Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na. Baraka Messa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuilinda na kuitunza miundombinu ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHP), akisema kuwa mradi huo ni mali ya Watanzania na urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Rais Samia amesema hayo  Agosti 22, 2026, wilayani Rufiji mkoani Pwani, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema kuwa Serikali imewekeza rasilimali kubwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme na kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa wananchi na kusisitiza kuwa jukumu la kulinda mradi huo si la Serikali pekee, bali ni la kila Mtanzania, kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa. Mradi huu ni wetu sote, Ni lazima tuulinde, tuutunze na tuhakikishe unaendelea kutoa manufaa kwa Watanzania wa leo na vizazi vijavyo,” amesema Rais Samia. Ameongeza kuwa Mradi wa JNHP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati nchini, hivyo akawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika katika kulinda miundombinu ya mradi huo. Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa megawati 2,115 kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya majumbani, viwandani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, uzinduzi  wa kituo hicho unafungua sura mpya katika safari ya Tanzania ya kuimarisha usalama wa nishati, huku Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa washiriki wakuu katika kulinda na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini.

Na Baraka Messa – MAELEZO Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu cha huduma za matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi nchini Tanzania na Afrika Mashariki, kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 10 uliowezesha hospitali hiyo kutoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingi za ukanda huu. Hayo yanaelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu mafanikio ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya. Msigwa anasema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 kuimarisha Hospitali ya Benjamin Mkapa ili ifikie viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa. “Hospitali ya Benjamin Mkapa leo inatoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi si Tanzania pekee, bali hata katika Afrika Mashariki, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 katika kipindi cha miaka 10 kuifanya hospitali hii kuwa kituo cha kisasa cha matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi,” anasema Msigwa. Anafafanua kuwa uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya kutolea huduma za kibingwa, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa, uboreshaji wa mifumo ya Tehama pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na kuboresha mazingira yao ya kazi. Msigwa anasema mwaka 2015 hospitali hiyo ilikuwa na watumishi 20 pekee, lakini kufikia mwaka 2026 idadi hiyo imeongezeka na kufikia watumishi 1,076, wakiwemo madaktari bingwa 105. Anasema hospitali hiyo sasa inatoa huduma 17 za kibingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, huduma za radiolojia ya kisasa pamoja na uchujaji wa damu (dialysis). “Huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu zinapatikana Hospitali ya Benjamin Mkapa na ni miongoni mwa huduma adimu ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi nchini na Afrika Mashariki,” anaeleza . Msigwa anasema kuimarika kwa huduma hizo kumepunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya Watanzania waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta matibabu, jambo ambalo limeokoa fedha nyingi za Serikali na wananchi. HOSPITALI BENJAMINI YAWA KIVUTIO WAGONJWA KUTOKA MATAIFA YA NJE Msigwa anasema hospitali hiyo sasa imekuwa kivutio cha wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. “Tumewahudumia wagonjwa 2,897 kutoka Burundi na wagonjwa 526 kutoka Comoro. Pia wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za Afrika Mashariki wanaendelea kuja kupata matibabu hapa, Tunawatibu ndugu zetu, lakini pia huu ni utalii wa matibabu unaoingizia taifa mapato,” anasema Msigwa. Anasema kuwa mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuanza kushindana na mataifa yaliyopiga hatua katika utalii wa matibabu kama India, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakipokea wagonjwa wengi kutoka Tanzania. “Kwa muda mrefu Watanzania walikuwa wakitumia fedha nyingi kwenda kutibiwa nje ya nchi, hususan India,..Sasa Serikali imewekeza kuhakikisha huduma hizo zinapatikana hapa nchini ili wananchi wapate matibabu bora na wakati huohuo Tanzania inufaike kupitia utalii wa matibabu,” anasema Msigwa. Pia Msigwa amesema Julai 10, 2025 Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzisha International Clinic, kitengo maalumu kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na wa kimataifa. Anasema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo, wagonjwa 18,607 wamehudumiwa, wakiwemo wagonjwa 390 kutoka mataifa mbalimbali, huku huduma ya Master Health Check-up ikiendelea kuvutia watu wanaohitaji uchunguzi wa afya kwa kiwango cha kimataifa. Aidha anasema hospitali hiyo pia imeanzisha eneo maalumu la huduma binafsi kwa wagonjwa wanaohitaji faragha na huduma za kiwango cha juu bila kuchangamana na wagonjwa wengine. Anasema Huduma hizi zinafanana na zile zinazotolewa katika hospitali za kisasa duniani kama za China, Ujerumani na India, huku dhamira ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ndani ya nchi na wakati huohuo Tanzania inakuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika. Kuimarika kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali mbalimbali za rufaa nchini ni sehemu ya malengi ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani wa kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu.

Na Josephina Lupasha na Immaculate Makilika – MAELEZO Ulimwenguni kote miundombinu imeendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi. Barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, nishati na teknolojia ya mawasiliano ni muhimu katika kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuunganisha masoko na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa. Kwa upande wa Afrika, kupitia taasisi ya fedha Africa50 inayoshirikiana na Serikali mbalimbali barani Afrika inabadili taswira na hadhi ya Afrika kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kimkakati, uwekezaji wenye tija na mageuzi ya kiuchumi na teknolojia barani humo. Taasisi hiyo inaandaa miradi hadi kufikia hatua ya kupata wawekezaji na kutafuta wawekezaji kwa utaratibu wa equity investment kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kutoka kwa wawekezaji na wafadhili wa ndani na nje ya Afrika. Lengo ni kuharakisha utekelezaji wa miundombinu yenye ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha. Aidha, miundombinu ya kipaumbele ni pamoja na nishati, uchukuzi, elimu, afya, mawasiliano na fedha (fintech). Ili kuendelea kutoa mchango wake hadhimu kwa Afrika, Tanzania imeendelea kujijengea nafasi muhimu katika ramani ya uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuamua kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), lililofanyika Agosti 5 – 6, 2026, jijini Dar es Salaam. Hivyo inategemewa mkutano utavutia wawekezaji wa kimataifa kutangaza miradi ya kimkakati kama reli ya SGR, Bandari ya Dar es Salaam, uzalishaji wa umeme, na miundombinu ya TEHAMA. Mkutano huo ambao umeleta pamoja viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, katika jitihada za kutafuta namna ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika, umekuwa nyenzo muhimu ya kuutangazia ulimwengu kuhusu utayari wa Afrika na kutumia fursa zake Afrika katika kujiletea maendeleo ya kweli. Kwa Tanzania, mkutano huo umekuwa zaidi ya tukio la kimataifa, umekuwa fursa ya kuonesha uwezo, fursa na mwelekeo wa nchi katika kujenga uchumi unaotegemea miundombinu ya kisasa, uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anasema kuwa kuongezeka kwa imani kwa Tanzania kunatokana na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea nchini, fursa za uwekezaji na nafasi yake ya kimkakati kama lango linalounganisha Afrika na masoko ya kimataifa. Aidha, anasema Afrika inapaswa kujenga mustakabali wake kupitia uongozi madhubuti, mitaji na ushirikiano wa waafrika wenyewe, na kuwa bara la Afrika linaweza kutumia rasilimali zake, mitaji ya ndani na fursa zilizopo ili kupunguza pengo la maendeleo, kuongeza biashara na kuimarisha ushindani wake katika uchumi wa dunia. “Wananchi hawapimi maendeleo kwa matamko, bali kwa matokeo wanayoyaona katika maisha yao, Kwa msingi huo, Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora, nishati ya uhakika, bandari zenye ufanisi, reli za kisasa, miundombinu ya kidijitali na huduma nyingine zinazochochea uzalishaji, ajira na biashara” anasema Rais Samia. Akionesha utayari wa hatua iliyopigwa na Tanzania katika kuleta mageuzi ya kiuchumi anasema tayari imeweka msingi kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi na uboreshaji wa barabara na madaraja, maendeleo ya viwanja vya ndege pamoja na miradi ya nishati na miundombinu ya TEHAMA. Hata hivyo katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania 2050, yanayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaotegemea viwanda, ubunifu, rasilimali watu, maendeleo endelevu na miundombinu ya kisasa. Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi, huku ikilenga kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa kuwa na miundombinu ya kimkakati na kujenga ubia unaoweza kuvutia mitaji binafsi, teknolojia na ubunifu. Kwa hakika, Tanzania inaendelea kubaki na nafasi muhimu kama lango la nchi zisizo na bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pia inatoa fursa kubwa ya kuifanya nchi kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na uwekezaji. Uwezo wa bandari, reli, barabara na nishati unapoimarishwa kwa pamoja, Tanzania inaweza kuongeza mchango wake katika minyororo ya thamani ya kikanda na bara. Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sidi Quld Tah akizungumza pia katika Mkutano huo wa Africa50 anasema kuwa Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake, ikiwemo gesi asilia, kwa ufanisi ili kuchochea ukuaji wa viwanda, kuimarisha ustahimilivu wa nishati na kuboresha maisha ya wananchi. Anasisitiza “Akiba ya gesi asillia barani Afrika inafikia takribani asilimia saba ya akiba ya gesi duniani, rasilimali hizi zikitumika kwa busara zinaweza kusaidia kuimarisha viwanda, kuongeza ustahimilivu wa nishati na kuchochea ustawi wa wananchi wetu”. Dkt. Tah anapendekeza kuwa ili Afrika itimize malengo yake na kupata maendeleo inayokusudia inatakiwa kufanyika kwa uwekezaji wa haraka barani humo, kuimarisha matumizi ya mitaji ya ndani, mifumo ya kifedha na taasisi za kifedha ili kuziba pengo la ufadhili wa miundombinu. Aidha, anaeleza kuwa Afrika kwa kushirikiana Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Afrika50 zitaendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa, kupunguza hatari za uwekezaji na kuvutia mitaji zaidi. Naye, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, anasema kuwa uamuzi huo wa Africa50 kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Infra for Africa Forum, ni heshima na ishara ya imani kwa Tanzania pamoja na maono yake ya kujenga Afrika iliyounganishwa, yenye ustawi na maendeleo. “Kwa kipindi cha miaka 10, Africa50 imejijenga kama taasisi muhimu katika kuchochea uwekezaji wa miundombinu barani Afrika kupitia uandaaji wa miradi, uhamasishaji wa mitaji na uwekezaji wa kimkakati,” anasema Balozi Omar Tanzania, imekuwa mwananchama katika Africa50 kuanzia mwaka 2023, ambao umefungua fursa ya nchi kushiriki katika mfumo mpana wa kuandaa miradi, kuhamasisha uwekezaji na kukuza maendeleo endelevu ya miundombinu. Balozi Omar anaeleza manufaa ya uanachama wa Tanzania katika Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kuhusisha maandalizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini, ikiwemo maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini LNG, miundombinu ya usafirishaji wa umeme pamoja na ushirikiano katika upanuzi wa huduma za usafishaji wa figo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Inaelezwa kuwa kupitia Mkutano huo pia umeiwezesha Tanzania kuwasilisha fursa mbalimbali

▪️Ujenzi Wake Kuanza Oktoba 2026 ▪️Fidia Shilingi bil 8.5 Imeshalipwa kwa Wananchi Waliopisha Mradi Na Adelina Johnbosco – MAELEZO Tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dodoma linaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu kufuatia ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Farkwa utakaoanza kujengwa Oktoba mwaka huu. Bwawa hilo litakalojengwa wilayani Chemba, kata ya Farkwa mkoani Dodoma litakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 128 kwa siku na kuhifadhi lita bilioni 390 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22. Bwawa hili litahudumia hasa wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino na maeneo mengine ndani na maeneo ya karibu na mkoa wa Dodoma, lengo ni kutokomeza kabisa upungufu wa maji ndani ya mkoa huo. Ujenzi wa bwawa la Farkwa utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi bilioni 163.43 hadi kukamilika kwake. Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 8.5 zimelipwa kama fidia kwa wananchi kutoka katika vijiji viwili vya Mombose na Bubutole waliopisha ujenzi. “Tuliambiwa tunahamishwa na kulipwa, mwaka 2017 tathmini ilifanyika katika maeneo yetu, ila ukiwa bado hujapokea kitu mkononi unaona kama haiwezekani, lakini mwaka 2019 tukalipwa fidia zetu, tukaanza maisha mapya na yenye matumaini zaidi katika kijiji cha Sankwaleto kwenye makazi mapya” Bi. Rahma Petro, mkazi wa Farkwa Hadi hapa, tayari inaonekana Dodoma yenye ukijani wakati wote, iwe mvua iwe jua, hakuna tena ukame katika mkoa huu pale mradi huu utakapokuwa umekamilika, yale yaliyokuwa yanasubiriwa kufanyika wakati wa kipindi cha mvua pekee yatafanyika pia kipindi cha kiangazi. “Tumeajiandaa kwa vingi kwa kweli, kijamii na kiuchumi, tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutafuga samaki na mengine mengi, ni furaha tupu. Hii ilikuwa ni hadithi ya muda mrefu ambayo tumezaliwa tukaikuta kutoka kwa wazee wetu, hakika leo inatimia” Bw. Suleiman Gawa, mkazi wa Farkwa Akiwa katika eneo utakapotekelezwa mradi huo, hivi karibuni, Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia ambaye ni mtaalam wa maji chini ya ardhi kutoka Wizara ya Maji, amebainisha uwepo wa maji ya akiba kwa watumiaji kutokana na wingi wa lita za maji utaokaozalishwa na bwawa hilo. “Mradi huu unaanza mwezi Oktoba, 2026, maandalizi yako tayari na baada ya kukamilika kwa mradi, si kwamba utaondoa kero ya maji tu bali hata kuchochea miradi mbali mbali ya kiuchumi kama vile kilimo cha umwagiliaji kisichosubiri msimu, ufugaji wa samaki na itakuwa ongezeko la maji katika hifadhi ya pori la akiba Swagaswaga Chemba, wanyama hifadhini watapata maji ya kunywa ya kutosha tofauti na hali ilivyo kwa sasa” Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia Mradi huu mwisho wake ni kuleta maji, lakini suala la ajira wakati na baada ya mradi ni vitu vinavotegemewa pakubwa. Mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya cha Sankwaleto, akaongea kuhusu wazawa kupata fursa mbalimbali kutokana na mradi huo. “Kama kiongozi tumeshashirikishwa na kuhakikishiwa kwamba, sisi wazawa tutapewa kipaumbele katika fursa mbalimbali zinazotokana na huu mradi ikiwemo ajira wakati na baada ya ujenzi, hivyo nawasihi vijana na wakazi wenzangu wa hapa kuwa tayari, tusikubali kukaa kinyonge katika kuchangamkia fursa katika hizi” Bw. Khalifa Salum, mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya Sankwaleto Si nyumba na umiliki wa ardhi pekee kwenye maeneo ya makazi mapya waliohamia wananchi waliopisha mradi, bali shule na zahanati vimejengwa kwa ajili ya kuwahudumia. “Kijiji cha Sankwaleto kimejengwa shule ya msingi na imeshaanza kazi, kuna nyumba za walimu na wanafunzi wote waliokuwa wakisoma kule kwenye vijiji vya zamani wako kwenye shule mpya wanaendelea na masomo, hakuna kilichosimama, pia zahanati inayowahudumia wananchi, kwa kweli tunashukuru sana” – Bi. Agnes Msote, Diwani wa kata ya Farkwa Kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kunatarajiwa kuimarisha usalama wa maji katika jiji la Dodoma na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo. Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji nchini kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upatikanaji wake maeneo yote hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na kuhakikisha juhudi za kufikisha huduma za maji katika vijiji vyote nchini linatimia ili kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO* Sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Inatoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania, inachangia usalama wa chakula na ni chanzo kikuu cha malighafi kwa viwanda. Hata hivyo, kwa miaka mingi sekta hii ilikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji, hali iliyowafanya wakulima wengi kuendelea na kilimo cha kujikimu badala ya kilimo cha biashara. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita , hali hiyo imeanza kubadilika kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kupitia ongezeko la mtaji na upanuzi wa utoaji wa mikopo, benki hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Serikali imeendelea kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa mikopo yenye masharti nafuu. Lengo kuu ni kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kukuza kilimo cha kisasa kinachozalisha kwa tija. Mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani alifanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Hatua hiyo ilienda sambamba na kuiongezea TADB mtaji kutoka shilingi bilioni 60 hadi bilioni 268 kupitia uwekezaji wa Serikali wa shilingi bilioni 208. Jitihada hizo ziliendelea mwaka 2024 ambapo Serikali, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliongeza mtaji wa shilingi bilioni 174.16 na kufanya mtaji wa benki kufikia shilingi bilioni 442.16. Mwaka 2025 Serikali iliongeza tena shilingi bilioni 10, hivyo mtaji kufikia shilingi bilioni 452.16. Ongezeko hilo la mtaji limeongeza uwezo wa TADB kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, TADB imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.55. Kati ya kiasi hicho, zaidi ya asilimia 80, sawa na takribani shilingi trilioni 1.24, kimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita. Aidha, idadi ya wanufaika imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kabla ya mwaka 2021, benki ilikuwa imewafikia takribani wakulima milioni 1.6. Hadi sasa, zaidi ya wakulima milioni 2.6 wamepata mikopo ya moja kwa moja, huku zaidi ya wakulima 659,000 wakinufaika kupitia Dirisha la Dhamana la Mikopo ya Wakulima Wadogo. Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, anasema dirisha hilo limepanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima ambao hapo awali walishindwa kupata mikopo kutokana na ukosefu wa dhamana. Anasema kupitia utaratibu huo, TADB hutoa dhamana kwa benki na taasisi za fedha ili ziweze kuwakopesha wakulima wadogo kwa masharti nafuu. “TADB inaendelea kutoa mikopo katika sekta zote za kilimo. Pia tunaziwezesha benki nyingine kwa kuzipa fedha za muda mrefu na dhamana ili nazo ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu,” anasema Nyabundege na kuongeza kuwa kwa sasa, dirisha hilo lina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 692 na linatekelezwa kupitia benki 19 nchini. Upatikanaji wa mitaji umeongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Mwaka 2021 Tanzania ilizalisha tani milioni 17.148 za mazao ya chakula, lakini kufikia mwaka 2025 uzalishaji umeongezeka hadi tani milioni 22.8. Ongezeko hilo limeifanya Tanzania kufikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130, hali inayowezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Mbali na usalama wa chakula, mikopo ya TADB imeongeza matumizi ya pembejeo bora, teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo, hatua ambazo zimeongeza tija na kipato cha wakulima. Matokeo yake yanaonekana pia katika mazao ya biashara. Kwa mfano, uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 210,000 mwaka 2021 hadi tani 750,000 mwaka 2025. Wakati huo huo, mapato yatokanayo na mauzo ya mazao nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 hadi dola bilioni 5. Ukuaji huo unaonesha namna upatikanaji wa mitaji unavyochangia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara ya mazao na kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Serikali pia ilianzisha kifurushi cha uchochezi cha shilingi trilioni moja kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili benki za biashara ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu. Sambamba na hilo, Benki Kuu ilizikopesha benki za biashara kwa riba ya asilimia tatu ili ziweze kutoa mikopo kwa wakulima kwa riba isiyozidi asilimia 10. Kabla ya hatua hiyo, wakulima wengi walikabiliwa na riba kati ya asilimia 20 na 25, kiwango kilichowafanya wengi kushindwa kukopa. Hatua hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa mikopo inayokwenda kwenye sekta ya kilimo. Mikopo ya sekta hiyo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.3 kabla ya mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 5.8. Athari chanya zimeonekana pia katika sekta ya benki ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa na benki nchini imeongezeka kutoka shilingi trilioni 18.1 mwaka 2021 hadi trilioni 44.7, huku mali za benki zikifikia shilingi trilioni 77.7. Ukuaji huo unaonesha jinsi uwekezaji katika sekta ya uzalishaji unavyochochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, hususan sekta ya fedha. Katika mwaka wa fedha 2026/27, TADB imejipanga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Aidha, benki hiyo inalenga kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, kuwawezesha vijana na wanawake kupata huduma za kifedha, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo. Pia itaendelea kuchochea uongezaji thamani wa mazao ya kilimo ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na kimataifa, sambamba na kuunga mkono ajenda ya uchumi wa viwanda na diplomasia ya uchumi. Kwa ujumla, uwekezaji wa Serikali katika TADB umeonyesha kuwa upatikanaji wa mitaji ni nguzo muhimu ya mageuzi ya sekta ya kilimo. Kupitia mikopo hiyo, wakulima wameongeza uzalishaji na kipato, usalama wa chakula umeimarika, sekta ya benki imekua na uchumi wa Taifa umeendelea kupata nguvu. Kadri TADB inavyoendelea kupanua huduma zake, kilimo kinazidi kuwa biashara yenye tija, chanzo cha ajira kwa vijana na nguzo imara ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Mageuzi ya kidijitali katika sekta ya ununuzi wa umma yanaendelea kuleta matokeo makubwa nchini kupitia mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) ambao umekua mkombozi kwa watoa huduma na Serikali, ukiimarisha uwazi, uwajibikaji na ushindani katika matumizi ya fedha za umma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Dennis Simba anabainisha hayo katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma lililowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi wa ununuzi wa umma na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hilo lililofanyika jijini Arusha lililoogozwa na kaulimbiu isemayo “Kutumia Fursa ya Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani kuelekea Dira ya Taifa 2050,” limeonesha kuwa ununuzi wa umma si shughuli ya kiutawala pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ushindani wa biashara na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija. Mkurugenzi huyo wa PPRA anaeleza kuwa tangu kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huo, Julai 1, 2023, uendeshaji wa shughuli za ununuzi nchini kwa kiasi kikubwa umebadilika kwa kuwa mfumo huo unawezesha usajili wa wazabuni, uchakataji wa zabuni kwa njia ya mtandao, usimamizi wa mikataba, malipo ya mikataba, minada ya kielektroniki pamoja na matumizi ya katalogi ya bidhaa na huduma. Mbali na kurahisisha utoaji wa huduma, Bw. Simba anasema PPRA imeendelea kuuboresha mfumo huo kwa kuanzisha moduli ya kisasa ya ufuatiliaji wa vihatarishi katika michakato ya ununuzi kwa wakati halisi. Teknolojia hiyo inaiwezesha Mamlaka kubaini mapema viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa fedha za umma au kukiukwa kwa taratibu za ununuzi, ikiwemo upangaji wa matokeo ya zabuni, ushindani usioridhisha, kula njama kati ya wazabuni na vitendo vya udanganyifu. Anasema hatua hiyo imeongeza uwezo wa PPRA kuchukua hatua za haraka kabla dosari hazijasababisha hasara kwa Serikali, huku ikiimarisha uadilifu na uwazi katika mnyororo mzima wa ununuzi wa umma. Mafanikio ya matumizi ya NeST yameonekana kupitia ongezeko la ushiriki wa wadau ambapo hadi Juni 30, 2026, zaidi ya wazabuni 45,270 walikuwa wamesajiliwa katika mfumo huo, huku asilimia 95 wakiwa wazabuni wa ndani. Aidha, zaidi ya taasisi nunuzi 62,847 na watumiaji zaidi ya 161,704 walikuwa wakitumia mfumo huo. Anasema katika kipindi hicho, zabuni 286,903 zilitangazwa kupitia NeST na zaidi ya tuzo za zabuni 181,057 zenye thamani ya shilingi trilioni 14.5 zikatolewa kwa njia ya mfumo huo, hatua inayoonesha kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika kusimamia fedha za umma. Aidha, ameeleza kuwa PPRA imeendelea kuwezesha ushiriki wa makundi maalumu katika fursa za zabuni. Kupitia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, Taasisi Nunuzi zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Matokeo ya utekelezaji huo yanaonekana ambapo hadi Julai 28, 2026 zaidi ya makundi maalumu 23,590 yalikuwa yamesajiliwa katika NeST na tuzo 745 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 53.68 zilitolewa kwa makundi maalumu. Hii inaonesha kuwa mageuzi ya kidijitali hayajaboresha tu ufanisi wa Serikali, bali pia yamepanua fursa za kiuchumi kwa makundi yaliyokuwa hayashiriki kwa kiwango kikubwa hapo awali. Mbali na manufaa ya kiuchumi, matumizi ya NeST yamechangia pia utunzaji wa mazingira. Utafiti wa PPRA unaonesha kuwa matumizi ya mfumo huo yalipunguza uzalishaji wa metariki tani 64,028 za hewa ya ukaa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kutokana na kupungua kwa matumizi ya karatasi. Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambulika kimataifa. Mfumo wa NeST umepata tuzo mbalimbali za ubunifu na mazingira, ikiwemo kutajwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali duniani katika tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026 zilizofanyika Geneva, Uswizi. Sambamba na mafanikio hayo, PPRA imeendelea kuimarisha ukaguzi wa ukidhi na thamani halisi ya fedha ili kuhakikisha taasisi zote zinazingatia sheria na taratibu za ununuzi wa umma. Jitihada hizo zinaenda sambamba na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza uwajibikaji, kudhibiti mianya ya ubadhirifu na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi. Kadhalika, Mamlaka hiyo imeendelea kupanua ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi kupitia kubadilishana uzoefu katika ununuzi endelevu, huku nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Benki ya Dunia zikiendelea kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kujenga na kutumia Mfumo wa NeST. Kwa ujumla, mafanikio ya PPRA yanaonesha kuwa uwekezaji katika mifumo ya kidijitali si tu umeongeza uwazi na ufanisi wa ununuzi wa umma, bali pia umeifanya sekta hiyo kuwa chombo muhimu cha kukuza uchumi shindani, jumuishi na endelevu. Kadiri matumizi ya NeST yanavyoendelea kuongezeka, ndivyo nafasi ya ununuzi wa umma katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inavyozidi kuimarika.

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Mkoa wa Kigoma umekuwa na nafasi ya kimkakati katika biashara ya kikanda kutokana na mwambao wake katika Ziwa Tanganyika na ukaribu wake na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia. Hata hivyo, changamoto za miundombinu ya usafirishaji zimekuwa zikizuia mkoa huo kutumia kikamilifu fursa hiyo, huku gharama za usafirishaji zikiwa kubwa na safari za mizigo kuchukua muda mrefu. Sasa hali hiyo imeanza kubadilika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora–Kigoma, uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na maboresho ya Bandari ya Kigoma. Miradi hiyo inatarajiwa kuibadili Kigoma kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari. Katika kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uchukuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua meli nne mpya za mizigo, akaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Tabora–Kigoma na kukagua maendeleo ya maboresho ya Bandari ya Kigoma. Hatua hizo zinaakisi mkakati wa Serikali wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara. Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, anasema Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia kutokana na nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika. Anasema kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. “Kwa nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika, Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia. Miradi hii ya SGR na meli mpya za mizigo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema Prof. Mbarawa. Meli hizo nne mpya, ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo, zinatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Kigoma kuhudumia zaidi ya tani 832,000 za mizigo kwa mwaka. Mbali na kuongeza ufanisi wa usafirishaji, uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea biashara na kuzalisha takribani ajira 600 za moja kwa moja katika sekta mbalimbali. Kwa wakazi wa Kigoma, uwekezaji huo una maana zaidi ya kujengwa kwa miundombinu. Ni mwanzo wa zama mpya za fursa za kiuchumi, ajira na uwekezaji. Kuimarika kwa usafiri wa reli na majini kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupanua masoko na kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi. Bi. Asha Mussa, mkazi wa Kibirizi, anasema wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu maendeleo ya aina hiyo. “Tunaamini meli mpya na reli ya kisasa zitafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi. Kuimarika kwa miundombinu ya usafiri kutasaidia wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali kupata nafasi zaidi za kujikwamua kiuchumi.” Hisia kama hizo zinaungwa mkono na wananchi wengi wanaoamini kuwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya usafirishaji kwa miaka mingi. Bw. John Mwakalinga, mkazi wa Kigoma Mjini, anasema gharama kubwa za usafirishaji zimekuwa zikikwamisha biashara na kupunguza ushindani wa bidhaa katika masoko. “Kwa miaka mingi usafirishaji wa bidhaa ulikuwa na changamoto nyingi na gharama kubwa. Tunaamini SGR pamoja na maboresho ya bandari utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda masoko ya ndani na nchi jirani, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara na kuinua kipato cha wananchi.” Mradi wa Reli ya Kisasa wa Tabora–Kigoma wenye urefu wa kilometa 506 unajengwa kwa gharama ya takribani dola za Marekani bilioni 2.7. Mradi huo utaunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa unaofika Dar es Salaam, hivyo kuimarisha Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Zambia. Faida za miradi hiyo hazitaishia katika kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria pekee. Pia zinatarajiwa kuongeza ushindani wa biashara za kikanda, kuvutia uwekezaji, kuchochea uzalishaji wa bidhaa na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kadri miradi hiyo inavyoendelea kukamilika, Kigoma inaelekea kujidhihirisha kama kitovu kipya cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati. Uwekezaji wa Serikali katika reli, bandari na usafiri wa majini unaweka msingi imara wa maendeleo endelevu, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi. Kwa hakika, kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, kuanza kwa huduma za meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi. Kigoma itaimarika kama lango kuu la biashara katika ukanda huu, huku Tanzania ikiendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara Afrika Mashariki na Kati.