Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Baraka Messa – MAELEZO Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya Wabunge wengi kuunga mkono mapendekezo ya matumizi na makusanyo ya Serikali yaliyowasilishwa bungeni. Akitoa matokeo ya kura zilizopigwa Juni 23, 2026, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema jumla ya wabunge 395 walihudhuria kikao hicho huku wabunge wanane wakikosekana. Mhe. Zungu amesema kati ya wabunge waliohudhuria, wabunge 385 walipiga kura za ndiyo, sawa na asilimia 97.26 ya kura zote zilizopigwa, huku wabunge wanane wakipiga kura za hapana. Matokeo hayo yamedhihirisha uungwaji mkono mkubwa wa bajeti hiyo kutoka kwa wajumbe wa Bunge. Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatoa idhini kwa Serikali kuendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo pamoja na shughuli za kawaida za kiutawala katika mwaka mpya wa fedha. Bajeti hiyo imelenga kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kuendeleza miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mipango ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza ustawi wa wananchi. Amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Prof. Mkumbo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochangia kuongezeka kwa uzalishaji na mapato ya taifa. Aidha, ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango na miradi iliyopangwa, ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania katika miaka ijayo.

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO.  Serikali imebainisha mikakati mipya ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa taifa kujitegemea kiuchumi na kugharamia maendeleo kupitia rasilimali zake. Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Juni 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya juhudi za kujitegemea kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali. “Ni muhimu kuendelea kuimarisha uwezo wa nchi kugharamia maendeleo yake kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mikopo na changamoto zake,” amesema Balozi Omary. Amefafanua kuwa kupitia Mkakati wa Ukusanyaji wa Mapato wa Muda wa Kati wa mwaka 2025/26 hadi 2027/28, Serikali itaanza kutekeleza hatua mbalimbali zitakazopanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya ndani. Miongoni mwa hatua hizo ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza shughuli za kiuchumi, ajira na mapato ya kodi. Serikali pia itaendelea kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kupitia majukwaa ya mazungumzo kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuimarisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD). Aidha, Waziri Omar amesema Serikali itaboresha mifumo ya TEHAMA inayosimamia mapato kwa kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo uchambuzi wa taarifa kubwa (Big Data), sambamba na kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali ili kuongeza uwazi, ufanisi na tija katika ukusanyaji wa mapato. Pia, amesema Serikali itaongeza usimamizi wa taasisi za umma ili ziweze kuchangia zaidi mapato ya Serikali kupitia gawio na michango inayowasilishwa kwa wakati katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Katika hatua nyingine, Serikali itaanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo 284 yaliyotolewa na Tume ya Rais ya Kuboresha Mfumo wa Kodi. Vilevile, bidhaa zote zinazozalishwa nchini zitatakiwa kuwa na misimbo pau (barcode) kwa lengo la kurahisisha ufuatiliaji wa bidhaa na kudhibiti upotevu wa mapato. Balozi Omar ametangaza pia kuanzishwa kwa programu mpya ya “Tuzo za Uzalendo” itakayozinduliwa rasmi Julai ,2026 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari kupitia mfumo wa risiti za kielektroniki na droo za bahati nasibu. Amesema hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa uzalendo katika ulipaji wa kodi, kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda mapato ya taifa na kuimarisha uwajibikaji katika shughuli za biashara pia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kupunguza utegemezi wa mikopo na kuimarisha msingi wa uchumi unaojitegemea, shindani na wenye uwezo mkubwa wa kugharamia maendeleo ya wananchi.