Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Tanzania Yaacha Alama ya Miundombinu, Uwekezaji na Mageuzi ya Uchumi Afrika

August 8, 2026

Na Josephina Lupasha na Immaculate Makilika – MAELEZO

Ulimwenguni kote miundombinu imeendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi. Barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, nishati na teknolojia ya mawasiliano ni muhimu katika kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuunganisha masoko na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa.

Kwa upande wa Afrika, kupitia taasisi ya fedha Africa50 inayoshirikiana na Serikali mbalimbali barani Afrika inabadili taswira na hadhi ya Afrika kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kimkakati, uwekezaji wenye tija na mageuzi ya kiuchumi na teknolojia barani humo.

Taasisi hiyo inaandaa miradi hadi kufikia hatua ya kupata wawekezaji na kutafuta wawekezaji kwa utaratibu wa equity investment kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kutoka kwa wawekezaji na wafadhili wa ndani na nje ya Afrika. Lengo ni kuharakisha utekelezaji wa miundombinu yenye ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha. Aidha, miundombinu ya kipaumbele ni pamoja na nishati, uchukuzi, elimu, afya, mawasiliano na fedha (fintech).

Ili kuendelea kutoa mchango wake hadhimu kwa Afrika, Tanzania imeendelea kujijengea nafasi muhimu katika ramani ya uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuamua kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), lililofanyika Agosti 5 – 6, 2026, jijini Dar es Salaam.

Hivyo inategemewa mkutano utavutia wawekezaji wa kimataifa kutangaza miradi ya kimkakati kama reli ya SGR, Bandari ya Dar es Salaam, uzalishaji wa umeme, na miundombinu ya TEHAMA.
Mkutano huo ambao umeleta pamoja viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, katika jitihada za kutafuta namna ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika, umekuwa nyenzo muhimu ya kuutangazia ulimwengu kuhusu utayari wa Afrika na kutumia fursa zake Afrika katika kujiletea maendeleo ya kweli.

Kwa Tanzania, mkutano huo umekuwa zaidi ya tukio la kimataifa, umekuwa fursa ya kuonesha uwezo, fursa na mwelekeo wa nchi katika kujenga uchumi unaotegemea miundombinu ya kisasa, uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anasema kuwa kuongezeka kwa imani kwa Tanzania kunatokana na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea nchini, fursa za uwekezaji na nafasi yake ya kimkakati kama lango linalounganisha Afrika na masoko ya kimataifa.

Aidha, anasema Afrika inapaswa kujenga mustakabali wake kupitia uongozi madhubuti, mitaji na ushirikiano wa waafrika wenyewe, na kuwa bara la Afrika linaweza kutumia rasilimali zake, mitaji ya ndani na fursa zilizopo ili kupunguza pengo la maendeleo, kuongeza biashara na kuimarisha ushindani wake katika uchumi wa dunia.

“Wananchi hawapimi maendeleo kwa matamko, bali kwa matokeo wanayoyaona katika maisha yao, Kwa msingi huo, Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora, nishati ya uhakika, bandari zenye ufanisi, reli za kisasa, miundombinu ya kidijitali na huduma nyingine zinazochochea uzalishaji, ajira na biashara” anasema Rais Samia.

Akionesha utayari wa hatua iliyopigwa na Tanzania katika kuleta mageuzi ya kiuchumi anasema tayari imeweka msingi kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi na uboreshaji wa barabara na madaraja, maendeleo ya viwanja vya ndege pamoja na miradi ya nishati na miundombinu ya TEHAMA.

Hata hivyo katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania 2050, yanayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea viwanda, ubunifu, rasilimali watu, maendeleo endelevu na miundombinu ya kisasa. Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi, huku ikilenga kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa kuwa na miundombinu ya kimkakati na kujenga ubia unaoweza kuvutia mitaji binafsi, teknolojia na ubunifu.

Kwa hakika, Tanzania inaendelea kubaki na nafasi muhimu kama lango la nchi zisizo na bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pia inatoa fursa kubwa ya kuifanya nchi kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na uwekezaji. Uwezo wa bandari, reli, barabara na nishati unapoimarishwa kwa pamoja, Tanzania inaweza kuongeza mchango wake katika minyororo ya thamani ya kikanda na bara.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sidi Quld Tah akizungumza pia katika Mkutano huo wa Africa50 anasema kuwa Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake, ikiwemo gesi asilia, kwa ufanisi ili kuchochea ukuaji wa viwanda, kuimarisha ustahimilivu wa nishati na kuboresha maisha ya wananchi.

Anasisitiza “Akiba ya gesi asillia barani Afrika inafikia takribani asilimia saba ya akiba ya gesi duniani, rasilimali hizi zikitumika kwa busara zinaweza kusaidia kuimarisha viwanda, kuongeza ustahimilivu wa nishati na kuchochea ustawi wa wananchi wetu”.

Dkt. Tah anapendekeza kuwa ili Afrika itimize malengo yake na kupata maendeleo inayokusudia inatakiwa kufanyika kwa uwekezaji wa haraka barani humo, kuimarisha matumizi ya mitaji ya ndani, mifumo ya kifedha na taasisi za kifedha ili kuziba pengo la ufadhili wa miundombinu. Aidha, anaeleza kuwa Afrika kwa kushirikiana Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Afrika50 zitaendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa, kupunguza hatari za uwekezaji na kuvutia mitaji zaidi.

Naye, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, anasema kuwa uamuzi huo wa Africa50 kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Infra for Africa Forum, ni heshima na ishara ya imani kwa Tanzania pamoja na maono yake ya kujenga Afrika iliyounganishwa, yenye ustawi na maendeleo.

“Kwa kipindi cha miaka 10, Africa50 imejijenga kama taasisi muhimu katika kuchochea uwekezaji wa miundombinu barani Afrika kupitia uandaaji wa miradi, uhamasishaji wa mitaji na uwekezaji wa kimkakati,” anasema Balozi Omar

Tanzania, imekuwa mwananchama katika Africa50 kuanzia mwaka 2023, ambao umefungua fursa ya nchi kushiriki katika mfumo mpana wa kuandaa miradi, kuhamasisha uwekezaji na kukuza maendeleo endelevu ya miundombinu.
Balozi Omar anaeleza manufaa ya uanachama wa Tanzania katika Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kuhusisha maandalizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini, ikiwemo maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini LNG, miundombinu ya usafirishaji wa umeme pamoja na ushirikiano katika upanuzi wa huduma za usafishaji wa figo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Inaelezwa kuwa kupitia Mkutano huo pia umeiwezesha Tanzania kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji kwa taasisi za fedha, wawekezaji na washirika wa maendeleo kutoka Afrika na nje ya bara. Ambapo maeneo yenye fursa yaliyowekwa wazi ni pamoja na nishati, uchukuzi, reli, bandari, usafiri wa anga, maji, afya, madini, mafuta na gesi, mawasiliano na teknolojia.

Ili kubadili taswira ya Afrika na kuiwezesha kutumia raslimali zake na fursa zake kwa manufaa na mstakabali wake, Mkutano huo umeweka msisitizo katika kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa na kuvutia wawekezaji, badala ya kubaki katika hatua ya mipango. Hii inaendana moja kwa moja na kaulimbiu ya Mkutano kutoka dhamira hadi utekelezaji.

Mafanikio ya Mkutano huo yatapimwa zaidi kwa kasi ambayo fursa na makubaliano yatageuzwa kuwa miradi halisi, mitaji, ajira, biashara na huduma bora kwa wananchi. Na ni vyema Waafrika sasa wakaelewa kuwa Afrika inawahitaji Waafrika kujiletea maendeleo yake ya kweli.

Iwapo dhamira, mitaji na utekelezaji vitaunganishwa kwa ufanisi, miundombinu inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha viwanda, biashara, ajira na maendeleo ya wananchi, na kuifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mustakabali wa uchumi wa Afrika.

Fauka ya hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Amina J. Mohammed akihutubia katika Mkutano wa Wadau katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani, Julai 21, 2025 ametoa wito kwa Afrika kuchukua hatua za haraka za kimfumo ili kuongeza kasi ya maendeleo barani humo “Afrika ina kila kitu kinachohitajika kubadilisha hali hii.”
Kisha akaeleza mabadiliko manne makuu ambayo, yakitekelezwa kikamilifu, yanaweza kubadilisha mwelekeo wa maendeleo kuelekea ustawi wa watu na maendeleo endelevu katika bara hilo ambayo ni kudhibiti mfumo wa fedha, kuwekeza kwa vijana, kujenga mifumo imara na jumuishi na kufanya uwajibikaji uonekane kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *