Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Katika bara linaloendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika afya ya uzazi, mama na mtoto, juhudi za kuweka maisha ya wanawake na watoto katika nafasi ya juu ya ajenda za maendeleo zimeendelea kupata msukumo mpya. Safari hiyo imepata nguvu jijini Arusha, ambako Wabunge kutoka Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Bara la Afrika kupitia Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU) wameunga mkono ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika. Uungwaji mkono huo umetolewa Oktoba 8, 2026, katika mkutano wa pembezoni mwa Mkutano wa 153 wa IPU, uliozikutanisha nchi mbalimbali za Afrika na wadau wa maendeleo ya afya duniani kujadili namna ya kuimarisha sera, mifumo ya utoaji huduma, uwekezaji na uwajibikaji katika sekta ya afya. Kwa Tanzania, mjadala huo unaenda sambamba na msisitizo wa Rais Samia wa kuhakikisha afya ya mama, mtoto na vijana inakuwa sehemu muhimu ya juhudi za kujenga jamii yenye afya na yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Ajenda inayovuka mipaka Kiongozi wa Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Wabunge wa Bara la Afrika kupitia IPU na Spika wa Jamhuri ya Chad, Mhe. Ali Kolotou Tchaïmi, amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuunganisha nguvu, kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuwa na agenda ya pamoja ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Kauli hiyo inaonyesha namna suala la afya ya mama na mtoto linavyotazamwa si kama jukumu la nchi moja pekee, bali changamoto ya bara inayohitaji mshikamano, uzoefu wa pamoja na hatua zinazotekelezwa kwa ushirikiano. Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Mhe. Angela Didiza, amesema Afrika inaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kuendeleza afya ya wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana. Amesisitiza kuwa uongozi wa kisiasa una nafasi muhimu katika kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji wa hatua za kibunge zinazolenga kuboresha huduma za afya. Kauli hiyo ni ishara nyingine ya namna juhudi zinazofanywa Tanzania zinavyoweza kuwa sehemu ya maarifa na uzoefu ambao nchi nyingine za Afrika zinaweza kujifunza na kuuboresha kulingana na mazingira yao. Uwekezaji lazima uende sambamba na matokeo Katika mjadala huo, Spika wa Bunge la Botswana, Mhe. Dithapelo Keorapetse, amegusa eneo muhimu la uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za afya. Amesema uwekezaji pekee hautoshi, bali nchi zinapaswa kuhakikisha rasilimali zinazotengwa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayopimika kwa wananchi. “Uwekezaji pekee hautoshi, bado tunakabiliwa na changamoto katika matokeo ya afya, hali hii inaonesha umuhimu wa kuangalia ufanisi wa matumizi ya rasilimali,” amesema. Mtazamo huo unaifanya ajenda ya afya kuwa zaidi ya kuongeza bajeti, kwa kuhitaji pia mifumo imara ya ufuatiliaji, uwajibikaji na kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa inaleta mabadiliko katika maisha ya wananchi. IPU Yaahidi Kuwa Mshirika wa Vitendo Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema juhudi za Rais Samia katika kuimarisha afya ya uzazi zinapaswa kuungwa mkono. Amesisitiza kuwa utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa viongozi ni muhimu katika kuhakikisha wataalamu wa afya na mifumo ya afya inafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kwa mtazamo huo, dhamira ya kisiasa ndiyo inayoweza kubadilisha sera na ahadi kuwa hatua zinazoonekana katika jamii. “IPU inajidhatiti kuwa mshirika wa vitendo kwa mabunge katika kuhakikisha ahadi zinatafsiriwa kuwa hatua na matokeo chanya ya kuimarisha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto,” amesema Dkt. Tulia. Kauli hiyo inaweka wazi nafasi ya mabunge katika safari ya kufikia malengo ya afya, hususan katika kutunga sheria, kuidhinisha na kusimamia matumizi ya rasilimali pamoja na kuishinikiza Serikali kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Tanzania Yaendelea Kuweka Afya ya Mama na Mtoto Mbele Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania, huku Bunge likiwa na wajibu wa kusimamia rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya huduma hizo kwa niaba ya wananchi. Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Bunge katika kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika sekta ya afya unalenga maeneo yenye athari kubwa kwa maisha ya wananchi. Kwa Tanzania, ajenda hiyo imepewa mwelekeo mpana zaidi kupitia Mpango Kazi wa Rais Samia wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Barani Afrika 2026–2030. Sifuri Tatu: Dira ya Rais Samia kwa Afrika Mshauri wa Rais kuhusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema vifo vitokanavyo na uzazi barani Afrika vimepungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023. Hata hivyo, amesema Afrika bado inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani, hali inayodhihirisha ukubwa wa kazi iliyopo mbele. Ndiyo maana Mpango Kazi wa Rais Samia wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Barani Afrika 2026–2030 umejengwa katika azma ya kufikia Sifuri Tatu: sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, na sifuri ya watoto wasiochanjwa. Dira hii inaweka mkazo katika hatua zinazolenga kuhakikisha mwanamke anapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua, mtoto anapata huduma zinazohitajika tangu anapozaliwa, na kila mtoto anapata kinga kupitia chanjo. Kwa mantiki hiyo, ajenda ya Rais Samia haionekani tena kama jambo linalohusu Tanzania pekee, bali kama wito wa Afrika kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto ambayo bado inagusa maisha ya mamilioni ya wanawake na watoto. Uungwaji mkono uliotolewa na wabunge wa Afrika jijini Arusha ni ishara kwamba bara linaona umuhimu wa kuwa na sauti na hatua za pamoja katika eneo hili. Na wakati Afrika ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto zake za kiafya, msisitizo wa Rais Samia wa kuwekeza katika afya ya mama, mtoto na vijana unaendelea kupata nafasi katika mjadala mpana wa bara — mjadala unaolenga kuhakikisha maendeleo ya Afrika yanaanza na kulindwa kupitia afya na ustawi wa watu wake. Kwa sababu, Afrika yenye afya bora ya mama na mtoto ndiyo msingi wa Afrika yenye kizazi chenye nguvu, chenye tija na chenye uwezo wa kujenga maendeleo endelevu.
London, Oktoba 7, 2026 Kampuni ya ndege ya British Airways imetangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Uingereza na Tanzania kuanzia Mei 2027, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za utalii, biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Tangazo hilo limetolewa Oktoba 7, 2026 na Mkuu wa Masoko wa British Airways kwa Bara la Afrika, Asia na Pasifiki, Bw. Moran Birger, katika Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini London akieleza kuwa uamuzi huo umechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya watalii na wasafiri wanaoitembelea Tanzania, pamoja na maendeleo ya kiuchumi na ongezeko la uwekezaji nchini. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amepongeza uamuzi huo na kueleza kuwa kurejea kwa British Airways kutaendelea kuifungua Tanzania kwa dunia na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi na Taifa. Amesema Tanzania ina nafasi ya kuwa kitovu cha uwekezaji kwa masoko ya kikanda, hivyo wawekezaji wanapaswa kulitazama Taifa hilo kama jukwaa la kuwafikia wadau wa nchi mbalimbali. Dkt. Mwigulu amesema amani, utulivu na uongozi imara, pamoja na miundombinu ya barabara, SGR, bandari, viwanja vya ndege na upatikanaji wa umeme wa uhakika, ni miongoni mwa mambo yanayowezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini. Amesema mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yanahitaji pia umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa uchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imeandaa sera, mipango na malengo thabiti kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa, kwa lengo la kufungua fursa za uwekezaji na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.