Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Mradi wa Maji Miji 28 Chamwino, Mwarobaini wa Changamoto ya Maji Dodoma

July 31, 2026

Na Josephina Lupasha – MAELEZO

Kwa miaka mingi, wakazi wa Chamwino na maeneo jirani mkoani Dodoma wameishi na simulizi moja inayofanana; kuamka alfajiri kutafuta maji, kusubiri kwa saa nyingi kwenye foleni au kuishi kwa mgao wa maji usiotabirika. Leo, simulizi hiyo inaelekea kuwa historia kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji miji 28 Chamwino, unaotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika huduma ya maji.

Mradi huu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17 unatekelezwa katika Wilaya ya Chamwino na unatarajiwa kuhudumia wakazi wa kata za Chamwino, Msanga, Buigiri, Chinangali pamoja na maeneo ya karibu ikiwemo Mtumba na Ihumwa.

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kutekeleza miradi ya maji katika miji 28 Tanzania Bara, ukiwa na lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika.

Ujenzi wa mradi ulianza Aprili mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Agosti, 2026 ambapo hadi sasa, utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 74, huku baadhi ya maeneo tayari yakiwa yameanza kupata huduma ya maji.

Kwa wakazi wa Chamwino, mradi huu si tu ujenzi wa miundombinu, bali ni ukombozi wa maisha yao ya kila siku.

“Kiukweli, hapo nyuma maji hayakuwa yanatosha. Serikali imetukumbuka. Mradi mkubwa wa namna hii kwa sisi tuliopitia ugumu wa maji kwa muda mrefu ni jambo la kujivunia na la kushukuru sana,” anasema Bi. Maila Nyembela, mkazi wa Chamwino Ikulu.

Licha ya mradi kutokamilika, tayari umeanza kuonesha matokeo chanya. Huduma ya maji sasa inapatikana kwa wastani wa saa 22 kwa siku, hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa mgao wa maji uliokuwa ukiwasumbua wakazi kwa miaka mingi.

Kwa wanawake, ambao kwa muda mrefu walibeba jukumu kubwa la kutafuta maji, mradi huu umeleta matumaini mapya. “Awali tulilazimika kuamka alfajiri kutafuta maji au kununua kwa gharama kubwa. Ilikuwa tabu sana, hasa kwa wanawake. Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha maisha ya familia zetu na kutupa muda zaidi wa kushiriki shughuli za maendeleo,” anasema Bi. Mluka Michael, mkazi wa Chamwino.

Mratibu Msaidizi wa Mradi huu kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Titho Alex, anaeleza kuwa mradi huo umejumuisha ujenzi wa visima virefu nane, matenki mawili ya kuhifadhi maji pamoja na miundombinu ya kutibu, kusukuma na kusambaza maji.

Anasema tanki moja lililopo Chamwino Ikulu lina uwezo wa kuhifadhi maji lita 500,000 , huku lingine lililopo Msanga likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 200,000.

“Mkakati huu utawezesha mradi kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku, kiwango kitakachohakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa saa 22 hadi 24 kila siku na kuondoa kabisa changamoto ya mgao wa maji Chamwino pamoja na kuimarisha huduma katika maeneo ya jirani,” anasema Mhandisi Alex.

Kwa wananchi walioishi muda mrefu Chamwino, mradi huu ni ushahidi wa mabadiliko makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika Makao Makuu ya Nchi.

“Nimeishi Dodoma tangu mwaka 1971. Wakati huo hatukuwa na maji kabisa. Baadaye yakaanza kupatikana lakini hayakutosha. Sasa karibu kila kitongoji kina maji, ingawa baadhi ya maeneo bado hupata kwa mgao. Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu ukikamilika tutapata maji kila siku. Hili ni jambo la kufurahisha sana,” anasema Mchungaji Anderson Ndoloji wa Mtaa wa Muungano.

Meneja wa DUWASA Kanda ya Chamwino, Mhandisi Gray Mbalikila, anasema mradi huo utaongeza uwezo wa mamlaka hiyo kupanua huduma katika maeneo mapya yanayokua kwa kasi kutokana na ongezeko la wakazi, biashara na taasisi mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma.

“Tunajivunia hatua tuliyofikia. Mradi huu ukikamilika, Chamwino itakuwa na akiba ya kutosha ya maji hata kwa ajili ya kata za jirani. Huduma itaongezeka kutoka kiwango cha sasa cha takribani asilimia 91 hadi kufikia asilimia 100,” anasema.

Mbali na kuboresha upatikanaji wa maji, mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali. Upatikanaji wa maji ya uhakika utaimarisha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama, kuongeza usafi wa mazingira, kukuza biashara ndogo na shughuli za uzalishaji, pamoja na kuboresha huduma katika shule na vituo vya afya.

Kadri Dodoma inavyoendelea kukua kama Makao Makuu ya Serikali, mahitaji ya huduma za msingi yanaongezeka. Mradi wa Maji Miji 28 Chamwino ni moja ya miradi ya kimkakati inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama.

Kukamilika kwa mradi huu hakutakuwa tu mwisho wa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wananchi wa Chamwino na maeneo jirani, bali kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ambapo maji yatakuwa si tena changamoto, bali chachu ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *