Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Baraka Messa – Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali na Taasisi za Umma kuongeza ubunifu na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuangazia zaidi uwekezaji unaofanywa na Serikali na matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi. Msigwa ametoa wito huo Septemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwakaribisha na kuwapa maelekezo Maafisa Habari wapya walioajiriwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba. Amesema wajibu wa Maafisa Habari ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kwa wakati hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, maji, nishati, usafiri, teknolojia na sekta nyingine zinazogusa maisha yao. Kazi yetu ni kuhabarisha wananchi. Tueleze Serikali imefanya nini, inafanya nini na inatarajia kufanya nini, kwa sababu hayo ndiyo mambo yanayowagusa wananchi. Amesema katika kutekeleza wajibu huo, Maafisa Habari wanapaswa kuwasilisha taarifa zinazoonesha kwa uwazi uwekezaji uliofanyika, miradi inayotekelezwa, thamani ya uwekezaji huo, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, ili wananchi waweze kutambua namna rasilimali za Serikali zinavyotumika katika kuleta maendeleo. Msigwa amesema taarifa za utekelezaji wa Serikali zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza tukio, badala yake zioneshe maana ya mradi kwa mwananchi, ikiwemo huduma zitakazopatikana, fursa zitakazozalishwa, ajira zitakazoongezeka na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Amesema Maafisa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mipango na vipaumbele vya Serikali, pamoja na kutambua hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili. Taarifa nzuri si ile inayosema tu mradi umejengwa, bali ieleze mradi huo umejengwa kwa gharama gani, unahudumia wananchi wangapi na umeleta mabadiliko gani katika maisha yao. Aidha, amewataka Maafisa Habari kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa na majukwaa ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, katika kufikisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto na inayoeleweka kwa makundi mbalimbali. Amesema matumizi ya teknolojia yanatoa fursa ya Serikali kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo Maafisa Habari wanapaswa kutumia ubunifu katika kuandaa maudhui yanayowapa wananchi uelewa wa shughuli, miradi na uwekezaji unaofanywa na Serikali. Vilevile, Msigwa amewataka Maafisa Habari hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji na maslahi mapana ya umma. Amesema Maafisa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinajenga uelewa kuhusu maendeleo yanayotekelezwa na Serikali na kuwasaidia wananchi kutambua fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo. Msigwa amesisitiza kuwa, kupitia taarifa sahihi, zenye ushahidi na zinazoonesha matokeo, Maafisa Habari wanaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa na mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanawasikiliza, wanatatua kero zao na kutoa huduma bora kwa ufanisi. Rais Samia ametoa wito huo Septemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, akisisitiza kuwa nafasi walizopewa si fursa ya kujinufaisha, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi ya Taifa. Amewakumbusha viongozi hao kuwa wao ni watumishi wa wananchi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi. Rais Samia amewasisitiza viongozi hao kuwa utumishi wa umma ni kuwa tayari kuwatumikia wananchi waliokupa dhamana hiyo, kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya nchi. Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za mikoa na wilaya zinapatiwa majibu na hatua stahiki kwa wakati. Amesema uongozi wa aina hiyo utasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na kuhakikisha huduma za umma zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi. Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawahitaji viongozi wanaosubiri kero zifikishwe ofisini pekee bali wanahitaji viongozi wanaokwenda kwao, kusikiliza changamoto zao, kutafuta suluhisho na kusimamia utekelezaji ili matokeo yaonekane.

Na. Baraka Messa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuilinda na kuitunza miundombinu ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHP), akisema kuwa mradi huo ni mali ya Watanzania na urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Rais Samia amesema hayo  Agosti 22, 2026, wilayani Rufiji mkoani Pwani, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema kuwa Serikali imewekeza rasilimali kubwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme na kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa wananchi na kusisitiza kuwa jukumu la kulinda mradi huo si la Serikali pekee, bali ni la kila Mtanzania, kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa. Mradi huu ni wetu sote, Ni lazima tuulinde, tuutunze na tuhakikishe unaendelea kutoa manufaa kwa Watanzania wa leo na vizazi vijavyo,” amesema Rais Samia. Ameongeza kuwa Mradi wa JNHP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati nchini, hivyo akawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika katika kulinda miundombinu ya mradi huo. Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa megawati 2,115 kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya majumbani, viwandani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, uzinduzi  wa kituo hicho unafungua sura mpya katika safari ya Tanzania ya kuimarisha usalama wa nishati, huku Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa washiriki wakuu katika kulinda na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetoa rai kwa Watanzania, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kuunga mkono harambee maalumu ya kuchangia matibabu ya upandikizaji figo na uloto kwa wagonjwa wenye uhitaji, hususan watoto wenye ugonjwa wa selimundu. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Prof Abel Makubi amesema harambee hiyo ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo mwaka 2015, ambapo lengo ni kukusanya shilingi bilioni saba ndani ya kipindi cha miaka miwili ili kusaidia kuwatibu wananchi wasioweza kumudu gharama za matibabu hayo. Amesema hospitali hiyo imeendelea kukua na kuwa kituo kikubwa cha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini, ikiwa na wataalamu wa afya zaidi ya 100 na kutoa huduma 20 za ubingwa pamoja na huduma 18 za ubingwa bobezi. Baadhi ya huduma zinazotolewa ni upasuaji wa moyo, upandikizaji figo, upandikizaji uloto, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, pamoja na huduma nyingine za kisasa zinazopatikana ndani ya nchi. “Tangu kuanza kwa huduma za upandikizaji figo mwaka 2018, jumla ya wagonjwa 56 wamefanyiwa upandikizaji wa figo nchini hatua iliyookoa zaidi ya shilingi bilioni 1.7 ambazo zingetumika kama wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi”, amesema Prof. Makubi. “Vile vile huduma za upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu zilianza mwaka 2023 ambapo hadi sasa watoto 30 wamefanyiwa upandikizaji huo kwa mafanikio ikiwemo mtoto mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo huduma hizo zimeokoa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya Tanzania”, amemalizia Prof. Makubi. Prof. Makubi ameongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, gharama za matibabu ya upandikizaji figo na uloto bado ni kubwa kwa wananchi wengi jambo lililoifanya kuanzisha mfuko maalumu wa kusaidia wagonjwa wenye uhitaji kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Kwa niaba ya Hospitali hiyo, Prof. Makubi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya hususan katika kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hospitalini hapo.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, amesema kuwa ujio wa wanamichezo wa kimataifa nchini Tanzania akiwemo mchezaji na nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand unashawishi wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo. Bw. Msigwa ameeleza hayo Mei 20, 2026 wakati akiwa safarini na mwanamichezo huyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia treni ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini. Ameongeza  kuwa wachezaji wa kimataifa wanapokuja nchini wanaongeza macho ya wadau mbalimbali wa michezo kuitazama nchi ya Tanzania na kuona ni namna gani wataweza kuwekeza  na nchi itaweza kunufaika kwa kupata mitaji ya kuwekeza kwenye michezo, wataalam wa kushirikiana nao pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na fursa ziliozopo duniani kupitia sekta hiyo. “Ujio wa mwanamichezo huyu, unapeleka ujumbe duniani kwamba Tanzania imejidhatiti kufanya mambo makubwa kwenye sekta ya michezo hivyo kupitia wao, nchi itafanikiwa kushawishi uwekezaji katika sekta ya michezo kwani nchi yetu ina changamoto kubwa kwenye eneo la uwekezaji hasa kwenye miundombinu ya michezo pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo jezi za wachezaji, viatu, mipira ambavyo tunaagiza kutoka nje. Vile vile, tunahitaji wataalam wa michezo ambao wataleta ujuzi wa namna ya kutengeneza viwanja.” Amesema Msigwa. Kwa upande wake, Mchezaji na Nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand amesema kuwa mpira wa miguu ukitumika vizuri unaweza kufungua fursa mbalimbali pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.  Amesema kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda pamoja na wadau wa sekta ya utalii ili kuongeza hamasa na ufuatiliaji wa sekta hiyo.