Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Ushirikiano na Singapore Kufungua Fursa za Uchumi wa Kidigitali kwa Vijana

June 9, 2026
MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

Na Scolastica Sambi – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore unafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya vijana, uwekezaji na uchumi wa kidijitali, akieleza kuwa Tanzania inalenga kujifunza na kushirikiana na taifa hilo ili kuharakisha safari ya maendeleo ya kizazi kijacho.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, June 9, 2026 baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, Dkt. Samia amesema ziara hiyo ya kihistoria, ambayo ni ya kwanza kufanywa na Rais wa Singapore nchini Tanzania, imekuja wakati muafaka ambapo mataifa hayo mawili yanatimiza miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia.

Rais Samia amesema pamoja na kuimarisha biashara na uwekezaji, viongozi hao wamejadili kwa kina namna ya kuwawezesha vijana wa Tanzania kupitia elimu, mafunzo ya ujuzi, ujasiriamali na ubunifu ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia na maarifa.

“Serikali imeweka kipaumbele kikubwa kwa vijana katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiamini kuwa ndani ya miaka 25 ijayo vijana hao ndio watakaokuwa viongozi, wabunifu na watendaji wakuu wa uchumi wa Tanzania” Amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania pia imejikita katika utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidijitali unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma, huku vijana wakitarajiwa kuwa nguvu kazi kuu ya mageuzi hayo.

Aidha, amebainisha kuwa kiwango cha sasa cha biashara kati ya Tanzania na Singapore, kinachofikia dola za Marekani milioni 269 pamoja na miradi 36 ya uwekezaji kutoka Singapore, bado hakilingani na ukubwa wa urafiki uliopo kati ya mataifa hayo mawili.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania pia imeikaribisha Singapore kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Rais Samia amesema ujio wa Rais Tharman Shanmugaratnam nchini Tanzania unaashiria mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano wa kimkakati, akisisitiza kuwa kuimarika kwa mahusiano na Singapore, taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi duniani, kutachangia kukuza fursa za maendeleo na kuongeza hadhi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *