Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Prof. Janabi Atoa Rai Magonjwa Yasiyoambukiza kuwa Kipaumbele cha Taifa

June 23, 2026

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi, ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi kwenye afya hasa upande wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwani afya haijawahi kuwa gharama na ni uwekezaji ambao nchi inaweza kuona faida yake.

Ametoa rai hiyo Juni 23, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika (ICPPA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.

Prof. Janabi amesema kuwa nchi inaweza kufanya magonjwa yasiyoambukiza kuwa kipaumbele cha maendeleo ya kitaifa kwa kutumia sera za kifedha zinazoweza kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na kodi kwenye tumbaku, pombe na bidhaa zote zenye sukari, kupanua ulinzi wa kifedha ili ugonjwa usimaanishe umaskini, kuongeza kiwango cha mpango wa Pen na Pen-Plus kitaifa pamoja na kuwalinda watoto kwa kutengeneza mazingira yenye afya bora.

Tunaweza kuwa na vipaumbele vingi lakini tunasahau kuwa vipaumbele vinahitaji vitendo. Magonjwa yasiyoambukiza si tishio la baadaye tena katika bara letu bali ni ukweli wa sasa kwani yanasababisha asilimia 37 ya vifo. Magonjwa kamwe hayapaswi kuamua hatma ya mtu kwa sababu kila maisha ya Mwafrika yana thamani na utu sawa”, amesema Prof. Janabi.

Akizungumzia kuhusu Pen-Plus, amesema kuwa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 20 na imeweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya 100,000 huku akisisitiza kuwa si miradi ya majaribio tu bali ina ushahidi kwani kupitia kuimarisha afya, watoto wanarudi shuleni, vijana wanaishi maisha marefu na akina mama wanajifungua salama na kuishi. 

Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa Maendeleo, Bw. James Reid kutoka Mfuko wa Hisani wa Helmsley Charitable Trust ameeleza kuwa, kwa muda mrefu wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini kwenye ukanda wa Afrika, wanakabiliwa na changamoto zikiwemo za huduma za afya zisizofikika, kukosa wafanyakazi wa afya waliofunzwa na mifumo michache ya kuwahudumia wagonjwa hao pamoja na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, dawa au huduma za ufuatiliaji.

“Tunahitaji kuendelea kupanua idadi ya nchi zinazohusika katika mtandao huu ili kufikia malengo ya kikanda ya nchi wanachama wa WHO. Tunahitaji kuendelea kujenga na kuimarisha nguvu kazi inayofanya huduma hii iwezekane, tunahitaji kufanya kazi pamoja na nchi husika ili kuhakikisha kuwa kuna ufadhili endelevu na kuhakikisha kuwa mfumo huu unaweza kuendelea kupanuka”, amemalizia Bw. Reid.

PEN-Plus ni mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa NCDI Poverty unaolenga kupanua huduma za afya kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yaliyo sugu na makali. Mpango huu unapanua wigo wa huduma kutoka ngazi za chini ili wagonjwa wapate matibabu katika hospitali za wilaya au rufaa za ngazi ya kwanza bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *