Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Blogu

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa kufungua fursa mpya za maendeleo kwa Taifa linalolenga kuongeza uzalishaji, kukuza viwanda na kujenga uchumi shindani. Tanzania inapofikisha ziada ya Megawati 2,000 za umeme, hatua hiyo inaashiria uwezo mkubwa wa nchi katika kuzalisha nishati ambayo inapaswa kugeuzwa kuwa kichocheo cha uzalishaji, uwekezaji, viwanda, kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi. Uwepo wa megawati 2000 za ziada ni habari njema kwa Watanzania kuichangamkia fursa hiyo na kutumia nguvu ya umeme kujenga uchumi wenye tija na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa. Akiongea hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika Bariadi mkoani Simiyu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Tanzania kwa sasa ina ziada ya MW 2,000 za umeme, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya uzalishaji wa nishati ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, SADC na maeneo mengine ya Afrika. Ziada hiyo ya umeme inapaswa kutazamwa kama fursa ya uzalishaji. Wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kutumia mazingira hayo kuanzisha na kupanua viwanda, hasa viwanda vidogo na vya kati vinavyoweza kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao. Kilimo, mifugo, uvuvi na madini vinaweza kuongezewa thamani kupitia uchakataji unaotumia umeme, na hivyo kuongeza kipato na ajira. Mkulima, kwa mfano, hapaswi kuishia kuuza zao ghafi ikiwa anaweza kulichakata na kupata bidhaa yenye thamani zaidi. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, mazao ya nafaka yanaweza kuchakatwa, maziwa yanaweza kuongezwa thamani na mazao mengine yanaweza kuhifadhiwa au kusindikwa kwa kutumia teknolojia. Hapo ndipo umeme unapogeuka kuwa mtaji wa uzalishaji. Kwa wafanyabiashara na vijana, ongezeko la upatikanaji wa umeme linaweza kufungua milango ya shughuli mpya. Kuanzia karakana na mashine za uzalishaji hadi teknolojia, huduma za kidijitali na biashara zinazohitaji nishati ya uhakika. Fursa hiyo inahitaji ubunifu na hatua, si kusubiri. Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuifanya nguvu hiyo iwafikie wananchi. Kupitia Mradi wa Gridi Imara, unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bariadi, uwezo wa gridi unaendelea kuimarishwa ili kuongeza uhakika wa usambazaji wa umeme. Aidha, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 302 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, hatua iliyowezesha mkoa wa Simiyu kufikisha huduma hiyo katika vijiji vyote 478. Hii ni nafasi ya wananchi wa mijini na vijijini kuangalia umeme kwa jicho jipya. Si huduma ya kutumia majumbani pekee, bali ni rasilimali ya kuzalisha utajiri. Kila eneo lenye umeme linaweza kuwa eneo la uzalishaji ikiwa wananchi watatumia fursa hiyo kuanzisha biashara, viwanda na shughuli zinazoongeza thamani. Tanzania pia ina rasilimali nyingi zinazoweza kuunganishwa na nguvu hii ya nishati. Ardhi, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini vinaweza kutoa malighafi kwa viwanda vya ndani. Changamoto sasa ni kuongeza ubunifu, uwekezaji na uzalishaji ili nishati inayopatikana itumike kikamilifu katika kuongeza thamani ya rasilimali hizo. Kwa vijana, wajasiriamali na wawekezaji, ujumbe ni mmoja tu kwao: Fursa hii isitazamwe kama takwimu ya Serikali, bali kama nafasi ya kufanya biashara na kuzalisha. Badala ya kusubiri ajira, mazingira haya yanatoa nafasi ya kuanzisha shughuli zinazoweza kutengeneza ajira kwa wengine. Ziada ya Megawati 2,000 pia ina maana kwamba Tanzania ina nafasi ya kujiandaa kwa mahitaji makubwa zaidi ya nishati yatakayotokana na ukuaji wa viwanda, miji na shughuli za kiuchumi. Hivyo, hatua inayofuata ni kuhakikisha uwezo huo unabadilishwa kuwa uzalishaji halisi na thamani kwa wananchi. Nguvu ya umeme inakuwa nguvu ya uchumi pale inapogeuzwa kuwa uzalishaji. Na uzalishaji unaanza pale wananchi wanapochukua hatua. Megawati 2,000 za ziada ni mwaliko kwa Watanzania kuchangamkia fursa, kuanzisha viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza biashara na kujenga ajira. Tanzania ina umeme wa kuzalisha zaidi; sasa ni wakati wa wananchi kuzalisha zaidi.

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya utalii duniani baada ya kujinyakulia jumla ya tuzo 54 katika World Travel Awards 2026, huku ikiibuka kinara wa vivutio vya utalii barani Afrika kwa mara ya nne. Mafanikio hayo ni uthibitisho wa nafasi inayozidi kuimarika ya Tanzania katika ramani ya utalii duniani na matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali, sekta binafsi, jamii na wadau mbalimbali. World Travel Awards ni miongoni mwa majukwaa yanayotambulika kimataifa kwa kutambua ubora na ushindani katika sekta ya safari na utalii. Ushindi wa Tanzania katika tuzo hizo za mwaka 2026 umeongeza heshima ya nchi katika soko la utalii la Afrika na dunia, huku ukiendelea kujenga chapa ya Tanzania kama miongoni mwa maeneo bora ya utalii duniani. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Agosti 28, 2026, Bwejuu, Zanzibar, iliifanya Tanzania kung’ara katika medani ya kimataifa baada ya kushinda tuzo katika maeneo mbalimbali yanayobeba sura na hadhi ya utalii wa nchi. Miongoni mwa tuzo kubwa zilizotwaa na Tanzania ni Eneo Bora la Utalii Afrika 2026, ushindi unaoendelea kuthibitisha uwezo wa nchi katika kutoa uzoefu wa kipekee wa utalii. Zanzibar nayo imeendelea kung’ara kwa kushinda tuzo ya Eneo Bora la Fukwe Afrika 2026, huku Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ikitwaa tuzo ya Bodi Bora ya Utalii Afrika 2026. Ushindi huo hauishii katika fukwe na mandhari ya kuvutia. Tanzania imeendelea kuthibitisha kuwa utajiri wake wa utalii unagusa maeneo mbalimbali, hususan uhifadhi wa wanyamapori na mazingira. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuonesha upekee wake baada ya kushinda tuzo mbili muhimu za Hifadhi Bora Afrika 2026 na Hifadhi Bora ya Big Five Afrika 2026. Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha hadhi ya Serengeti kama moja ya maeneo maarufu ya utalii barani Afrika na duniani. Kwa upande mwingine, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imetwaa tuzo ya Hifadhi Bora ya Utalii wa Kiutamaduni Afrika 2026, huku Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikishinda tuzo ya Hifadhi Bora ya Mandhari Afrika 2026. Hifadhi ya Taifa ya Tarangire nayo imeibuka mshindi wa tuzo ya Hifadhi Bora ya Paradiso ya Tembo Afrika 2026. Mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Tanzania si nchi ya hifadhi na wanyamapori pekee, bali ina hazina pana ya vivutio vinavyoweza kuwavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katika sekta ya usafiri wa anga, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umeibuka mshindi wa tuzo ya Uwanja Bora wa Ndege Afrika 2026, hatua inayoongeza ushindani na hadhi ya Tanzania katika kurahisisha safari na kuwapa wageni huduma bora wanapoingia na kutoka nchini. Mafanikio haya si ya taasisi moja wala kundi moja. Ni matokeo ya ushirikiano wa Serikali, taasisi za utalii na uhifadhi, sekta binafsi, jamii zinazozunguka maeneo ya utalii na wadau wengine wanaoshiriki katika kulinda rasilimali, kuboresha huduma na kujenga uzoefu bora kwa wageni wanaotembelea Tanzania. Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amempongeza na kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wenye dira na dhamira ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuweka utalii miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi. Mafanikio haya yanatambua mchango wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Ngorongoro, pamoja na taasisi nyingine za uhifadhi na utalii zinazoendelea kulinda, kuendeleza na kutangaza rasilimali za kipekee za utalii za Tanzania. Kwa hakika, nyuma ya kila tuzo kuna kazi ya Watanzania wengi. Wapo waendesha safari za kitalii, kampuni za safari, hoteli na kambi, mashirika ya ndege, waongoza watalii, askari wa wanyamapori, wahifadhi, wawekezaji, vyama vya utalii, jamii zinazozunguka maeneo ya utalii, vyombo vya habari na maelfu ya Watanzania wanaoshiriki kila siku kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata uzoefu wa kipekee. Akizungumzia mafanikio hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Masuala ya Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema Tanzania inajivunia hatua kubwa iliyofikiwa katika sekta hiyo, ikiwemo kujinyakulia tuzo 54 na kutajwa kuwa kinara wa vivutio vya utalii barani Afrika kwa mara ya nne. Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya dira na juhudi endelevu za Serikali pamoja na ushirikiano mkubwa wa wadau katika kulinda, kuendeleza na kuitangaza rasilimali na vivutio vya Tanzania. Kwa mtazamo mpana, ushindi huo ni zaidi ya medali na tuzo. Ni fursa ya kuitangaza Tanzania, kuongeza idadi ya watalii, kukuza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa Watanzania. Ni pia ujumbe kwa dunia kwamba Tanzania ina kila sababu ya kuwa miongoni mwa chaguo la kwanza kwa mtu anayetamani kuona wanyamapori wa aina yake, fukwe za kuvutia, mandhari ya kipekee, utamaduni na ukarimu wa watu wake. Hatua iliyofikiwa inapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi za kutunza rasilimali za nchi, kuboresha huduma, kuimarisha miundombinu na kuendelea kuitangaza Tanzania kwa nguvu zaidi katika masoko ya ndani, Afrika na kimataifa. Kwa Watanzania, tuzo hizi ni fahari ya Taifa na ushahidi kwamba tukilinda tulichonacho, tukiboresha huduma na kushirikiana, Tanzania inaweza si tu kushindana, bali pia kushinda katika soko la utalii duniani. Ushindi huu ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu—ya kuhakikisha jina la Tanzania linaendelea kung’ara, fursa za utalii zinaongezeka na matunda ya sekta hiyo yanazidi kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani wa kugharamia, kusimamia na kuzalisha mahitaji muhimu ya huduma za afya, badala ya kuendelea kutegemea misaada na mifumo kutoka nje. Dkt. Mwigulu ameyasema hayo, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, ukishirikisha zaidi ya washiriki 2,700 kutoka mataifa 27. Amesema wakati umefika kwa Afrika kubadili namna inavyoelewa na kutekeleza dhana ya kujenga uwezo, akisisitiza kuwa dhana hiyo haipaswi kuishia katika miradi midogo isiyojenga uwezo wa kudumu, bali ielekezwe katika uwekezaji wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia na wataalamu. Enzi zile nikiwa Waziri wa Fedha nilikuwa nawaambia nchi za Afrika zimeshashuhudia muda mrefu sasa wa maisha ya misaada na misaada inayoelekezwa pengine katika maeneo ambayo yanatofautiana na malengo ya ndani ya nchi kwa jina la capacity building. Capacity building. Capacity building. Na ndio tunaishia chapati, mandazi, sambusa. Hatuwekezi kitu kitakachodumu na kikawa endelevu. Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, malengo ya ndani ya nchi yanayokwenda sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuheshimiwa na washirika wa maendeleo, ili misaada na uwekezaji katika sekta ya afya viweze kuacha matokeo ya kudumu kwa wananchi wa Afrika. Amesema Tanzania inaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza miundombinu, rasilimali watu pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambayo Serikali imeanza kuitekeleza mwaka 2026. Tunapozungumza kuhusu afya ya msingi, tusizungumzie tu kujenga vituo vya afya. Tujenge pia uwezo wa nchi zetu kugharamia huduma hizo, kuzalisha mahitaji yake na kutumia teknolojia zetu wenyewe. Ameongeza kuwa Tanzania imeanza kuwekeza katika uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa kwa lengo la kupunguza utegemezi wa misaada na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuwa wa uhakika, hususan wakati dunia inapokumbwa na changamoto zinazoathiri minyororo ya usambazaji. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza ajira katika sekta hiyo, hatua ambazo zitasaidia kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Dkt. Mwigulu amesema mkutano huo unapaswa kuzaa hatua mahsusi zinazoweza kutekelezwa na kupimwa, badala ya kuishia katika mijadala na maazimio yasiyotekelezwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, amesema Afrika ya mwaka 2026 si Afrika ya mwaka 1960 na kwamba wakati umefika kwa washirika wa maendeleo kubadili namna wanavyoshirikiana na Serikali za Afrika. Dkt. Kaseya amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuwa na umiliki na uelewa wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya afya, huku fedha za washirika wa maendeleo zikiendana na mipango na vipaumbele vya kitaifa. Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohammed Janabi, amesema changamoto kubwa kwa Afrika si kukosa suluhisho katika sekta ya afya, bali ni kukosa ujasiri wa kuyafadhili, nidhamu ya kuyatekeleza na uwajibikaji wa kuyadumisha. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuwa ndiyo ngazi inayohudumia wananchi wengi zaidi nchini. Amesema asilimia 95.6 ya wajawazito wanaojifungua nchini wanapata huduma katika ngazi ya afya ya msingi, huku asilimia 86 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma yakihudumiwa katika ngazi hiyo. Profesa Shemdoe amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya afya ya msingi, hivyo kuongeza uwekezaji katika ngazi hiyo ni kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kwa wananchi wengi nchini. Mkutano huo wa siku tatu unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kupitia ufadhili endelevu, ufanisi, ubora wa huduma, ubunifu, ushirikiano wa kikanda na kujenga mifumo ya afya inayostahimili majanga. Kwa ujumla, mkutano huo unalenga kuhimiza Afrika kujenga mifumo ya afya inayojitegemea, yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, huku ikiweka mkazo katika uwekezaji wa muda mrefu, uzalishaji wa ndani, rasilimali watu na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.

Na Baraka Messa – Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali na Taasisi za Umma kuongeza ubunifu na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuangazia zaidi uwekezaji unaofanywa na Serikali na matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi. Msigwa ametoa wito huo Septemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwakaribisha na kuwapa maelekezo Maafisa Habari wapya walioajiriwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba. Amesema wajibu wa Maafisa Habari ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kwa wakati hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, maji, nishati, usafiri, teknolojia na sekta nyingine zinazogusa maisha yao. Kazi yetu ni kuhabarisha wananchi. Tueleze Serikali imefanya nini, inafanya nini na inatarajia kufanya nini, kwa sababu hayo ndiyo mambo yanayowagusa wananchi. Amesema katika kutekeleza wajibu huo, Maafisa Habari wanapaswa kuwasilisha taarifa zinazoonesha kwa uwazi uwekezaji uliofanyika, miradi inayotekelezwa, thamani ya uwekezaji huo, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, ili wananchi waweze kutambua namna rasilimali za Serikali zinavyotumika katika kuleta maendeleo. Msigwa amesema taarifa za utekelezaji wa Serikali zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza tukio, badala yake zioneshe maana ya mradi kwa mwananchi, ikiwemo huduma zitakazopatikana, fursa zitakazozalishwa, ajira zitakazoongezeka na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Amesema Maafisa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mipango na vipaumbele vya Serikali, pamoja na kutambua hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili. Taarifa nzuri si ile inayosema tu mradi umejengwa, bali ieleze mradi huo umejengwa kwa gharama gani, unahudumia wananchi wangapi na umeleta mabadiliko gani katika maisha yao. Aidha, amewataka Maafisa Habari kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa na majukwaa ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, katika kufikisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto na inayoeleweka kwa makundi mbalimbali. Amesema matumizi ya teknolojia yanatoa fursa ya Serikali kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo Maafisa Habari wanapaswa kutumia ubunifu katika kuandaa maudhui yanayowapa wananchi uelewa wa shughuli, miradi na uwekezaji unaofanywa na Serikali. Vilevile, Msigwa amewataka Maafisa Habari hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji na maslahi mapana ya umma. Amesema Maafisa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinajenga uelewa kuhusu maendeleo yanayotekelezwa na Serikali na kuwasaidia wananchi kutambua fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo. Msigwa amesisitiza kuwa, kupitia taarifa sahihi, zenye ushahidi na zinazoonesha matokeo, Maafisa Habari wanaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa na mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.