Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Netumbo: Kongwa Imebeba Historia ya  Uhuru wa Namibia

June 21, 2026

Na Baraka Messa- MAELEZO 

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema Tanzania itaendelea kuwa sehemu muhimu katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake mkubwa wa kuhifadhi na kusaidia wapigania uhuru waliowezesha taifa hilo kupata uhuru, akieleza kuwa Kongwa ni moja ya maeneo yenye thamani kubwa katika historia ya ukombozi wa Afrika.

Dkt. Nandi-Ndaitwah ametoa kauli hiyo Juni 21, 2026 alipotembelea eneo la kihistoria la Kambi ya Wapigania Uhuru wa Namibia wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katika ziara yake ya kwanza ya Kiserikali nchini Tanzania tangu aingie madarakani.

Amesema ziara hiyo imekuwa ya kipekee kwake na kwa wananchi wa Namibia kwa kuwa imewapa fursa ya kushuhudia kwa macho yao sehemu ambayo mashujaa wa taifa hilo waliwahi kuishi, kupata mafunzo na kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni.

Kongwa ni mahali Patakatifu pa ukombozi kwa sababu nchi nyingi zilizopigania uhuru zilipata hifadhi na mafunzo hapa. Mashujaa wetu wamelala mahali hapa na damu yao ilimwagilia uhuru wetu,”amesema.

Amewataka Watanzania na Wanamibia kuendeleza ushirikiano uliowekwa na waasisi wa mataifa hayo kwa kushirikiana katika kukamilisha ukombozi wa kiuchumi wa nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla ili kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi.

Akizungumzia umuhimu wa kuhifadhi historia hiyo, Rais Netumbo amesema ni wajibu wa kizazi cha sasa kuhakikisha mchango wa mashujaa wa ukombozi unaenziwa na kulindwa ili maadili, misingi na malengo waliyozipigania visiweze kupotea kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania na Namibia zina historia moja ya ukombozi na zinaendelea kushirikiana katika kutimiza azma ya kukamilisha ukombozi wa Afrika kupitia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuhifadhi maeneo yote ya kihistoria yaliyotumiwa na wapigania uhuru kwa kuyaacha katika hali yake ya asili ili kulinda uhalisia wa historia hiyo, huku ikiendelea kuboresha miundombinu katika maeneo jirani kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *