Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani wa kugharamia, kusimamia na kuzalisha mahitaji muhimu ya huduma za afya, badala ya kuendelea kutegemea misaada na mifumo kutoka nje. Dkt. Mwigulu ameyasema hayo, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, ukishirikisha zaidi ya washiriki 2,700 kutoka mataifa 27. Amesema wakati umefika kwa Afrika kubadili namna inavyoelewa na kutekeleza dhana ya kujenga uwezo, akisisitiza kuwa dhana hiyo haipaswi kuishia katika miradi midogo isiyojenga uwezo wa kudumu, bali ielekezwe katika uwekezaji wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia na wataalamu. Enzi zile nikiwa Waziri wa Fedha nilikuwa nawaambia nchi za Afrika zimeshashuhudia muda mrefu sasa wa maisha ya misaada na misaada inayoelekezwa pengine katika maeneo ambayo yanatofautiana na malengo ya ndani ya nchi kwa jina la capacity building. Capacity building. Capacity building. Na ndio tunaishia chapati, mandazi, sambusa. Hatuwekezi kitu kitakachodumu na kikawa endelevu. Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, malengo ya ndani ya nchi yanayokwenda sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuheshimiwa na washirika wa maendeleo, ili misaada na uwekezaji katika sekta ya afya viweze kuacha matokeo ya kudumu kwa wananchi wa Afrika. Amesema Tanzania inaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza miundombinu, rasilimali watu pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambayo Serikali imeanza kuitekeleza mwaka 2026. Tunapozungumza kuhusu afya ya msingi, tusizungumzie tu kujenga vituo vya afya. Tujenge pia uwezo wa nchi zetu kugharamia huduma hizo, kuzalisha mahitaji yake na kutumia teknolojia zetu wenyewe. Ameongeza kuwa Tanzania imeanza kuwekeza katika uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa kwa lengo la kupunguza utegemezi wa misaada na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuwa wa uhakika, hususan wakati dunia inapokumbwa na changamoto zinazoathiri minyororo ya usambazaji. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza ajira katika sekta hiyo, hatua ambazo zitasaidia kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Dkt. Mwigulu amesema mkutano huo unapaswa kuzaa hatua mahsusi zinazoweza kutekelezwa na kupimwa, badala ya kuishia katika mijadala na maazimio yasiyotekelezwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, amesema Afrika ya mwaka 2026 si Afrika ya mwaka 1960 na kwamba wakati umefika kwa washirika wa maendeleo kubadili namna wanavyoshirikiana na Serikali za Afrika. Dkt. Kaseya amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuwa na umiliki na uelewa wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya afya, huku fedha za washirika wa maendeleo zikiendana na mipango na vipaumbele vya kitaifa. Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohammed Janabi, amesema changamoto kubwa kwa Afrika si kukosa suluhisho katika sekta ya afya, bali ni kukosa ujasiri wa kuyafadhili, nidhamu ya kuyatekeleza na uwajibikaji wa kuyadumisha. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuwa ndiyo ngazi inayohudumia wananchi wengi zaidi nchini. Amesema asilimia 95.6 ya wajawazito wanaojifungua nchini wanapata huduma katika ngazi ya afya ya msingi, huku asilimia 86 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma yakihudumiwa katika ngazi hiyo. Profesa Shemdoe amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya afya ya msingi, hivyo kuongeza uwekezaji katika ngazi hiyo ni kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kwa wananchi wengi nchini. Mkutano huo wa siku tatu unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kupitia ufadhili endelevu, ufanisi, ubora wa huduma, ubunifu, ushirikiano wa kikanda na kujenga mifumo ya afya inayostahimili majanga. Kwa ujumla, mkutano huo unalenga kuhimiza Afrika kujenga mifumo ya afya inayojitegemea, yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, huku ikiweka mkazo katika uwekezaji wa muda mrefu, uzalishaji wa ndani, rasilimali watu na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali takribani Shilingi bilioni 121.99 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi, baada ya kuwapatia wagonjwa 2,282 huduma za ubingwa na ubingwa bobezi katika mwaka wa fedha 2025/26.   Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Taasisi hiyo ilihudumia jumla ya wagonjwa 211,359, wakiwemo wagonjwa 202,000 wa nje na 9,359 waliolazwa. Amesema kuimarishwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa, kumeiwezesha MOI kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97. Huduma zilizoboreshwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa teknolojia za kisasa, upasuaji kupitia matundu, tiba ya maumivu, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, huduma za kiharusi, pamoja na upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua. Katika huduma za ubingwa bobezi, wagonjwa 2,282 walipatiwa matibabu yakiwemo upasuaji wa nyonga, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa hydrocephalus na scoliosis, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za Serikali. Aidha, amesema MOI imeendelea kuchangia ukuaji wa tiba utalii nchini, ambapo katika mwaka huo ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Balozi Dkt. Ulisubisya amesema uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na mifumo bora ya utoaji huduma umeifanya MOI kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania. Katika kuimarisha ubora wa huduma, asilimia 87.5 ya wagonjwa waliridhishwa na huduma walizopata, huku kiwango cha kuridhika kwa watumishi kikifikia asilimia 82 na ushughulikiaji wa malalamiko kufikia asilimia 90. Aidha, katika kipindi hicho MOI ilifanya vipimo 83,847 vya radiolojia, ikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384, huku wagonjwa 71,819 wakipatiwa huduma za tiba kwa mazoezi (fiziotherapia). Taasisi hiyo pia imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, zilizowafikia wagonjwa 18,455, ambapo 4,310 walifanyiwa upasuaji. Mafanikio hayo yamekwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD lenye thamani ya Shilingi bilioni 13.8, ukarabati wa MOI Annex, maboresho ya vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa, ukarabati wa ICU ya watoto pamoja na ujenzi wa tenki la Hewa Tiba ya Oksijeni lenye ujazo wa tani 10. Kuhusu mipango ya baadaye ya taasisi hiyo, Dkt. Ulisubisya amesema MOI itaendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa. Amesema pia Taasisi hiyo inaendelea kujiandaa kutoa huduma za afya kwa wanamichezo na wadau wengine wakati wa michuano ya AFCON 2027.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi, ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi kwenye afya hasa upande wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwani afya haijawahi kuwa gharama na ni uwekezaji ambao nchi inaweza kuona faida yake. Ametoa rai hiyo Juni 23, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika (ICPPA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam. Prof. Janabi amesema kuwa nchi inaweza kufanya magonjwa yasiyoambukiza kuwa kipaumbele cha maendeleo ya kitaifa kwa kutumia sera za kifedha zinazoweza kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na kodi kwenye tumbaku, pombe na bidhaa zote zenye sukari, kupanua ulinzi wa kifedha ili ugonjwa usimaanishe umaskini, kuongeza kiwango cha mpango wa Pen na Pen-Plus kitaifa pamoja na kuwalinda watoto kwa kutengeneza mazingira yenye afya bora. Tunaweza kuwa na vipaumbele vingi lakini tunasahau kuwa vipaumbele vinahitaji vitendo. Magonjwa yasiyoambukiza si tishio la baadaye tena katika bara letu bali ni ukweli wa sasa kwani yanasababisha asilimia 37 ya vifo. Magonjwa kamwe hayapaswi kuamua hatma ya mtu kwa sababu kila maisha ya Mwafrika yana thamani na utu sawa”, amesema Prof. Janabi. Akizungumzia kuhusu Pen-Plus, amesema kuwa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 20 na imeweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya 100,000 huku akisisitiza kuwa si miradi ya majaribio tu bali ina ushahidi kwani kupitia kuimarisha afya, watoto wanarudi shuleni, vijana wanaishi maisha marefu na akina mama wanajifungua salama na kuishi.  Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa Maendeleo, Bw. James Reid kutoka Mfuko wa Hisani wa Helmsley Charitable Trust ameeleza kuwa, kwa muda mrefu wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini kwenye ukanda wa Afrika, wanakabiliwa na changamoto zikiwemo za huduma za afya zisizofikika, kukosa wafanyakazi wa afya waliofunzwa na mifumo michache ya kuwahudumia wagonjwa hao pamoja na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, dawa au huduma za ufuatiliaji. “Tunahitaji kuendelea kupanua idadi ya nchi zinazohusika katika mtandao huu ili kufikia malengo ya kikanda ya nchi wanachama wa WHO. Tunahitaji kuendelea kujenga na kuimarisha nguvu kazi inayofanya huduma hii iwezekane, tunahitaji kufanya kazi pamoja na nchi husika ili kuhakikisha kuwa kuna ufadhili endelevu na kuhakikisha kuwa mfumo huu unaweza kuendelea kupanuka”, amemalizia Bw. Reid. PEN-Plus ni mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa NCDI Poverty unaolenga kupanua huduma za afya kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yaliyo sugu na makali. Mpango huu unapanua wigo wa huduma kutoka ngazi za chini ili wagonjwa wapate matibabu katika hospitali za wilaya au rufaa za ngazi ya kwanza bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeandika historia nyingine baada ya jopo la madaktari bingwa na wataalamu wa afya kufanikisha salama uzazi wa watoto watano kwa wakati mmoja kwa Bi. Victoria Mkwizu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam. Watoto hao ambao watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike, wamezaliwa tarehe 13 Juni 2026 na wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa wataalamu wa hospitali hiyo. Akiwa wodini, Bi. Victoria amesema anafurahia huduma alizopata katika hospitali hiyo tangu alipopokelewa hadi kujifungua. “Nawapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya kwa uangalizi wa karibu walionipatia katika kipindi chote cha matibabu kwani mchango wao umetuwezesha mimi na watoto kuendelea vizuri”, amesema Bi. Victoria. Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville amesema tukio hilo ni la kipekee na limehitaji ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa hospitali hiyo ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto huku akimpongeza Bi. Victoria kwa kujifungua salama na kuwatakia wote afya njema. Tunampongeza sana Bi. Veronica kwa kubarikiwa watoto mapacha watano, hospitali yetu itagharamia gharama zote za matibabu za kwake na watoto wake kuanzia alipolazwa hospitalini tarehe 15 Mei, 2026 hadi watakapomaliza matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani”, ameeleza Dkt. Rachel. Amefafanua kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za hospitali kuhakikisha mama na watoto wanaendelea kupata huduma bora na salama katika kipindi hicho.