Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Baraka Messa – MAELEZO Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu cha huduma za matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi nchini Tanzania na Afrika Mashariki, kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 10 uliowezesha hospitali hiyo kutoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingi za ukanda huu. Hayo yanaelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu mafanikio ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya. Msigwa anasema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 kuimarisha Hospitali ya Benjamin Mkapa ili ifikie viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa. “Hospitali ya Benjamin Mkapa leo inatoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi si Tanzania pekee, bali hata katika Afrika Mashariki, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 katika kipindi cha miaka 10 kuifanya hospitali hii kuwa kituo cha kisasa cha matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi,” anasema Msigwa. Anafafanua kuwa uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya kutolea huduma za kibingwa, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa, uboreshaji wa mifumo ya Tehama pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na kuboresha mazingira yao ya kazi. Msigwa anasema mwaka 2015 hospitali hiyo ilikuwa na watumishi 20 pekee, lakini kufikia mwaka 2026 idadi hiyo imeongezeka na kufikia watumishi 1,076, wakiwemo madaktari bingwa 105. Anasema hospitali hiyo sasa inatoa huduma 17 za kibingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, huduma za radiolojia ya kisasa pamoja na uchujaji wa damu (dialysis). “Huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu zinapatikana Hospitali ya Benjamin Mkapa na ni miongoni mwa huduma adimu ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi nchini na Afrika Mashariki,” anaeleza . Msigwa anasema kuimarika kwa huduma hizo kumepunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya Watanzania waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta matibabu, jambo ambalo limeokoa fedha nyingi za Serikali na wananchi. HOSPITALI BENJAMINI YAWA KIVUTIO WAGONJWA KUTOKA MATAIFA YA NJE Msigwa anasema hospitali hiyo sasa imekuwa kivutio cha wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. “Tumewahudumia wagonjwa 2,897 kutoka Burundi na wagonjwa 526 kutoka Comoro. Pia wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za Afrika Mashariki wanaendelea kuja kupata matibabu hapa, Tunawatibu ndugu zetu, lakini pia huu ni utalii wa matibabu unaoingizia taifa mapato,” anasema Msigwa. Anasema kuwa mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuanza kushindana na mataifa yaliyopiga hatua katika utalii wa matibabu kama India, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakipokea wagonjwa wengi kutoka Tanzania. “Kwa muda mrefu Watanzania walikuwa wakitumia fedha nyingi kwenda kutibiwa nje ya nchi, hususan India,..Sasa Serikali imewekeza kuhakikisha huduma hizo zinapatikana hapa nchini ili wananchi wapate matibabu bora na wakati huohuo Tanzania inufaike kupitia utalii wa matibabu,” anasema Msigwa. Pia Msigwa amesema Julai 10, 2025 Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzisha International Clinic, kitengo maalumu kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na wa kimataifa. Anasema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo, wagonjwa 18,607 wamehudumiwa, wakiwemo wagonjwa 390 kutoka mataifa mbalimbali, huku huduma ya Master Health Check-up ikiendelea kuvutia watu wanaohitaji uchunguzi wa afya kwa kiwango cha kimataifa. Aidha anasema hospitali hiyo pia imeanzisha eneo maalumu la huduma binafsi kwa wagonjwa wanaohitaji faragha na huduma za kiwango cha juu bila kuchangamana na wagonjwa wengine. Anasema Huduma hizi zinafanana na zile zinazotolewa katika hospitali za kisasa duniani kama za China, Ujerumani na India, huku dhamira ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ndani ya nchi na wakati huohuo Tanzania inakuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika. Kuimarika kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali mbalimbali za rufaa nchini ni sehemu ya malengi ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani wa kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu.

▪️Ujenzi Wake Kuanza Oktoba 2026 ▪️Fidia Shilingi bil 8.5 Imeshalipwa kwa Wananchi Waliopisha Mradi Na Adelina Johnbosco – MAELEZO Tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dodoma linaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu kufuatia ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Farkwa utakaoanza kujengwa Oktoba mwaka huu. Bwawa hilo litakalojengwa wilayani Chemba, kata ya Farkwa mkoani Dodoma litakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 128 kwa siku na kuhifadhi lita bilioni 390 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22. Bwawa hili litahudumia hasa wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino na maeneo mengine ndani na maeneo ya karibu na mkoa wa Dodoma, lengo ni kutokomeza kabisa upungufu wa maji ndani ya mkoa huo. Ujenzi wa bwawa la Farkwa utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi bilioni 163.43 hadi kukamilika kwake. Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 8.5 zimelipwa kama fidia kwa wananchi kutoka katika vijiji viwili vya Mombose na Bubutole waliopisha ujenzi. “Tuliambiwa tunahamishwa na kulipwa, mwaka 2017 tathmini ilifanyika katika maeneo yetu, ila ukiwa bado hujapokea kitu mkononi unaona kama haiwezekani, lakini mwaka 2019 tukalipwa fidia zetu, tukaanza maisha mapya na yenye matumaini zaidi katika kijiji cha Sankwaleto kwenye makazi mapya” Bi. Rahma Petro, mkazi wa Farkwa Hadi hapa, tayari inaonekana Dodoma yenye ukijani wakati wote, iwe mvua iwe jua, hakuna tena ukame katika mkoa huu pale mradi huu utakapokuwa umekamilika, yale yaliyokuwa yanasubiriwa kufanyika wakati wa kipindi cha mvua pekee yatafanyika pia kipindi cha kiangazi. “Tumeajiandaa kwa vingi kwa kweli, kijamii na kiuchumi, tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutafuga samaki na mengine mengi, ni furaha tupu. Hii ilikuwa ni hadithi ya muda mrefu ambayo tumezaliwa tukaikuta kutoka kwa wazee wetu, hakika leo inatimia” Bw. Suleiman Gawa, mkazi wa Farkwa Akiwa katika eneo utakapotekelezwa mradi huo, hivi karibuni, Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia ambaye ni mtaalam wa maji chini ya ardhi kutoka Wizara ya Maji, amebainisha uwepo wa maji ya akiba kwa watumiaji kutokana na wingi wa lita za maji utaokaozalishwa na bwawa hilo. “Mradi huu unaanza mwezi Oktoba, 2026, maandalizi yako tayari na baada ya kukamilika kwa mradi, si kwamba utaondoa kero ya maji tu bali hata kuchochea miradi mbali mbali ya kiuchumi kama vile kilimo cha umwagiliaji kisichosubiri msimu, ufugaji wa samaki na itakuwa ongezeko la maji katika hifadhi ya pori la akiba Swagaswaga Chemba, wanyama hifadhini watapata maji ya kunywa ya kutosha tofauti na hali ilivyo kwa sasa” Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia Mradi huu mwisho wake ni kuleta maji, lakini suala la ajira wakati na baada ya mradi ni vitu vinavotegemewa pakubwa. Mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya cha Sankwaleto, akaongea kuhusu wazawa kupata fursa mbalimbali kutokana na mradi huo. “Kama kiongozi tumeshashirikishwa na kuhakikishiwa kwamba, sisi wazawa tutapewa kipaumbele katika fursa mbalimbali zinazotokana na huu mradi ikiwemo ajira wakati na baada ya ujenzi, hivyo nawasihi vijana na wakazi wenzangu wa hapa kuwa tayari, tusikubali kukaa kinyonge katika kuchangamkia fursa katika hizi” Bw. Khalifa Salum, mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya Sankwaleto Si nyumba na umiliki wa ardhi pekee kwenye maeneo ya makazi mapya waliohamia wananchi waliopisha mradi, bali shule na zahanati vimejengwa kwa ajili ya kuwahudumia. “Kijiji cha Sankwaleto kimejengwa shule ya msingi na imeshaanza kazi, kuna nyumba za walimu na wanafunzi wote waliokuwa wakisoma kule kwenye vijiji vya zamani wako kwenye shule mpya wanaendelea na masomo, hakuna kilichosimama, pia zahanati inayowahudumia wananchi, kwa kweli tunashukuru sana” – Bi. Agnes Msote, Diwani wa kata ya Farkwa Kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kunatarajiwa kuimarisha usalama wa maji katika jiji la Dodoma na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo. Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji nchini kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upatikanaji wake maeneo yote hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na kuhakikisha juhudi za kufikisha huduma za maji katika vijiji vyote nchini linatimia ili kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Mkoa wa Kigoma umekuwa na nafasi ya kimkakati katika biashara ya kikanda kutokana na mwambao wake katika Ziwa Tanganyika na ukaribu wake na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia. Hata hivyo, changamoto za miundombinu ya usafirishaji zimekuwa zikizuia mkoa huo kutumia kikamilifu fursa hiyo, huku gharama za usafirishaji zikiwa kubwa na safari za mizigo kuchukua muda mrefu. Sasa hali hiyo imeanza kubadilika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora–Kigoma, uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na maboresho ya Bandari ya Kigoma. Miradi hiyo inatarajiwa kuibadili Kigoma kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari. Katika kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uchukuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua meli nne mpya za mizigo, akaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Tabora–Kigoma na kukagua maendeleo ya maboresho ya Bandari ya Kigoma. Hatua hizo zinaakisi mkakati wa Serikali wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara. Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, anasema Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia kutokana na nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika. Anasema kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. “Kwa nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika, Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia. Miradi hii ya SGR na meli mpya za mizigo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema Prof. Mbarawa. Meli hizo nne mpya, ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo, zinatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Kigoma kuhudumia zaidi ya tani 832,000 za mizigo kwa mwaka. Mbali na kuongeza ufanisi wa usafirishaji, uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea biashara na kuzalisha takribani ajira 600 za moja kwa moja katika sekta mbalimbali. Kwa wakazi wa Kigoma, uwekezaji huo una maana zaidi ya kujengwa kwa miundombinu. Ni mwanzo wa zama mpya za fursa za kiuchumi, ajira na uwekezaji. Kuimarika kwa usafiri wa reli na majini kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupanua masoko na kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi. Bi. Asha Mussa, mkazi wa Kibirizi, anasema wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu maendeleo ya aina hiyo. “Tunaamini meli mpya na reli ya kisasa zitafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi. Kuimarika kwa miundombinu ya usafiri kutasaidia wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali kupata nafasi zaidi za kujikwamua kiuchumi.” Hisia kama hizo zinaungwa mkono na wananchi wengi wanaoamini kuwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya usafirishaji kwa miaka mingi. Bw. John Mwakalinga, mkazi wa Kigoma Mjini, anasema gharama kubwa za usafirishaji zimekuwa zikikwamisha biashara na kupunguza ushindani wa bidhaa katika masoko. “Kwa miaka mingi usafirishaji wa bidhaa ulikuwa na changamoto nyingi na gharama kubwa. Tunaamini SGR pamoja na maboresho ya bandari utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda masoko ya ndani na nchi jirani, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara na kuinua kipato cha wananchi.” Mradi wa Reli ya Kisasa wa Tabora–Kigoma wenye urefu wa kilometa 506 unajengwa kwa gharama ya takribani dola za Marekani bilioni 2.7. Mradi huo utaunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa unaofika Dar es Salaam, hivyo kuimarisha Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Zambia. Faida za miradi hiyo hazitaishia katika kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria pekee. Pia zinatarajiwa kuongeza ushindani wa biashara za kikanda, kuvutia uwekezaji, kuchochea uzalishaji wa bidhaa na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kadri miradi hiyo inavyoendelea kukamilika, Kigoma inaelekea kujidhihirisha kama kitovu kipya cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati. Uwekezaji wa Serikali katika reli, bandari na usafiri wa majini unaweka msingi imara wa maendeleo endelevu, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi. Kwa hakika, kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, kuanza kwa huduma za meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi. Kigoma itaimarika kama lango kuu la biashara katika ukanda huu, huku Tanzania ikiendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara Afrika Mashariki na Kati.

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Kwa miaka mingi, wakazi wa Chamwino na maeneo jirani mkoani Dodoma wameishi na simulizi moja inayofanana; kuamka alfajiri kutafuta maji, kusubiri kwa saa nyingi kwenye foleni au kuishi kwa mgao wa maji usiotabirika. Leo, simulizi hiyo inaelekea kuwa historia kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji miji 28 Chamwino, unaotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika huduma ya maji. Mradi huu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17 unatekelezwa katika Wilaya ya Chamwino na unatarajiwa kuhudumia wakazi wa kata za Chamwino, Msanga, Buigiri, Chinangali pamoja na maeneo ya karibu ikiwemo Mtumba na Ihumwa. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kutekeleza miradi ya maji katika miji 28 Tanzania Bara, ukiwa na lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika. Ujenzi wa mradi ulianza Aprili mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Agosti, 2026 ambapo hadi sasa, utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 74, huku baadhi ya maeneo tayari yakiwa yameanza kupata huduma ya maji. Kwa wakazi wa Chamwino, mradi huu si tu ujenzi wa miundombinu, bali ni ukombozi wa maisha yao ya kila siku. “Kiukweli, hapo nyuma maji hayakuwa yanatosha. Serikali imetukumbuka. Mradi mkubwa wa namna hii kwa sisi tuliopitia ugumu wa maji kwa muda mrefu ni jambo la kujivunia na la kushukuru sana,” anasema Bi. Maila Nyembela, mkazi wa Chamwino Ikulu. Licha ya mradi kutokamilika, tayari umeanza kuonesha matokeo chanya. Huduma ya maji sasa inapatikana kwa wastani wa saa 22 kwa siku, hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa mgao wa maji uliokuwa ukiwasumbua wakazi kwa miaka mingi. Kwa wanawake, ambao kwa muda mrefu walibeba jukumu kubwa la kutafuta maji, mradi huu umeleta matumaini mapya. “Awali tulilazimika kuamka alfajiri kutafuta maji au kununua kwa gharama kubwa. Ilikuwa tabu sana, hasa kwa wanawake. Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha maisha ya familia zetu na kutupa muda zaidi wa kushiriki shughuli za maendeleo,” anasema Bi. Mluka Michael, mkazi wa Chamwino. Mratibu Msaidizi wa Mradi huu kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Titho Alex, anaeleza kuwa mradi huo umejumuisha ujenzi wa visima virefu nane, matenki mawili ya kuhifadhi maji pamoja na miundombinu ya kutibu, kusukuma na kusambaza maji. Anasema tanki moja lililopo Chamwino Ikulu lina uwezo wa kuhifadhi maji lita 500,000 , huku lingine lililopo Msanga likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 200,000. “Mkakati huu utawezesha mradi kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku, kiwango kitakachohakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa saa 22 hadi 24 kila siku na kuondoa kabisa changamoto ya mgao wa maji Chamwino pamoja na kuimarisha huduma katika maeneo ya jirani,” anasema Mhandisi Alex. Kwa wananchi walioishi muda mrefu Chamwino, mradi huu ni ushahidi wa mabadiliko makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika Makao Makuu ya Nchi. “Nimeishi Dodoma tangu mwaka 1971. Wakati huo hatukuwa na maji kabisa. Baadaye yakaanza kupatikana lakini hayakutosha. Sasa karibu kila kitongoji kina maji, ingawa baadhi ya maeneo bado hupata kwa mgao. Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu ukikamilika tutapata maji kila siku. Hili ni jambo la kufurahisha sana,” anasema Mchungaji Anderson Ndoloji wa Mtaa wa Muungano. Meneja wa DUWASA Kanda ya Chamwino, Mhandisi Gray Mbalikila, anasema mradi huo utaongeza uwezo wa mamlaka hiyo kupanua huduma katika maeneo mapya yanayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la wakazi, biashara na taasisi mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma. “Tunajivunia hatua tuliyofikia. Mradi huu ukikamilika, Chamwino itakuwa na akiba ya kutosha ya maji hata kwa ajili ya kata za jirani. Huduma itaongezeka kutoka kiwango cha sasa cha takribani asilimia 91 hadi kufikia asilimia 100,” anasema. Mbali na kuboresha upatikanaji wa maji, mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali. Upatikanaji wa maji ya uhakika utaimarisha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama, kuongeza usafi wa mazingira, kukuza biashara ndogo na shughuli za uzalishaji, pamoja na kuboresha huduma katika shule na vituo vya afya. Kadri Dodoma inavyoendelea kukua kama Makao Makuu ya Serikali, mahitaji ya huduma za msingi yanaongezeka. Mradi wa Maji Miji 28 Chamwino ni moja ya miradi ya kimkakati inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama. Kukamilika kwa mradi huu hakutakuwa tu mwisho wa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wananchi wa Chamwino na maeneo jirani, bali kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ambapo maji yatakuwa si tena changamoto, bali chachu ya maendeleo.

■ Utekelezaji wake mbioni kukamilika ■ Wafanyabiashara wausubiri kwa hamu Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Ule msemo wa Kiswahili unaosema “Mgeni njoo, mwenyeji apone” unaendelea kupata uhalisia kupitia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali jijini Dodoma. Mbali na kuimarisha usafiri wa anga nchini, mradi huo tayari umeanza kuleta manufaa kwa wananchi kupitia ajira, biashara na fursa za uwekezaji, huku ukitarajiwa kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha uchumi na usafiri wa anga. Mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 370 unatarajiwa kukamilika Septemba 2026. Kwa sasa, ujenzi wa miundombinu umefikia asilimia 87.97, huku ujenzi wa majengo ukiwa umefikia asilimia 76.15. Ajira Zimefungua Milango ya Mafanikio Tangu ulipoanza mwaka 2022, mamia ya wakazi wa Dodoma wamepata ajira za muda na fursa za biashara zilizoongeza kipato cha familia zao. Mkazi wa Mpamaa, Maximilian Mwagike, ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo. Anasema alianza kuuza miwa kwa kutumia baiskeli, lakini kuongezeka kwa shughuli za ujenzi kulipanua soko lake kiasi cha sasa kutumia guta kusafirisha bidhaa zake. “Biashara hii imenibadilisha maisha. Nimeboresha makazi yangu, ninalipia watoto wangu ada za shule binafsi na nimepanua biashara yangu,” anasema Mwagike, ambaye pia amepata ajira ya usimamizi wa mazingira katika mradi huo. Kwa upande wake, Mama Juma, aliyekuwa mama wa nyumbani, anasema mradi ulimwezesha kuanzisha biashara ya kupika na kuuza chakula kwa wafanyakazi wa ujenzi. “Leo naweza kulipia watoto wangu ada za shule, nimeweza kununua pikipiki inayoniingizia kipato na nina uhakika wa kuendelea na biashara hata baada ya mradi kukamilika,” anasema. Mradi Wajenga Ujuzi kwa Vijana Mbali na ajira za moja kwa moja, mradi huu umechangia kuwajengea vijana ujuzi na uzoefu wa kazi. Adam Kiula, anayefanya kazi katika kampuni inayosimika mifumo ya TEHAMA, kamera za usalama na mawasiliano, anasema amepata maarifa na uzoefu unaomuwezesha kushindana katika soko la ajira. Anawahimiza vijana kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali badala ya kusubiri ajira za kawaida. Wafanyabiashara Wanatazamia Mapinduzi ya Uchumi Faida za uwanja huo zinatarajiwa kuonekana zaidi baada ya kuanza kutoa huduma. Mfanyabiashara wa vifaa vya simu jijini Dodoma, anayefahamika kwa jina la Jeshi, anasema uwanja huo utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama zinazotokana na kupitisha bidhaa kupitia Dar es Salaam. Naye mfanyabiashara wa bidhaa za urembo, Happiness Mgeani, anaamini kukamilika kwa uwanja huo kutapunguza hasara zinazotokana na ucheleweshaji na uhamishaji wa mizigo kutoka usafiri mmoja kwenda mwingine. Uwanja wa Hadhi ya Kimataifa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, anasema kazi zilizobaki ziko katika hatua za mwisho za ukamilishaji, zikiwemo ufungaji wa mifumo mbalimbali, taa za kuongozea ndege, alama za barabara za ndege na umaliziaji wa majengo. Anasema uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kimataifa na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kama Airbus A330 na Boeing 787 Dreamliner, pamoja na kuhudumia (maegesho) ndege 17 kwa wakati mmoja. Aidha, anaeleza kuwa uwanja huo utakuwa na mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, mnara wa pili kwa urefu Afrika Mashariki, pamoja na maeneo ya biashara, maegesho ya magari na nafasi ya upanuzi wa baadaye. Maandalizi ya Uendeshaji Yamekamilika Kwa upande wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Zacharo Mduma amesema maandalizi ya kuanza uendeshaji wa uwanja huo yanaendelea, ikiwa ni pamoja na kuandaa watumishi watakaotoa huduma za uhamiaji, forodha, afya, usalama na zimamoto mara baada ya mradi kukabidhiwa rasmi. Lango Jipya la Ukuaji wa Uchumi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unatarajiwa kuwa wa Daraja F, kiwango cha juu kinachotambulika kimataifa. Mradi huo umefadhiliwa kwa asilimia 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku Serikali ya Tanzania ikichangia asilimia 15. Baada ya kukamilika, uwanja huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kuwa lango jipya la biashara, utalii na uwekezaji. Zaidi ya miundombinu ya usafiri, Uwanja wa Ndege wa Msalato unatajwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, huku ukiendelea kuthibitisha kwamba miradi mikubwa ya maendeleo inaweza kubadili maisha ya wananchi hata kabla haijakamilika.

Na Adelina Johnbosco – MAELEZO Barabara za Mzunguko Jijini Dodoma imechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa magari katikati ya jiji, hususan magari makubwa ya mizigo ya ndani na yanayokwenda nchi za nje. Mradi huu wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami una urefu wa jumla ya kilometa 112.3 huku sehemu ya kwanza (lot 1) yenye kilometa 52.3 ikiwa imekamilika kwa asilimia 93.3. Barabara hii imeunganisha barabara kuu za mikoa minne, bandari kavu Ihumwa – Morogoro, Veyula – Arusha, Nala – Singida na Matumbulu – Iringa ambako sehemu ya pili ya ujenzi (lot 2) inaanzia. Shughuli za usafiri na usafirishaji tayari zimeanza katika barabra hiyo, watumiaji wanashuhudia urahisi wa safari kutokana na kutokuwepo foleni.  Imeturahisishia sana, inafanya safari iwe fupi kutokana na ukweli kwamba njia hii haina foleni hata kidogo kama kule mjini kati, mwanzoni kutoka Ihumwa hadi Nala ilikuwa tunatumia takribani saa na nusu hata zaidi, lakini kwa sasa tunatumia dakika 45 hadi 48 kwa safari hiyo hiyo” Bw. Simon Ndamanyilu, dereva lori Akitoa ufafanuzi kuhusu barabara hiyo hivi karibuni, Mhandisi Morice Mlay, kutoka kampuni ya mzawa ya  Inter-Consult Ltd (Mhandisi Mshauri wa Mradi), amesema barabara hiyo tayari imeanza kutumika na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba, 2026 ambapo itakuwa imekamilika kabisa. “Ujenzi sehemu ya kwanza umefikia ukingoni, bado baadhi ya vitu vichache sana ikiwemo taa za barabarani na umaliziaji wa njia za watembea kwa miguu, magari mengi yanapita na yanapata urahisi kwa sababu hakuna foleni kwenye njia hii, mfano magari yanatoka moja kwa moja kutoka eneo la mzunguko wa Ihumwa hadi Nala ile barabara inayounganisha barabara ya Iringa bila kusimama popote” ametanabaisha Mha. Mlay Barabara hiyo ya njia nne yenye njia mbili kila upande, zimetenganishwa na uwazi katikati kwa ajili ya matumizi mengine pindi itakapohitajika kuongeza miundombinu mingine au uboreshaji. “Kuna baadhi ya watu wanashangaa kuhusu hili tuta lililoachwa katikati, hili ni kwa ajili ya matumizi ya baadaye mfano ujenzi wa barabara za mwendo kasi au kitu chochote kitakachoamuliwa kufanyika, lengo kuu ni kuepuka kutobomoa barabara kwa ajili ya kufanya kitu kipya” – Mha. Mlay  Baadhi ya wananchi jijini Dodoma wanaonesha furaha yao kutokana na uwepo wa barabara hiyo mpya inayopitisha magari mengi hasa magari makubwa ya mizingo kwenda ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Mha. Mlay, yapo magari yanayoelekea nchini Rwanda, Congo na Burundi kupitia barabara ya mzunguko. Katika eneo la Nala ambako kuna mojawapo ya makutano ya barabara hiyo na sehemu ya maegesho ya magari, wakazi wa maeneo hayo wamepata fursa ya kufanya biashara kutokana na uwepo wa watu wengi kwa wakati mmoja. “Kituo hiki yanapitisha na kusimama magari ya kila aina, hii ni tofauti na mwanzo, magari yakisimama hapa watu wanashuka na wengine wanakuwa wamesubiria kupanda, wengine ni madereva wa magari makubwa, kwa hiyo lazima watahitaji kupata mahitaji kutoka kwetu hasa chakula, hii ni furaha kwetu” Mary John, mama ntilie Tamanio la wengi ni kuona barabara inaanza kazi rasmi kwani kwao ni tegemeo mojawapo la njia ya kuongeza kipato. Kama kwa sasa nauza bidhaa zangu kwa kiwango ambacho naona kinafaa, nawaza kwamba barabara hii ikianza kutumika rasmi magari yataongezeka, yataegeshwa kwa wingi zaidi na watu watakuwa wengi kuliko hivi” amesema Bi. Veronica Alfred, muuza nafaka eneo la Nala. Mussa Rajab mkazi wa Nala na mkuli eneo hilo, akiwawakilisha wabeba mizigo wenzake, anasema uwepo wa sehemu ya kisasa ya kuegesha magari umefanya kazi yao kuwa rahisi na kukuza kipato. “Mwanzoni eneo hili halikuwepo, hivyo kusimama kwa magari hapa ilitegemea udharura wa dereva hapo na sisi tunavizia kubeba mizigo japo kwa uchache sana, siku hizi magari yanasimama na mizigo inateremshwa hivyo tunabeba na kupata riziki” – Bw. Rajab Mradi huu kipande cha kwanza utagharimu shilingi bil. 100.84 hadi kukamilika kwake, na unatarajiwa kuwa mwarobaini wa msongamano wa magari katikati ya jiji pia kukuza uchumi wa mkoa wa Dodoma, mikoa ya jirani na nchi kwa ujumla.