeneo mapya yanayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la wakazi, biashara na taasisi mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma. “Tunajivunia hatua tuliyofikia. Mradi huu ukikamilika, Chamwino itakuwa na akiba ya kutosha ya maji hata kwa ajili ya kata za jirani. Huduma itaongezeka kutoka kiwango cha sasa cha takribani asilimia 91 hadi kufikia asilimia 100,” anasema. Mbali na kuboresha upatikanaji wa maji, mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali. Upatikanaji wa maji ya uhakika utaimarisha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama, kuongeza usafi wa mazingira, kukuza biashara ndogo na shughuli za uzalishaji, pamoja na kuboresha huduma katika shule na vituo vya afya. Kadri Dodoma inavyoendelea kukua kama Makao Makuu ya Serikali, mahitaji ya huduma za msingi yanaongezeka. Mradi wa Maji Miji 28 Chamwino ni moja ya miradi ya kimkakati inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama. Kukamilika kwa mradi huu hakutakuwa tu mwisho wa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wananchi wa Chamwino na maeneo jirani, bali kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ambapo maji yatakuwa si tena changamoto, bali chachu ya maendeleo.

■ Utekelezaji wake mbioni kukamilika ■ Wafanyabiashara wausubiri kwa hamu Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Ule msemo wa Kiswahili unaosema “Mgeni njoo, mwenyeji apone” unaendelea kupata uhalisia kupitia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali jijini Dodoma. Mbali na kuimarisha usafiri wa anga nchini, mradi huo tayari umeanza kuleta manufaa kwa wananchi kupitia ajira, biashara na fursa za uwekezaji, huku ukitarajiwa kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha uchumi na usafiri wa anga. Mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 370 unatarajiwa kukamilika Septemba 2026. Kwa sasa, ujenzi wa miundombinu umefikia asilimia 87.97, huku ujenzi wa majengo ukiwa umefikia asilimia 76.15. Ajira Zimefungua Milango ya Mafanikio Tangu ulipoanza mwaka 2022, mamia ya wakazi wa Dodoma wamepata ajira za muda na fursa za biashara zilizoongeza kipato cha familia zao. Mkazi wa Mpamaa, Maximilian Mwagike, ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo. Anasema alianza kuuza miwa kwa kutumia baiskeli, lakini kuongezeka kwa shughuli za ujenzi kulipanua soko lake kiasi cha sasa kutumia guta kusafirisha bidhaa zake. “Biashara hii imenibadilisha maisha. Nimeboresha makazi yangu, ninalipia watoto wangu ada za shule binafsi na nimepanua biashara yangu,” anasema Mwagike, ambaye pia amepata ajira ya usimamizi wa mazingira katika mradi huo. Kwa upande wake, Mama Juma, aliyekuwa mama wa nyumbani, anasema mradi ulimwezesha kuanzisha biashara ya kupika na kuuza chakula kwa wafanyakazi wa ujenzi. “Leo naweza kulipia watoto wangu ada za shule, nimeweza kununua pikipiki inayoniingizia kipato na nina uhakika wa kuendelea na biashara hata baada ya mradi kukamilika,” anasema. Mradi Wajenga Ujuzi kwa Vijana Mbali na ajira za moja kwa moja, mradi huu umechangia kuwajengea vijana ujuzi na uzoefu wa kazi. Adam Kiula, anayefanya kazi katika kampuni inayosimika mifumo ya TEHAMA, kamera za usalama na mawasiliano, anasema amepata maarifa na uzoefu unaomuwezesha kushindana katika soko la ajira. Anawahimiza vijana kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali badala ya kusubiri ajira za kawaida. Wafanyabiashara Wanatazamia Mapinduzi ya Uchumi Faida za uwanja huo zinatarajiwa kuonekana zaidi baada ya kuanza kutoa huduma. Mfanyabiashara wa vifaa vya simu jijini Dodoma, anayefahamika kwa jina la Jeshi, anasema uwanja huo utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama zinazotokana na kupitisha bidhaa kupitia Dar es Salaam. Naye mfanyabiashara wa bidhaa za urembo, Happiness Mgeani, anaamini kukamilika kwa uwanja huo kutapunguza hasara zinazotokana na ucheleweshaji na uhamishaji wa mizigo kutoka usafiri mmoja kwenda mwingine. Uwanja wa Hadhi ya Kimataifa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, anasema kazi zilizobaki ziko katika hatua za mwisho za ukamilishaji, zikiwemo ufungaji wa mifumo mbalimbali, taa za kuongozea ndege, alama za barabara za ndege na umaliziaji wa majengo. Anasema uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kimataifa na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kama Airbus A330 na Boeing 787 Dreamliner, pamoja na kuhudumia (maegesho) ndege 17 kwa wakati mmoja. Aidha, anaeleza kuwa uwanja huo utakuwa na mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, mnara wa pili kwa urefu Afrika Mashariki, pamoja na maeneo ya biashara, maegesho ya magari na nafasi ya upanuzi wa baadaye. Maandalizi ya Uendeshaji Yamekamilika Kwa upande wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Zacharo Mduma amesema maandalizi ya kuanza uendeshaji wa uwanja huo yanaendelea, ikiwa ni pamoja na kuandaa watumishi watakaotoa huduma za uhamiaji, forodha, afya, usalama na zimamoto mara baada ya mradi kukabidhiwa rasmi. Lango Jipya la Ukuaji wa Uchumi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unatarajiwa kuwa wa Daraja F, kiwango cha juu kinachotambulika kimataifa. Mradi huo umefadhiliwa kwa asilimia 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku Serikali ya Tanzania ikichangia asilimia 15. Baada ya kukamilika, uwanja huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kuwa lango jipya la biashara, utalii na uwekezaji. Zaidi ya miundombinu ya usafiri, Uwanja wa Ndege wa Msalato unatajwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, huku ukiendelea kuthibitisha kwamba miradi mikubwa ya maendeleo inaweza kubadili maisha ya wananchi hata kabla haijakamilika.

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limeidhinisha kutolewa mara moja kwa takriban dola za Marekani milioni 443.9 kwa Tanzania baada ya kukamilisha tathmini za mwisho chini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience and Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika taarifa iliyotolewa Julai 10, IMF imesema uamuzi huo unafuatia kukamilika kwa mapitio ya sita na saba ya mpango wa ECF pamoja na mapitio ya tatu na nne ya mpango wa RSF, ambapo fedha hizo zinajumuisha takriban dola za Marekani milioni 158.75 chini ya ECF na dola za Marekani milioni 298.37 chini ya RSF. IMF imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara, huku ukuaji wa Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na kutarajiwa kufika karibu asilimia 6.2 kwa muda wa kati. Sekta zilizotajwa kuchangia matarajio hayo ni pamoja na madini, kilimo na utalii. Kwa mujibu wa tathmini hiyo, Tanzania imeendelea kudumisha utulivu wa uchumi mpana na mfumuko wa bei umebaki chini, ukiwa asilimia 4.0 mwezi Juni 2026. Hata hivyo, IMF imeonya kuwa kupanda kwa bei za mafuta duniani kunaendelea kutoa shinikizo kwa gharama za maisha na uchumi kwa ujumla. Taarifa hiyo imeonyesha pia kuwa utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kiuchumi kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Vigezo vingi vya utendaji vilifikiwa kwa wakati, ingawa baadhi ya malengo na mageuzi, hasa katika maeneo ya nishati, usimamizi wa VAT, utawala wa Benki Kuu na uwekezaji wa umma, yalichelewa au hayakukamilika kama ilivyotarajiwa. Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Bo Li, alisema Tanzania imefanikiwa kuhifadhi utulivu wa uchumi licha ya misukosuko ya ndani na nje. Alisema hatua zaidi zinahitajika katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha za umma, na kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu kama elimu na afya. Aidha, IMF imeishauri Tanzania kuendelea na mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha sekta binafsi, na kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Shirika hilo limeonya kuwa kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati kunaweza kudhoofisha ukuaji wa uchumi na kuongeza mfumuko wa bei. Pamoja na mtazamo chanya wa uchumi, IMF imesisitiza kuwa Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa za kupunguza umaskini, kufikia malengo ya maendeleo endelevu, na kuandaa fursa za kutosha kwa idadi ya watu inayotarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050. Kwa ujumla, uamuzi wa IMF unaonekana kuwa ishara ya kuendelea kwa imani ya taasisi hiyo kwa mwenendo wa uchumi wa Tanzania, huku ukitoa msukumo mpya kwa Serikali kuharakisha mageuzi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi. Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameshukuru uamuzi huo wa Taasisi hiyo kubwa ya Fedha duniani (IMF), kwa kuendelea kuamini mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi imeendelea kupiga hatua kubwa hadi sasa na kuungwa mkono na IMF. Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu ilipojiunga na IMF tarehe 10 Septemba 1962, ambapo jumla ya ahadi ya mikopo na misaada ya IMF kwa Tanzania imefikia Dola ya Marekani bilioni 4.578. Kati ya kiasi hicho, portfolio hai ya sasa ni dola za Marekani bilioni 2.52.

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa Ithibati ya Maisha utakaowezesha waandishi wa habari wakongwe waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari nchini kutambuliwa rasmi, licha ya kutokukidhi vigezo vya kielimu vilivyowekwa na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016. Uzinduzi wa mwongozo huo umetajwa kuwa hatua muhimu ya kutambua mchango wa wanahabari waliolitumikia taifa kwa uadilifu na weledi kwa miaka mingi kabla ya kuanza kutumika kwa masharti mapya ya kitaaluma yanayomtaka mwandishi wa habari kuwa na angalau stashahada (Diploma) ya uandishi wa habari. Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya JAB, uliofanyika Julai 11, 2026 katika kijiji cha Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo katika viwanja vya Maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara Dar es salaam (sabasaba) Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Tildo Mhando, kupitia taarifa iliyosomwa na Dkt. Egbert Mkoko, alisema mwongozo huo unalenga kuwapa Ithibati ya Maisha waandishi wa habari wakongwe ambao wakati Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ilipopitishwa mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi na walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika sekta ya habari. Alieleza kuwa waandishi hao hawakupata fursa ya kusomea darasani hadi kufikia kiwango cha diploma, lakini walijijengea uwezo kupitia uzoefu na walishiriki kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya vyombo vya habari na ujenzi wa taifa. “Mwongozo huu unalenga kuhifadhi historia ya tasnia ya habari, kuthamini mchango wa waandishi wa kizazi cha mwanzo na kuhakikisha uzoefu wao unaendelea kuwa sehemu ya urithi wa taaluma hii” ilisisitiza taarifa hiyo. Aidha, aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kushirikiana na JAB katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na kusisitiza umuhimu wa weledi, uwajibikaji na maadili kwa waandishi wa habari nchini. Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Bwana Patrick Kipangula alisema kuwa uzinduzi wa Mwongozo wa Ithibati ya Maisha ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kuhakikisha kuwa ni pamoja na kuimarisha viwango vya taaluma kupitia sheria, mchango wa waandishi wa habari wakongwe waliolitumikia taifa kwa uaminifu na uzalendo unaendelea kutambuliwa na kuthaminiwa.