Na Scolastica Sambi – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani kuongeza nguvu katika utoaji wa haki nchini na kuwasisitiza kuwa dhamana waliyopewa ni kubwa kwa mustakabali wa Taifa na ustawi wa wananchi. Akizungumza wakati wa kuwaapisha majaji hao, tarehe 26 Mei, 2026, Ikulu Dar es Salaam, Rais, Dkt. Samia amesema uteuzi wao umetokana na uzoefu, weledi pamoja na utumishi mzuri waliouonyesha katika nafasi mbalimbali walizowahi kuzitumikia ndani ya mhimili wa Mahakama. Amesema hatua ya kupandishwa kwao ni ishara kuwa kazi zao zimetambuliwa na kuthaminiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, jambo linaloonyesha imani kubwa waliyopewa katika kusimamia haki za Watanzania. “Nendeni mkatumikie nchi kwa uadilifu, weledi na uzalendo kama mlivyoapa hapa. Dhamana hii si ya cheo tu, bali ni wajibu wa kulinda haki za wananchi,” amesema Rais Samia. Katika hotuba yake, Rais Samia amesema kazi ya jaji ni miongoni mwa majukumu yenye uzito mkubwa katika jamii kwa sababu ndiyo yanayogusa moja kwa moja maisha, haki na matumaini ya wananchi. “Ukimuacha Mungu anayesimamia haki za wote, basi wengine aliowateua kusimamia haki za wananchi ni ninyi majaji. Hivyo mnafanya kazi yenye dhamana kubwa kwa Taifa,” amesisitiza. Aidha, aliwataka majaji hao kuhakikisha wanaitunza heshima na uhuru wa mahakama kwa kutoa maamuzi yanayozingatia sheria, haki pamoja na maslahi mapana ya Taifa, huku akieleza kuwa Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya juu kabisa ya utoaji haki nchini. Rais Samia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mhimili wa mahakama kupitia maboresho mbalimbali ili kuhakikisha taasisi hiyo muhimu inaendelea kutoa haki kwa ufanisi, weledi na kwa wakati.