Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Baraka Messa- MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ( Sabasaba) yameendelea kuwa daraja muhimu linalowaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo ya 50 Julai 3,2026 jijini Dares Salaam amesema maonesho hayo yamekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania wengi, huku yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kukua na kuwa wawekezaji wakubwa kupitia upatikanaji wa masoko na mitaji. “Kwa karibu miaka 50, maonesho ya Sabasaba yamekuwa daraja la kuwaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji, huku yakiiunganisha Tanzania na dunia katika biashara na uwekezaji.” amesema. Amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku mafanikio hayo yakichangiwa na maboresho makubwa ya miundombinu na matumizi ya teknolojia yaliyofanywa na Serikali. Aidha, Rais Samia amesema diplomasia ya uchumi imeendelea kuzaa matunda ambapo katika mwaka uliopita mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yalifikia takribani dola za Marekani bilioni 17, sawa na ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na kipindi kilichopita. Pia, mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 35, yakionesha ukuaji wa sekta ya madini. Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, amesema Tanzania na Msumbiji zinapaswa kutumia historia yao ya ushirikiano kuimarisha uchumi wa kikanda kwa kubadilisha mipaka ya nchi hizo kuwa korido za maendeleo, biashara na uwekezaji badala ya kuwa vikwazo Amesema uchumi wa Tanzania na Msumbiji unakamilishana na una fursa kubwa ya kukuza minyororo ya thamani, biashara ya kikanda na uwekezaji kutokana na rasilimali nyingi, nguvu kazi ya vijana na nafasi ya kimkakati inayounganisha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitia Bahari ya Hindi. Aidha, Rais Chapo amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika waitazame Tanzania na Msumbiji kama washirika wa kuaminika wenye mazingira rafiki ya biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda, sayansi, ubunifu, uchumi wa kidijitali na akili Unde (AI).

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kujitegemea katika kugharamia shughuli za maendeleo kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani huku akieleza kuwa mchango wa makampuni, mashirika na taasisi za umma unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo. Rais Samia amesema hayo Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, Ikulu jijini Dar Es Salaam. Rais Samia ameeleza kuwa mafanikio hayo yatachangia kupunguza pengo la kujitegemea katika bajeti ya mwaka huu na kwa miaka miwili ijayo jambo linaloonyesha kuwa mikakati ya kuongeza mapato ya ndani imeanza kuzaa matunda. “Gawio na mchango uliotolewa na makampuni, taasisi na mashirika yetu ni sehemu ya lengo letu la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharamia shughuli za maendeleo” amesema Rais Samia Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa matumaini yataongezeka endapo kasi ya ukusanyaji wa mapato na ufanisi wa taasisi utaendelea kuimarika ndani ya miaka miwili ijayo, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kugharamia maendeleo yake kwa kutegemea vyanzo vya ndani pekee. Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amewaelekeza viongozi na watendaji wote kutoridhika na pongezi wanazopata, bali amewasisitiza kuwa, pongezi hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii, ubunifu na maarifa ili kufikia matokeo makubwa zaidi katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa mapato. Kadhalika, ameeleza kuwa maendeleo ya uchumi wa Taifa yanahitaji uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa rasilimali na juhudi endelevu kutoka kwa taasisi zote za umma ili kuhakikisha mchango wao unaendelea kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amevigiza vituo vya utafiti wa afya nchini kushirikiana na wabobezi wa tafitri duniani, kutafuta sababu za ongezeko la saratani na moyo kwa watoto wadogo ili kupata sababu zinazosababisha ongezeko la maradhi hayo na kutoa elimu kwa Watanzania ili kuepuka mambo yanayosababisha saratani kwa watoto. Rais Samia ametoa maagizo hayo Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa huduma za tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC mjini Moshi,  na kueleza kuwa uwepo wa tiba mionzi katika Kanda ya Kaskazini, utasaidia kupunguza changamoto kwa wagonjwa wa saratani ambao awali walilazimika kwenda maeneo mengine yakiwemo Dar es Salaam kupata matibabu. Hili ni suala la kuangalia kwa kina hasa watafiti wetu. Vituo vyetu vya watafiti wa afya kwa kushirikiana na waliotuzidi ujuzi duniani, tuzame kutafuta sababu zinazoleta ongezeko la maradhi hayo kwa watoto wetu na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ya Watanzania ili kuepuka yale yote yanayofanya tulete watoto wenye maradhi hayo duniani”, ameelekeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema ili kuimarisha huduma za afya nchini zikiwemo kinga, uchunguzi, na matibabu, Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika huduma hizo, ambapo imetoa shilingi bilioni 5.5 kusaidia kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi. “Hospitali ya rufaa ya KCMC ina heshima kubwa hapa nchini na hata jirani kwa huduma bobezi na za kibingwa zinazotolewa hapa. Uzinduzi wa jengo hili la tiba mionzi ni hatua nyingine muhimu katika kusogeza huduma hizo karibu na wananchi”, ameeleza Rais Samia. Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma kubwa za afya ikiwemo matibabu ya saratani na magonjwa ya moyo katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma karibu na wanapoishi na kwamba uwepo wa hospitali hiyo ya rufaa KCMC ni faraja kubwa kwa familia nyingi zilizokuwa zikibeba gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata matibabu. Rais Samia amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za afya, taasisi za dini na mashirika ya maendeleo yaliyoshiriki katika kufanikisha mradi huo, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini. Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kituo hicho kwa sasa kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka na kikikamilika kitaweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 3,900 kwa mwaka. Mhe. Mchengerwa amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama kwa familia, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini umeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya. Mwisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa ndege maalum kwa ajili ya kuwachukua mashujaa, Timu ya Taifa ya Vijana U-17 (Serengeti Boys) baada ya kufuzu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON U-17, 2026. Ndege hiyo imeondoka Juni 01, 2026 inatarajiwa kurejea Jumatano tarehe 3 Juni 2026. Msafara huo umeongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda (Mb.), akiambatana na viongozi wa serikali pamoja na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) ambao watatumia fursa hiyo kushiriki mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu zilizopo kwenye kalenda ya FIFA, kama sehemu ya maandalizi ya mashindano yajayo. Aidha, Waziri Makonda amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza kwenye michezo na kurahisisha safari hii. Ameziomba familia za Watanzania kuungana kuiombea na kuishangilia Serengeti Boys ili wailetee nchi Kombe la AFCON U-17 na kupeperusha bendera yetu kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto mchanga wa kike leo tarehe 11 Machi, 2026, katika makazi yake, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma. Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu, alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai. Akizungumza wakati wa kumkabidhi mtoto huyo, Mkuu wa Wilaya Tukai alisema mtoto huyo aliokotwa tarehe 17 Januari, 2026 akiwa ametelekezwa katika eneo jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, Nzega Mjini. Alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio. Rais Dkt. Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo. “Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” alisema Rais Dkt. Samia.

Dodoma. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kufikia lengo kuu la kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, la haki na linalojitegemea. Rais Dkt. Samia aliyasema hayo Alhamis, Julai 17, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa Dira uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC)—tukio ambalo pamoja na viongozi wengine lilihudhuriwa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu. Aidha, Rais Dkt. Samia alisema Dira 2050 ni matokeo ya mchakato jumuishi uliohusisha maoni ya wananchi na wadau wote na inalenga kufanikisha maendeleo jumuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Rais Dkt. Samia alisema Dira hiyo iliyozingatia matarajio ya Watanzania imejengwa juu ya msingi wa mafanikio na mafunzo ya historia ya maendeleo ya Tanzania tangu Uhuru, ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa Dira ya 2025. “Maudhui ya Dira 2050 yametokana na maoni na matakwa ya Watanzania wenyewe. Tumefikiri wenyewe, tumeandika wenyewe, tumepanga wenyewe na tutatekeleza wenyewe,” alisema Mhe. Rais. Rais Dkt. Samia alisema kuwa uandaaji wa Dira hii umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia. Aliongeza kuwa kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa $1 trilioni ifikapo mwaka 2050. alisema kuwa uandaaji wa Dira hii umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia. Aliongeza kuwa kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa $1 trilioni ifikapo mwaka 2050.