Serikali Kuanza Kulipa Kifuta Jasho Askari Walioshiriki Vita ya Kagera
Na Baraka Messa – MAELEZO
Serikali imekamilisha hatua muhimu za kisheria zitakazowezesha kuanza kwa malipo ya kifuta jasho kwa askari waliojitolea kushiriki Vita ya Kagera dhidi ya utawala wa Idd Amin mwaka 1978/79 ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kulinda uhuru na usalama wa Taifa.
Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akijibu maswali ya papo kwa papo Juni, 18, 2026, bungeni Dodoma, amesema kuwa vikwazo vya kisheria vilivyokuwa vinazuia utekelezaji wa malipo hayo vimeondolewa kufuatia maelekezo ya Rais, hivyo kufungua njia kwa askari hao kupata stahiki zao baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Njombe, Mhe. Deo Mwanyika, Mhe. Waziri Mkuu, amesema kuwa Serikali inaendelea na zoezi la utambuzi na uhakiki wa askari hao, ambapo takribani askari 7,200 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo mara baada ya taratibu husika kukamilika.
Hatua hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuthamini na kutambua mchango wa wananchi walioweka maisha yao rehani katika nyakati muhimu za historia ya Taifa. Mwaka 2025 Serikali ilikamilisha zoezi la kuwatambua baadhi ya washiriki wa vita hii kutoka Uganda waliokuwa na mchango katika harakati za kuikomboa nchi wakati wa Vita vya Kagera, hatua iliyoweka msingi wa kuendelea kuwathamini wote walioshiriki katika mapambano hayo,” amesema Mhe. Waziri Mkuu.
Vita ya Kagera ya mwaka 1978/79 inabaki kuwa moja ya matukio muhimu katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki, ambapo majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na wapigania uhuru wa Uganda yaliweza kuondoa utawala wa Idd Amin na kurejesha usalama katika eneo hilo.