Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Mikopo ya TADB Yachochea Mapinduzi ya Kilimo na Ukuaji wa Uchumi

August 7, 2026

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO*

Sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Inatoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania, inachangia usalama wa chakula na ni chanzo kikuu cha malighafi kwa viwanda. Hata hivyo, kwa miaka mingi sekta hii ilikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji, hali iliyowafanya wakulima wengi kuendelea na kilimo cha kujikimu badala ya kilimo cha biashara.

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita , hali hiyo imeanza kubadilika kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kupitia ongezeko la mtaji na upanuzi wa utoaji wa mikopo, benki hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Serikali imeendelea kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa mikopo yenye masharti nafuu. Lengo kuu ni kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kukuza kilimo cha kisasa kinachozalisha kwa tija.

Mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani alifanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Hatua hiyo ilienda sambamba na kuiongezea TADB mtaji kutoka shilingi bilioni 60 hadi bilioni 268 kupitia uwekezaji wa Serikali wa shilingi bilioni 208.

Jitihada hizo ziliendelea mwaka 2024 ambapo Serikali, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliongeza mtaji wa shilingi bilioni 174.16 na kufanya mtaji wa benki kufikia shilingi bilioni 442.16. Mwaka 2025 Serikali iliongeza tena shilingi bilioni 10, hivyo mtaji kufikia shilingi bilioni 452.16.

Ongezeko hilo la mtaji limeongeza uwezo wa TADB kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.

Kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, TADB imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.55. Kati ya kiasi hicho, zaidi ya asilimia 80, sawa na takribani shilingi trilioni 1.24, kimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Aidha, idadi ya wanufaika imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kabla ya mwaka 2021, benki ilikuwa imewafikia takribani wakulima milioni 1.6. Hadi sasa, zaidi ya wakulima milioni 2.6 wamepata mikopo ya moja kwa moja, huku zaidi ya wakulima 659,000 wakinufaika kupitia Dirisha la Dhamana la Mikopo ya Wakulima Wadogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, anasema dirisha hilo limepanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima ambao hapo awali walishindwa kupata mikopo kutokana na ukosefu wa dhamana.

Anasema kupitia utaratibu huo, TADB hutoa dhamana kwa benki na taasisi za fedha ili ziweze kuwakopesha wakulima wadogo kwa masharti nafuu.

“TADB inaendelea kutoa mikopo katika sekta zote za kilimo. Pia tunaziwezesha benki nyingine kwa kuzipa fedha za muda mrefu na dhamana ili nazo ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu,” anasema Nyabundege na kuongeza kuwa kwa sasa, dirisha hilo lina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 692 na linatekelezwa kupitia benki 19 nchini.

Upatikanaji wa mitaji umeongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Mwaka 2021 Tanzania ilizalisha tani milioni 17.148 za mazao ya chakula, lakini kufikia mwaka 2025 uzalishaji umeongezeka hadi tani milioni 22.8.

Ongezeko hilo limeifanya Tanzania kufikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130, hali inayowezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mbali na usalama wa chakula, mikopo ya TADB imeongeza matumizi ya pembejeo bora, teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo, hatua ambazo zimeongeza tija na kipato cha wakulima.

Matokeo yake yanaonekana pia katika mazao ya biashara. Kwa mfano, uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 210,000 mwaka 2021 hadi tani 750,000 mwaka 2025. Wakati huo huo, mapato yatokanayo na mauzo ya mazao nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 hadi dola bilioni 5.

Ukuaji huo unaonesha namna upatikanaji wa mitaji unavyochangia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara ya mazao na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Serikali pia ilianzisha kifurushi cha uchochezi cha shilingi trilioni moja kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili benki za biashara ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu.

Sambamba na hilo, Benki Kuu ilizikopesha benki za biashara kwa riba ya asilimia tatu ili ziweze kutoa mikopo kwa wakulima kwa riba isiyozidi asilimia 10. Kabla ya hatua hiyo, wakulima wengi walikabiliwa na riba kati ya asilimia 20 na 25, kiwango kilichowafanya wengi kushindwa kukopa.

Hatua hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa mikopo inayokwenda kwenye sekta ya kilimo. Mikopo ya sekta hiyo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.3 kabla ya mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 5.8.

Athari chanya zimeonekana pia katika sekta ya benki ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa na benki nchini imeongezeka kutoka shilingi trilioni 18.1 mwaka 2021 hadi trilioni 44.7, huku mali za benki zikifikia shilingi trilioni 77.7.

Ukuaji huo unaonesha jinsi uwekezaji katika sekta ya uzalishaji unavyochochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, hususan sekta ya fedha.

Katika mwaka wa fedha 2026/27, TADB imejipanga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Aidha, benki hiyo inalenga kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, kuwawezesha vijana na wanawake kupata huduma za kifedha, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo.

Pia itaendelea kuchochea uongezaji thamani wa mazao ya kilimo ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na kimataifa, sambamba na kuunga mkono ajenda ya uchumi wa viwanda na diplomasia ya uchumi.

Kwa ujumla, uwekezaji wa Serikali katika TADB umeonyesha kuwa upatikanaji wa mitaji ni nguzo muhimu ya mageuzi ya sekta ya kilimo. Kupitia mikopo hiyo, wakulima wameongeza uzalishaji na kipato, usalama wa chakula umeimarika, sekta ya benki imekua na uchumi wa Taifa umeendelea kupata nguvu. Kadri TADB inavyoendelea kupanua huduma zake, kilimo kinazidi kuwa biashara yenye tija, chanzo cha ajira kwa vijana na nguzo imara ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *