Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO.  Serikali imebainisha mikakati mipya ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa taifa kujitegemea kiuchumi na kugharamia maendeleo kupitia rasilimali zake. Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Juni 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya juhudi za kujitegemea kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali. “Ni muhimu kuendelea kuimarisha uwezo wa nchi kugharamia maendeleo yake kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mikopo na changamoto zake,” amesema Balozi Omary. Amefafanua kuwa kupitia Mkakati wa Ukusanyaji wa Mapato wa Muda wa Kati wa mwaka 2025/26 hadi 2027/28, Serikali itaanza kutekeleza hatua mbalimbali zitakazopanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya ndani. Miongoni mwa hatua hizo ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza shughuli za kiuchumi, ajira na mapato ya kodi. Serikali pia itaendelea kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kupitia majukwaa ya mazungumzo kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuimarisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD). Aidha, Waziri Omar amesema Serikali itaboresha mifumo ya TEHAMA inayosimamia mapato kwa kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo uchambuzi wa taarifa kubwa (Big Data), sambamba na kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali ili kuongeza uwazi, ufanisi na tija katika ukusanyaji wa mapato. Pia, amesema Serikali itaongeza usimamizi wa taasisi za umma ili ziweze kuchangia zaidi mapato ya Serikali kupitia gawio na michango inayowasilishwa kwa wakati katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Katika hatua nyingine, Serikali itaanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo 284 yaliyotolewa na Tume ya Rais ya Kuboresha Mfumo wa Kodi. Vilevile, bidhaa zote zinazozalishwa nchini zitatakiwa kuwa na misimbo pau (barcode) kwa lengo la kurahisisha ufuatiliaji wa bidhaa na kudhibiti upotevu wa mapato. Balozi Omar ametangaza pia kuanzishwa kwa programu mpya ya “Tuzo za Uzalendo” itakayozinduliwa rasmi Julai ,2026 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari kupitia mfumo wa risiti za kielektroniki na droo za bahati nasibu. Amesema hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa uzalendo katika ulipaji wa kodi, kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda mapato ya taifa na kuimarisha uwajibikaji katika shughuli za biashara pia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kupunguza utegemezi wa mikopo na kuimarisha msingi wa uchumi unaojitegemea, shindani na wenye uwezo mkubwa wa kugharamia maendeleo ya wananchi.