Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa Ithibati ya Maisha utakaowezesha waandishi wa habari wakongwe waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari nchini kutambuliwa rasmi, licha ya kutokukidhi vigezo vya kielimu vilivyowekwa na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016. Uzinduzi wa mwongozo huo umetajwa kuwa hatua muhimu ya kutambua mchango wa wanahabari waliolitumikia taifa kwa uadilifu na weledi kwa miaka mingi kabla ya kuanza kutumika kwa masharti mapya ya kitaaluma yanayomtaka mwandishi wa habari kuwa na angalau stashahada (Diploma) ya uandishi wa habari. Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya JAB, uliofanyika Julai 11, 2026 katika kijiji cha Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo katika viwanja vya Maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara Dar es salaam (sabasaba) Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Tildo Mhando, kupitia taarifa iliyosomwa na Dkt. Egbert Mkoko, alisema mwongozo huo unalenga kuwapa Ithibati ya Maisha waandishi wa habari wakongwe ambao wakati Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ilipopitishwa mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au zaidi na walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika sekta ya habari. Alieleza kuwa waandishi hao hawakupata fursa ya kusomea darasani hadi kufikia kiwango cha diploma, lakini walijijengea uwezo kupitia uzoefu na walishiriki kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya vyombo vya habari na ujenzi wa taifa. “Mwongozo huu unalenga kuhifadhi historia ya tasnia ya habari, kuthamini mchango wa waandishi wa kizazi cha mwanzo na kuhakikisha uzoefu wao unaendelea kuwa sehemu ya urithi wa taaluma hii” ilisisitiza taarifa hiyo. Aidha, aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kushirikiana na JAB katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na kusisitiza umuhimu wa weledi, uwajibikaji na maadili kwa waandishi wa habari nchini. Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Bwana Patrick Kipangula alisema kuwa uzinduzi wa Mwongozo wa Ithibati ya Maisha ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kuhakikisha kuwa ni pamoja na kuimarisha viwango vya taaluma kupitia sheria, mchango wa waandishi wa habari wakongwe waliolitumikia taifa kwa uaminifu na uzalendo unaendelea kutambuliwa na kuthaminiwa.

Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa mafanikio ya Tamasha la Lugha ya Kiswahili lililofanyika nchini Ufaransa yamefungua ukurasa mpya wa kuitangaza lugha ya Kiswahili duniani na kuifanya kuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi, biashara na diplomasia ya Tanzania. Akizungumza Julai 8, 2026, alipotembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Msigwa amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika tamasha hilo umeonyesha kuwa Kiswahili sasa si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni rasilimali yenye uwezo wa kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania.   Msigwa ameendelea kusema kuwa mataifa mengi yaliyofanikiwa kiuchumi yamenufaika pia kwa kutumia lugha zao kama chachu ya biashara na ubunifu, hivyo Watanzania wanapaswa kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kutangaza bidhaa, huduma na utamaduni wao katika soko la kimataifa. ” Baada ya mafanikio ya tamasha hilo, taasisi za Serikali na sekta binafsi zinapaswa kujipanga kimkakati ili kutumia fursa zinazotokana na kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili duniani, hatua itakayochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yenye lengo la kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja”, amesisitiza Msigwa. Akihusisha ujumbe huo na Maonesho ya Sabasaba, Msigwa amefafanua kuwa maonesho hayo yanatoa jukwaa muhimu la kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za ndani, ubunifu wa teknolojia na uongezaji thamani wa mazao, akitaja mfano wa vijana wa DIT ambao wametengeneza bajaji ya umeme na wafanyabiashara wanaochakata mazao kama korosho na parachichi na kusisitiza kuwa maendeleo hayo yanapaswa kuungwa mkono ili kuongeza ajira, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuhakikisha fedha nyingi zaidi zinabaki kuzunguka ndani ya uchumi wa Tanzania. Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kuelekeza nguvu katika uzalishaji, biashara, kilimo, viwanda na ubunifu badala ya kushawishiwa na ajenda zinazoweza kuvuruga maendeleo ya Taifa. Sambamba na hilo amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza teknolojia mpya, kupata maarifa kutoka kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi na kutumia fursa hizo kuboresha shughuli zao za kiuchumi huku akibainisha kuwa ongezeko la idadi ya nchi na kampuni zinazoshiriki katika maonesho ya mwaka huu ni ishara ya kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Ambapo, maarifa, teknolojia na lugha ya Kiswahili vinatajwa kuwa ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazoifanya Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo.

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema hali ya amani na usalama katika Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere. Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo leo Julai 7, 2026, Chalamila aliwapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki maonesho hayo, akisema ushiriki huo unaonesha wananchi wanatumia vyema fursa ya kujifunza, kufanya biashara na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na washiriki. Alisema Serikali inaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanatawala ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao bila hofu, huku akiwataka kupuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga kuwakatisha tamaa kushiriki maonesho hayo. Pokeeni salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tunaendelea kuhamasisha Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kuona teknolojia mpya, kununua bidhaa kwa bei nafuu na kujifunza ubunifu mbalimbali unaooneshwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Chalamila. Alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 25, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Jumanne Muliro alisema hali ya usalama katika jiji hilo inaendelea kuwa tulivu, huku akieleza kuwa tathmini ya maeneo mbalimbali, ikiwemo Kibamba, Kimara, Ubungo, Manzese, Tegeta, Bunju na Kigamboni, inaonesha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani. Aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika katika kipindi chote cha maonesho hayo, na kuwataka waendelee kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama. Muliro alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa, akiwahimiza Watanzania kuendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa utulivu na uzalendo.