Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Dar es Salaam Ipo Salama, Wananchi Wajitokeze kwa Wingi Sabasaba

July 7, 2026

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema hali ya amani na usalama katika Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo leo Julai 7, 2026, Chalamila aliwapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki maonesho hayo, akisema ushiriki huo unaonesha wananchi wanatumia vyema fursa ya kujifunza, kufanya biashara na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na washiriki.

Alisema Serikali inaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanatawala ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao bila hofu, huku akiwataka kupuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga kuwakatisha tamaa kushiriki maonesho hayo.

Pokeeni salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tunaendelea kuhamasisha Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kuona teknolojia mpya, kununua bidhaa kwa bei nafuu na kujifunza ubunifu mbalimbali unaooneshwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Chalamila.

Alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 25, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Jumanne Muliro alisema hali ya usalama katika jiji hilo inaendelea kuwa tulivu, huku akieleza kuwa tathmini ya maeneo mbalimbali, ikiwemo Kibamba, Kimara, Ubungo, Manzese, Tegeta, Bunju na Kigamboni, inaonesha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani.

Aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika katika kipindi chote cha maonesho hayo, na kuwataka waendelee kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama.

Muliro alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa, akiwahimiza Watanzania kuendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa utulivu na uzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *