Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Samia Aagiza Kufanyika Utafiti Ongezeko la Saratani na Moyo kwa Watoto

June 24, 2026

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amevigiza vituo vya utafiti wa afya nchini kushirikiana na wabobezi wa tafitri duniani, kutafuta sababu za ongezeko la saratani na moyo kwa watoto wadogo ili kupata sababu zinazosababisha ongezeko la maradhi hayo na kutoa elimu kwa Watanzania ili kuepuka mambo yanayosababisha saratani kwa watoto.

Rais Samia ametoa maagizo hayo Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa huduma za tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC mjini Moshi,  na kueleza kuwa uwepo wa tiba mionzi katika Kanda ya Kaskazini, utasaidia kupunguza changamoto kwa wagonjwa wa saratani ambao awali walilazimika kwenda maeneo mengine yakiwemo Dar es Salaam kupata matibabu.

Hili ni suala la kuangalia kwa kina hasa watafiti wetu. Vituo vyetu vya watafiti wa afya kwa kushirikiana na waliotuzidi ujuzi duniani, tuzame kutafuta sababu zinazoleta ongezeko la maradhi hayo kwa watoto wetu na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ya Watanzania ili kuepuka yale yote yanayofanya tulete watoto wenye maradhi hayo duniani”, ameelekeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema ili kuimarisha huduma za afya nchini zikiwemo kinga, uchunguzi, na matibabu, Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika huduma hizo, ambapo imetoa shilingi bilioni 5.5 kusaidia kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

“Hospitali ya rufaa ya KCMC ina heshima kubwa hapa nchini na hata jirani kwa huduma bobezi na za kibingwa zinazotolewa hapa. Uzinduzi wa jengo hili la tiba mionzi ni hatua nyingine muhimu katika kusogeza huduma hizo karibu na wananchi”, ameeleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma kubwa za afya ikiwemo matibabu ya saratani na magonjwa ya moyo katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma karibu na wanapoishi na kwamba uwepo wa hospitali hiyo ya rufaa KCMC ni faraja kubwa kwa familia nyingi zilizokuwa zikibeba gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata matibabu.

Rais Samia amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za afya, taasisi za dini na mashirika ya maendeleo yaliyoshiriki katika kufanikisha mradi huo, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kituo hicho kwa sasa kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka na kikikamilika kitaweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 3,900 kwa mwaka.

Mhe. Mchengerwa amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama kwa familia, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini umeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya.

Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *