Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Hospitali ya Benjamin Mkapa inavyopunguza Rufaa za Matibabu Nje ya Nchi

August 10, 2026

Na Baraka Messa – MAELEZO

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu cha huduma za matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi nchini Tanzania na Afrika Mashariki, kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 10 uliowezesha hospitali hiyo kutoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingi za ukanda huu.

Hayo yanaelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu mafanikio ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya.

Msigwa anasema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 kuimarisha Hospitali ya Benjamin Mkapa ili ifikie viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa.

“Hospitali ya Benjamin Mkapa leo inatoa huduma ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi si Tanzania pekee, bali hata katika Afrika Mashariki, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 283 katika kipindi cha miaka 10 kuifanya hospitali hii kuwa kituo cha kisasa cha matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi,” anasema Msigwa.

Anafafanua kuwa uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya kutolea huduma za kibingwa, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa, uboreshaji wa mifumo ya Tehama pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na kuboresha mazingira yao ya kazi.

Msigwa anasema mwaka 2015 hospitali hiyo ilikuwa na watumishi 20 pekee, lakini kufikia mwaka 2026 idadi hiyo imeongezeka na kufikia watumishi 1,076, wakiwemo madaktari bingwa 105.

Anasema hospitali hiyo sasa inatoa huduma 17 za kibingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, huduma za radiolojia ya kisasa pamoja na uchujaji wa damu (dialysis).

“Huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa seli mundu zinapatikana Hospitali ya Benjamin Mkapa na ni miongoni mwa huduma adimu ambazo hazipatikani katika hospitali nyingine nyingi nchini na Afrika Mashariki,” anaeleza .

Msigwa anasema kuimarika kwa huduma hizo kumepunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya Watanzania waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta matibabu, jambo ambalo limeokoa fedha nyingi za Serikali na wananchi.

HOSPITALI BENJAMINI YAWA KIVUTIO WAGONJWA KUTOKA MATAIFA YA NJE

Msigwa anasema hospitali hiyo sasa imekuwa kivutio cha wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Tumewahudumia wagonjwa 2,897 kutoka Burundi na wagonjwa 526 kutoka Comoro. Pia wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za Afrika Mashariki wanaendelea kuja kupata matibabu hapa, Tunawatibu ndugu zetu, lakini pia huu ni utalii wa matibabu unaoingizia taifa mapato,” anasema Msigwa.

Anasema kuwa mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuanza kushindana na mataifa yaliyopiga hatua katika utalii wa matibabu kama India, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakipokea wagonjwa wengi kutoka Tanzania.

“Kwa muda mrefu Watanzania walikuwa wakitumia fedha nyingi kwenda kutibiwa nje ya nchi, hususan India,..Sasa Serikali imewekeza kuhakikisha huduma hizo zinapatikana hapa nchini ili wananchi wapate matibabu bora na wakati huohuo Tanzania inufaike kupitia utalii wa matibabu,” anasema Msigwa.

Pia Msigwa amesema Julai 10, 2025 Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzisha International Clinic, kitengo maalumu kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na wa kimataifa.

Anasema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo, wagonjwa 18,607 wamehudumiwa, wakiwemo wagonjwa 390 kutoka mataifa mbalimbali, huku huduma ya Master Health Check-up ikiendelea kuvutia watu wanaohitaji uchunguzi wa afya kwa kiwango cha kimataifa.

Aidha anasema hospitali hiyo pia imeanzisha eneo maalumu la huduma binafsi kwa wagonjwa wanaohitaji faragha na huduma za kiwango cha juu bila kuchangamana na wagonjwa wengine.

Anasema Huduma hizi zinafanana na zile zinazotolewa katika hospitali za kisasa duniani kama za China, Ujerumani na India, huku dhamira ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ndani ya nchi na wakati huohuo Tanzania inakuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika.

Kuimarika kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali mbalimbali za rufaa nchini ni sehemu ya malengi ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani wa kimataifa katika utoaji wa huduma za matibabu.

No Next Post Available

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *