Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Josephina Lupasha na Immaculate Makilika – MAELEZO Ulimwenguni kote miundombinu imeendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi. Barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, nishati na teknolojia ya mawasiliano ni muhimu katika kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuunganisha masoko na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa. Kwa upande wa Afrika, kupitia taasisi ya fedha Africa50 inayoshirikiana na Serikali mbalimbali barani Afrika inabadili taswira na hadhi ya Afrika kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kimkakati, uwekezaji wenye tija na mageuzi ya kiuchumi na teknolojia barani humo. Taasisi hiyo inaandaa miradi hadi kufikia hatua ya kupata wawekezaji na kutafuta wawekezaji kwa utaratibu wa equity investment kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kutoka kwa wawekezaji na wafadhili wa ndani na nje ya Afrika. Lengo ni kuharakisha utekelezaji wa miundombinu yenye ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha. Aidha, miundombinu ya kipaumbele ni pamoja na nishati, uchukuzi, elimu, afya, mawasiliano na fedha (fintech). Ili kuendelea kutoa mchango wake hadhimu kwa Afrika, Tanzania imeendelea kujijengea nafasi muhimu katika ramani ya uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuamua kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), lililofanyika Agosti 5 – 6, 2026, jijini Dar es Salaam. Hivyo inategemewa mkutano utavutia wawekezaji wa kimataifa kutangaza miradi ya kimkakati kama reli ya SGR, Bandari ya Dar es Salaam, uzalishaji wa umeme, na miundombinu ya TEHAMA. Mkutano huo ambao umeleta pamoja viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, katika jitihada za kutafuta namna ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika, umekuwa nyenzo muhimu ya kuutangazia ulimwengu kuhusu utayari wa Afrika na kutumia fursa zake Afrika katika kujiletea maendeleo ya kweli. Kwa Tanzania, mkutano huo umekuwa zaidi ya tukio la kimataifa, umekuwa fursa ya kuonesha uwezo, fursa na mwelekeo wa nchi katika kujenga uchumi unaotegemea miundombinu ya kisasa, uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anasema kuwa kuongezeka kwa imani kwa Tanzania kunatokana na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea nchini, fursa za uwekezaji na nafasi yake ya kimkakati kama lango linalounganisha Afrika na masoko ya kimataifa. Aidha, anasema Afrika inapaswa kujenga mustakabali wake kupitia uongozi madhubuti, mitaji na ushirikiano wa waafrika wenyewe, na kuwa bara la Afrika linaweza kutumia rasilimali zake, mitaji ya ndani na fursa zilizopo ili kupunguza pengo la maendeleo, kuongeza biashara na kuimarisha ushindani wake katika uchumi wa dunia. “Wananchi hawapimi maendeleo kwa matamko, bali kwa matokeo wanayoyaona katika maisha yao, Kwa msingi huo, Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora, nishati ya uhakika, bandari zenye ufanisi, reli za kisasa, miundombinu ya kidijitali na huduma nyingine zinazochochea uzalishaji, ajira na biashara” anasema Rais Samia. Akionesha utayari wa hatua iliyopigwa na Tanzania katika kuleta mageuzi ya kiuchumi anasema tayari imeweka msingi kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi na uboreshaji wa barabara na madaraja, maendeleo ya viwanja vya ndege pamoja na miradi ya nishati na miundombinu ya TEHAMA. Hata hivyo katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania 2050, yanayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea viwanda, ubunifu, rasilimali watu, maendeleo endelevu na miundombinu ya kisasa. Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi, huku ikilenga kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa kuwa na miundombinu ya kimkakati na kujenga ubia unaoweza kuvutia mitaji binafsi, teknolojia na ubunifu. Kwa hakika, Tanzania inaendelea kubaki na nafasi muhimu kama lango la nchi zisizo na bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pia inatoa fursa kubwa ya kuifanya nchi kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na uwekezaji. Uwezo wa bandari, reli, barabara na nishati unapoimarishwa kwa pamoja, Tanzania inaweza kuongeza mchango wake katika minyororo ya thamani ya kikanda na bara. Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sidi Quld Tah akizungumza pia katika Mkutano huo wa Africa50 anasema kuwa Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake, ikiwemo gesi asilia, kwa ufanisi ili kuchochea ukuaji wa viwanda, kuimarisha ustahimilivu wa nishati na kuboresha maisha ya wananchi. Anasisitiza “Akiba ya gesi asillia barani Afrika inafikia takribani asilimia saba ya akiba ya gesi duniani, rasilimali hizi zikitumika kwa busara zinaweza kusaidia kuimarisha viwanda, kuongeza ustahimilivu wa nishati na kuchochea ustawi wa wananchi wetu”. Dkt. Tah anapendekeza kuwa ili Afrika itimize malengo yake na kupata maendeleo inayokusudia inatakiwa kufanyika kwa uwekezaji wa haraka barani humo, kuimarisha matumizi ya mitaji ya ndani, mifumo ya kifedha na taasisi za kifedha ili kuziba pengo la ufadhili wa miundombinu. Aidha, anaeleza kuwa Afrika kwa kushirikiana Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Afrika50 zitaendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa, kupunguza hatari za uwekezaji na kuvutia mitaji zaidi. Naye, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, anasema kuwa uamuzi huo wa Africa50 kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Infra for Africa Forum, ni heshima na ishara ya imani kwa Tanzania pamoja na maono yake ya kujenga Afrika iliyounganishwa, yenye ustawi na maendeleo. “Kwa kipindi cha miaka 10, Africa50 imejijenga kama taasisi muhimu katika kuchochea uwekezaji wa miundombinu barani Afrika kupitia uandaaji wa miradi, uhamasishaji wa mitaji na uwekezaji wa kimkakati,” anasema Balozi Omar Tanzania, imekuwa mwananchama katika Africa50 kuanzia mwaka 2023, ambao umefungua fursa ya nchi kushiriki katika mfumo mpana wa kuandaa miradi, kuhamasisha uwekezaji na kukuza maendeleo endelevu ya miundombinu. Balozi Omar anaeleza manufaa ya uanachama wa Tanzania katika Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kuhusisha maandalizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini, ikiwemo maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini LNG, miundombinu ya usafirishaji wa umeme pamoja na ushirikiano katika upanuzi wa huduma za usafishaji wa figo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Inaelezwa kuwa kupitia Mkutano huo pia umeiwezesha Tanzania kuwasilisha fursa mbalimbali

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO* Sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Inatoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania, inachangia usalama wa chakula na ni chanzo kikuu cha malighafi kwa viwanda. Hata hivyo, kwa miaka mingi sekta hii ilikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji, hali iliyowafanya wakulima wengi kuendelea na kilimo cha kujikimu badala ya kilimo cha biashara. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita , hali hiyo imeanza kubadilika kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kupitia ongezeko la mtaji na upanuzi wa utoaji wa mikopo, benki hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Serikali imeendelea kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa mikopo yenye masharti nafuu. Lengo kuu ni kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kukuza kilimo cha kisasa kinachozalisha kwa tija. Mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani alifanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Hatua hiyo ilienda sambamba na kuiongezea TADB mtaji kutoka shilingi bilioni 60 hadi bilioni 268 kupitia uwekezaji wa Serikali wa shilingi bilioni 208. Jitihada hizo ziliendelea mwaka 2024 ambapo Serikali, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliongeza mtaji wa shilingi bilioni 174.16 na kufanya mtaji wa benki kufikia shilingi bilioni 442.16. Mwaka 2025 Serikali iliongeza tena shilingi bilioni 10, hivyo mtaji kufikia shilingi bilioni 452.16. Ongezeko hilo la mtaji limeongeza uwezo wa TADB kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, TADB imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.55. Kati ya kiasi hicho, zaidi ya asilimia 80, sawa na takribani shilingi trilioni 1.24, kimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita. Aidha, idadi ya wanufaika imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kabla ya mwaka 2021, benki ilikuwa imewafikia takribani wakulima milioni 1.6. Hadi sasa, zaidi ya wakulima milioni 2.6 wamepata mikopo ya moja kwa moja, huku zaidi ya wakulima 659,000 wakinufaika kupitia Dirisha la Dhamana la Mikopo ya Wakulima Wadogo. Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, anasema dirisha hilo limepanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima ambao hapo awali walishindwa kupata mikopo kutokana na ukosefu wa dhamana. Anasema kupitia utaratibu huo, TADB hutoa dhamana kwa benki na taasisi za fedha ili ziweze kuwakopesha wakulima wadogo kwa masharti nafuu. “TADB inaendelea kutoa mikopo katika sekta zote za kilimo. Pia tunaziwezesha benki nyingine kwa kuzipa fedha za muda mrefu na dhamana ili nazo ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu,” anasema Nyabundege na kuongeza kuwa kwa sasa, dirisha hilo lina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 692 na linatekelezwa kupitia benki 19 nchini. Upatikanaji wa mitaji umeongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Mwaka 2021 Tanzania ilizalisha tani milioni 17.148 za mazao ya chakula, lakini kufikia mwaka 2025 uzalishaji umeongezeka hadi tani milioni 22.8. Ongezeko hilo limeifanya Tanzania kufikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130, hali inayowezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Mbali na usalama wa chakula, mikopo ya TADB imeongeza matumizi ya pembejeo bora, teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo, hatua ambazo zimeongeza tija na kipato cha wakulima. Matokeo yake yanaonekana pia katika mazao ya biashara. Kwa mfano, uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 210,000 mwaka 2021 hadi tani 750,000 mwaka 2025. Wakati huo huo, mapato yatokanayo na mauzo ya mazao nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 hadi dola bilioni 5. Ukuaji huo unaonesha namna upatikanaji wa mitaji unavyochangia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara ya mazao na kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Serikali pia ilianzisha kifurushi cha uchochezi cha shilingi trilioni moja kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili benki za biashara ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu. Sambamba na hilo, Benki Kuu ilizikopesha benki za biashara kwa riba ya asilimia tatu ili ziweze kutoa mikopo kwa wakulima kwa riba isiyozidi asilimia 10. Kabla ya hatua hiyo, wakulima wengi walikabiliwa na riba kati ya asilimia 20 na 25, kiwango kilichowafanya wengi kushindwa kukopa. Hatua hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa mikopo inayokwenda kwenye sekta ya kilimo. Mikopo ya sekta hiyo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.3 kabla ya mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 5.8. Athari chanya zimeonekana pia katika sekta ya benki ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa na benki nchini imeongezeka kutoka shilingi trilioni 18.1 mwaka 2021 hadi trilioni 44.7, huku mali za benki zikifikia shilingi trilioni 77.7. Ukuaji huo unaonesha jinsi uwekezaji katika sekta ya uzalishaji unavyochochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, hususan sekta ya fedha. Katika mwaka wa fedha 2026/27, TADB imejipanga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Aidha, benki hiyo inalenga kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, kuwawezesha vijana na wanawake kupata huduma za kifedha, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo. Pia itaendelea kuchochea uongezaji thamani wa mazao ya kilimo ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na kimataifa, sambamba na kuunga mkono ajenda ya uchumi wa viwanda na diplomasia ya uchumi. Kwa ujumla, uwekezaji wa Serikali katika TADB umeonyesha kuwa upatikanaji wa mitaji ni nguzo muhimu ya mageuzi ya sekta ya kilimo. Kupitia mikopo hiyo, wakulima wameongeza uzalishaji na kipato, usalama wa chakula umeimarika, sekta ya benki imekua na uchumi wa Taifa umeendelea kupata nguvu. Kadri TADB inavyoendelea kupanua huduma zake, kilimo kinazidi kuwa biashara yenye tija, chanzo cha ajira kwa vijana na nguzo imara ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Mageuzi ya kidijitali katika sekta ya ununuzi wa umma yanaendelea kuleta matokeo makubwa nchini kupitia mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) ambao umekua mkombozi kwa watoa huduma na Serikali, ukiimarisha uwazi, uwajibikaji na ushindani katika matumizi ya fedha za umma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Dennis Simba anabainisha hayo katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma lililowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi wa ununuzi wa umma na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hilo lililofanyika jijini Arusha lililoogozwa na kaulimbiu isemayo “Kutumia Fursa ya Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani kuelekea Dira ya Taifa 2050,” limeonesha kuwa ununuzi wa umma si shughuli ya kiutawala pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ushindani wa biashara na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija. Mkurugenzi huyo wa PPRA anaeleza kuwa tangu kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huo, Julai 1, 2023, uendeshaji wa shughuli za ununuzi nchini kwa kiasi kikubwa umebadilika kwa kuwa mfumo huo unawezesha usajili wa wazabuni, uchakataji wa zabuni kwa njia ya mtandao, usimamizi wa mikataba, malipo ya mikataba, minada ya kielektroniki pamoja na matumizi ya katalogi ya bidhaa na huduma. Mbali na kurahisisha utoaji wa huduma, Bw. Simba anasema PPRA imeendelea kuuboresha mfumo huo kwa kuanzisha moduli ya kisasa ya ufuatiliaji wa vihatarishi katika michakato ya ununuzi kwa wakati halisi. Teknolojia hiyo inaiwezesha Mamlaka kubaini mapema viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa fedha za umma au kukiukwa kwa taratibu za ununuzi, ikiwemo upangaji wa matokeo ya zabuni, ushindani usioridhisha, kula njama kati ya wazabuni na vitendo vya udanganyifu. Anasema hatua hiyo imeongeza uwezo wa PPRA kuchukua hatua za haraka kabla dosari hazijasababisha hasara kwa Serikali, huku ikiimarisha uadilifu na uwazi katika mnyororo mzima wa ununuzi wa umma. Mafanikio ya matumizi ya NeST yameonekana kupitia ongezeko la ushiriki wa wadau ambapo hadi Juni 30, 2026, zaidi ya wazabuni 45,270 walikuwa wamesajiliwa katika mfumo huo, huku asilimia 95 wakiwa wazabuni wa ndani. Aidha, zaidi ya taasisi nunuzi 62,847 na watumiaji zaidi ya 161,704 walikuwa wakitumia mfumo huo. Anasema katika kipindi hicho, zabuni 286,903 zilitangazwa kupitia NeST na zaidi ya tuzo za zabuni 181,057 zenye thamani ya shilingi trilioni 14.5 zikatolewa kwa njia ya mfumo huo, hatua inayoonesha kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika kusimamia fedha za umma. Aidha, ameeleza kuwa PPRA imeendelea kuwezesha ushiriki wa makundi maalumu katika fursa za zabuni. Kupitia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, Taasisi Nunuzi zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Matokeo ya utekelezaji huo yanaonekana ambapo hadi Julai 28, 2026 zaidi ya makundi maalumu 23,590 yalikuwa yamesajiliwa katika NeST na tuzo 745 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 53.68 zilitolewa kwa makundi maalumu. Hii inaonesha kuwa mageuzi ya kidijitali hayajaboresha tu ufanisi wa Serikali, bali pia yamepanua fursa za kiuchumi kwa makundi yaliyokuwa hayashiriki kwa kiwango kikubwa hapo awali. Mbali na manufaa ya kiuchumi, matumizi ya NeST yamechangia pia utunzaji wa mazingira. Utafiti wa PPRA unaonesha kuwa matumizi ya mfumo huo yalipunguza uzalishaji wa metariki tani 64,028 za hewa ya ukaa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kutokana na kupungua kwa matumizi ya karatasi. Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambulika kimataifa. Mfumo wa NeST umepata tuzo mbalimbali za ubunifu na mazingira, ikiwemo kutajwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali duniani katika tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026 zilizofanyika Geneva, Uswizi. Sambamba na mafanikio hayo, PPRA imeendelea kuimarisha ukaguzi wa ukidhi na thamani halisi ya fedha ili kuhakikisha taasisi zote zinazingatia sheria na taratibu za ununuzi wa umma. Jitihada hizo zinaenda sambamba na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza uwajibikaji, kudhibiti mianya ya ubadhirifu na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi. Kadhalika, Mamlaka hiyo imeendelea kupanua ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi kupitia kubadilishana uzoefu katika ununuzi endelevu, huku nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Benki ya Dunia zikiendelea kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kujenga na kutumia Mfumo wa NeST. Kwa ujumla, mafanikio ya PPRA yanaonesha kuwa uwekezaji katika mifumo ya kidijitali si tu umeongeza uwazi na ufanisi wa ununuzi wa umma, bali pia umeifanya sekta hiyo kuwa chombo muhimu cha kukuza uchumi shindani, jumuishi na endelevu. Kadiri matumizi ya NeST yanavyoendelea kuongezeka, ndivyo nafasi ya ununuzi wa umma katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inavyozidi kuimarika.

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limeidhinisha kutolewa mara moja kwa takriban dola za Marekani milioni 443.9 kwa Tanzania baada ya kukamilisha tathmini za mwisho chini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience and Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika taarifa iliyotolewa Julai 10, IMF imesema uamuzi huo unafuatia kukamilika kwa mapitio ya sita na saba ya mpango wa ECF pamoja na mapitio ya tatu na nne ya mpango wa RSF, ambapo fedha hizo zinajumuisha takriban dola za Marekani milioni 158.75 chini ya ECF na dola za Marekani milioni 298.37 chini ya RSF. IMF imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara, huku ukuaji wa Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na kutarajiwa kufika karibu asilimia 6.2 kwa muda wa kati. Sekta zilizotajwa kuchangia matarajio hayo ni pamoja na madini, kilimo na utalii. Kwa mujibu wa tathmini hiyo, Tanzania imeendelea kudumisha utulivu wa uchumi mpana na mfumuko wa bei umebaki chini, ukiwa asilimia 4.0 mwezi Juni 2026. Hata hivyo, IMF imeonya kuwa kupanda kwa bei za mafuta duniani kunaendelea kutoa shinikizo kwa gharama za maisha na uchumi kwa ujumla. Taarifa hiyo imeonyesha pia kuwa utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kiuchumi kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Vigezo vingi vya utendaji vilifikiwa kwa wakati, ingawa baadhi ya malengo na mageuzi, hasa katika maeneo ya nishati, usimamizi wa VAT, utawala wa Benki Kuu na uwekezaji wa umma, yalichelewa au hayakukamilika kama ilivyotarajiwa. Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Bo Li, alisema Tanzania imefanikiwa kuhifadhi utulivu wa uchumi licha ya misukosuko ya ndani na nje. Alisema hatua zaidi zinahitajika katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha za umma, na kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu kama elimu na afya. Aidha, IMF imeishauri Tanzania kuendelea na mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha sekta binafsi, na kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Shirika hilo limeonya kuwa kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati kunaweza kudhoofisha ukuaji wa uchumi na kuongeza mfumuko wa bei. Pamoja na mtazamo chanya wa uchumi, IMF imesisitiza kuwa Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa za kupunguza umaskini, kufikia malengo ya maendeleo endelevu, na kuandaa fursa za kutosha kwa idadi ya watu inayotarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050. Kwa ujumla, uamuzi wa IMF unaonekana kuwa ishara ya kuendelea kwa imani ya taasisi hiyo kwa mwenendo wa uchumi wa Tanzania, huku ukitoa msukumo mpya kwa Serikali kuharakisha mageuzi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi. Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameshukuru uamuzi huo wa Taasisi hiyo kubwa ya Fedha duniani (IMF), kwa kuendelea kuamini mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi imeendelea kupiga hatua kubwa hadi sasa na kuungwa mkono na IMF. Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu ilipojiunga na IMF tarehe 10 Septemba 1962, ambapo jumla ya ahadi ya mikopo na misaada ya IMF kwa Tanzania imefikia Dola ya Marekani bilioni 4.578. Kati ya kiasi hicho, portfolio hai ya sasa ni dola za Marekani bilioni 2.52.