Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Katika bara linaloendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika afya ya uzazi, mama na mtoto, juhudi za kuweka maisha ya wanawake na watoto katika nafasi ya juu ya ajenda za maendeleo zimeendelea kupata msukumo mpya. Safari hiyo imepata nguvu jijini Arusha, ambako Wabunge kutoka Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Bara la Afrika kupitia Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU) wameunga mkono ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika. Uungwaji mkono huo umetolewa Oktoba 8, 2026, katika mkutano wa pembezoni mwa Mkutano wa 153 wa IPU, uliozikutanisha nchi mbalimbali za Afrika na wadau wa maendeleo ya afya duniani kujadili namna ya kuimarisha sera, mifumo ya utoaji huduma, uwekezaji na uwajibikaji katika sekta ya afya. Kwa Tanzania, mjadala huo unaenda sambamba na msisitizo wa Rais Samia wa kuhakikisha afya ya mama, mtoto na vijana inakuwa sehemu muhimu ya juhudi za kujenga jamii yenye afya na yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Ajenda inayovuka mipaka Kiongozi wa Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Wabunge wa Bara la Afrika kupitia IPU na Spika wa Jamhuri ya Chad, Mhe. Ali Kolotou Tchaïmi, amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuunganisha nguvu, kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuwa na agenda ya pamoja ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Kauli hiyo inaonyesha namna suala la afya ya mama na mtoto linavyotazamwa si kama jukumu la nchi moja pekee, bali changamoto ya bara inayohitaji mshikamano, uzoefu wa pamoja na hatua zinazotekelezwa kwa ushirikiano. Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Mhe. Angela Didiza, amesema Afrika inaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kuendeleza afya ya wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana.   Amesisitiza kuwa uongozi wa kisiasa una nafasi muhimu katika kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji wa hatua za kibunge zinazolenga kuboresha huduma za afya. Kauli hiyo ni ishara nyingine ya namna juhudi zinazofanywa Tanzania zinavyoweza kuwa sehemu ya maarifa na uzoefu ambao nchi nyingine za Afrika zinaweza kujifunza na kuuboresha kulingana na mazingira yao. Uwekezaji lazima uende sambamba na matokeo Katika mjadala huo, Spika wa Bunge la Botswana, Mhe. Dithapelo Keorapetse, amegusa eneo muhimu la uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za afya. Amesema uwekezaji pekee hautoshi, bali nchi zinapaswa kuhakikisha rasilimali zinazotengwa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayopimika kwa wananchi. “Uwekezaji pekee hautoshi, bado tunakabiliwa na changamoto katika matokeo ya afya, hali hii inaonesha umuhimu wa kuangalia ufanisi wa matumizi ya rasilimali,” amesema. Mtazamo huo unaifanya ajenda ya afya kuwa zaidi ya kuongeza bajeti, kwa kuhitaji pia mifumo imara ya ufuatiliaji, uwajibikaji na kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa inaleta mabadiliko katika maisha ya wananchi. IPU Yaahidi Kuwa Mshirika wa Vitendo Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema juhudi za Rais Samia katika kuimarisha afya ya uzazi zinapaswa kuungwa mkono. Amesisitiza kuwa utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa viongozi ni muhimu katika kuhakikisha wataalamu wa afya na mifumo ya afya inafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kwa mtazamo huo, dhamira ya kisiasa ndiyo inayoweza kubadilisha sera na ahadi kuwa hatua zinazoonekana katika jamii. “IPU inajidhatiti kuwa mshirika wa vitendo kwa mabunge katika kuhakikisha ahadi zinatafsiriwa kuwa hatua na matokeo chanya ya kuimarisha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto,” amesema Dkt. Tulia. Kauli hiyo inaweka wazi nafasi ya mabunge katika safari ya kufikia malengo ya afya, hususan katika kutunga sheria, kuidhinisha na kusimamia matumizi ya rasilimali pamoja na kuishinikiza Serikali kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Tanzania Yaendelea Kuweka Afya ya Mama na Mtoto Mbele Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania, huku Bunge likiwa na wajibu wa kusimamia rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya huduma hizo kwa niaba ya wananchi. Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Bunge katika kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika sekta ya afya unalenga maeneo yenye athari kubwa kwa maisha ya wananchi. Kwa Tanzania, ajenda hiyo imepewa mwelekeo mpana zaidi kupitia Mpango Kazi wa Rais Samia wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Barani Afrika 2026–2030. Sifuri Tatu: Dira ya Rais Samia kwa Afrika Mshauri wa Rais kuhusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema vifo vitokanavyo na uzazi barani Afrika vimepungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023. Hata hivyo, amesema Afrika bado inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani, hali inayodhihirisha ukubwa wa kazi iliyopo mbele. Ndiyo maana Mpango Kazi wa Rais Samia wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Barani Afrika 2026–2030 umejengwa katika azma ya kufikia Sifuri Tatu: sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, na sifuri ya watoto wasiochanjwa. Dira hii inaweka mkazo katika hatua zinazolenga kuhakikisha mwanamke anapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua, mtoto anapata huduma zinazohitajika tangu anapozaliwa, na kila mtoto anapata kinga kupitia chanjo. Kwa mantiki hiyo, ajenda ya Rais Samia haionekani tena kama jambo linalohusu Tanzania pekee, bali kama wito wa Afrika kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto ambayo bado inagusa maisha ya mamilioni ya wanawake na watoto. Uungwaji mkono uliotolewa na wabunge wa Afrika jijini Arusha ni ishara kwamba bara linaona umuhimu wa kuwa na sauti na hatua za pamoja katika eneo hili. Na wakati Afrika ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto zake za kiafya, msisitizo wa Rais Samia wa kuwekeza katika afya ya mama, mtoto na vijana unaendelea kupata nafasi katika mjadala mpana wa bara — mjadala unaolenga kuhakikisha maendeleo ya Afrika yanaanza na kulindwa kupitia afya na ustawi wa watu wake. Kwa sababu, Afrika yenye afya bora ya mama na mtoto ndiyo msingi wa Afrika yenye kizazi chenye nguvu, chenye tija na chenye uwezo wa kujenga maendeleo endelevu.

London, Oktoba 7, 2026 Kampuni ya ndege ya British Airways imetangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Uingereza na Tanzania kuanzia Mei 2027, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za utalii, biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Tangazo hilo limetolewa Oktoba 7, 2026 na Mkuu wa Masoko wa British Airways kwa Bara la Afrika, Asia na Pasifiki, Bw. Moran Birger, katika Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini London akieleza kuwa uamuzi huo umechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya watalii na wasafiri wanaoitembelea Tanzania, pamoja na maendeleo ya kiuchumi na ongezeko la uwekezaji nchini. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amepongeza uamuzi huo na kueleza kuwa kurejea kwa British Airways kutaendelea kuifungua Tanzania kwa dunia na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi na Taifa. Amesema Tanzania ina nafasi ya kuwa kitovu cha uwekezaji kwa masoko ya kikanda, hivyo wawekezaji wanapaswa kulitazama Taifa hilo kama jukwaa la kuwafikia wadau wa nchi mbalimbali. Dkt. Mwigulu amesema amani, utulivu na uongozi imara, pamoja na miundombinu ya barabara, SGR, bandari, viwanja vya ndege na upatikanaji wa umeme wa uhakika, ni miongoni mwa mambo yanayowezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini. Amesema mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yanahitaji pia umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa uchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imeandaa sera, mipango na malengo thabiti kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa, kwa lengo la kufungua fursa za uwekezaji na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha ukomavu wa kisiasa kupitia dhamira yake ya kuhimiza maridhiano ya kitaifa kwa kushirikisha vyama vya siasa. Prof. Kabudi amesema hayo Oktoba 6, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua uongozi mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa pamoja na nembo mpya ya Baraza hilo. Amesema Rais Samia amekuwa msikivu na mwenye utulivu katika kusikiliza maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, akilenga kuimarisha umoja, mshikamano na amani nchini. Rais Samia amekuwa na dhamira ya dhati ya kuanzisha 4R, ambazo zimeonekana kuwa na matokeo chanya katika kuleta nchi pamoja na kuondoa tofauti zetu. Amekuwa na utulivu wa kumsikiliza kila mtu ambaye amewahi kukutana naye,” Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Baraza hilo kunapaswa kuwa chachu kwa viongozi wake kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Aidha, Prof. Kabudi amewataka viongozi wapya wa Baraza hilo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni za Baraza, ikiwemo kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake na wadau wengine katika mijadala na shughuli zake. Amesema Baraza hilo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto mbalimbali za kisiasa, ikiwemo zile zinazoonekana kuwa ngumu kutatuliwa, huku akiwataka viongozi kulitumia jukwaa hilo kujenga maelewano na mshikamano wa kitaifa. Prof. Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa kutumia misingi ya 4R kama dira ya kuimarisha ushirikiano na kupiga hatua katika masuala mbalimbali ya kisiasa nchini. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Juma Ally Khatib, amesema Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kwa lengo la kuchochea maendeleo na kujenga mazingira chanya ya kisiasa nchini. Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Eveline Munishi, amesema uwepo wa Baraza hilo utasaidia kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini. Mkutano huo umeandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi. Baraza hilo la Vyama vya Siasa lilichaguliwa Septemba 3, 2026, na linatarajiwa kudumu madarakani hadi Septemba 3, 2028. Kwa sasa, Baraza hilo linaongozwa na Mheshimiwa Juma Ally Khatib ambaye ni Mwenyekiti, huku Mheshimiwa Aggrey Mwanri akiwa Makamu Mwenyekiti.

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kupanua usambazaji wa umeme, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi. Akizungumza Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini mkataba na uzinduzi wa mpango wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, , amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa uhakika na kwa urahisi zaidi. Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme ni kukamilika na kuanza kuzalisha kwa Bwawa la Julius Nyerere, lililopo katika Mto Rufiji, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema ongezeko la uzalishaji linaenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji ili umeme uwafikie walaji wa mwisho. Mhe. Ndejembi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme nchini, ikiwemo jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya Shilingi bilioni 231 zimetengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kuimarisha huduma hiyo. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vikubwa vya kusambaza umeme, ikiwemo Dege na Mabibo, pamoja na ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi, Kimara, Ilala, Ubungo na Ununio, hatua inayolenga kuongeza uwezo na uhakika wa huduma ya umeme jijini Dar es Salaam. Akizungumza kuhusu mwelekeo wa muda mrefu, Makamu wa Rais amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta ya nishati nafasi muhimu katika kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia tija, ushindani, ubunifu na matumizi ya teknolojia. Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na megawati 74,000 ifikapo mwaka 2050. Aidha, amesema Tanzania inaendelea kushiriki katika juhudi za kimataifa za kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika kupitia ‘Mission 300’, unaolenga kuwaunganisha takribani watu milioni 300 barani Afrika na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia iliandaa Mkutano wa Africa Energy Summit – Mission 300 jijini Dar es Salaam mwaka 2025. Mhe. Ndejembi ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zake na sekta binafsi katika kuharakisha uwekezaji wa nishati. Amesema umeme unaofikishwa kwa wananchi unapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, uzalishaji, biashara, teknolojia na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo jitihada za kuongeza uzalishaji zinapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa ufanisi.

Bilioni 2 za Mirabaha Kuwanufaisha Wasanii Nchini Na Josephina Lupasha – MAELEZO Takribani shilingi bilioni mbili zilizokusanywa kutokana na matumizi ya kazi za wasanii kupitia mfumo wa mirabaha zinatarajiwa kugawiwa kwa wasanii nchini, hatua inayolenga kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao na kuongeza mchango wa sekta ya sanaa katika ajira, kipato na uchumi wa Taifa. Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, usimamizi na ugawaji wa mirabaha kwa uwazi na ufanisi, ili wasanii wanufaike ipasavyo na kazi zao. Sheria imeweka utaratibu kupitia COSOTA wa kulinda haki miliki na namna ya kugawa mirabaha. Zipo fedha takribani shilingi bilioni mbili ambazo zinapaswa kutolewa kama gawio kwa wasanii wetu. Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta ya sanaa na kuifanya kuwa chanzo endelevu cha ajira, kipato na fursa za kiuchumi kwa wasanii, huku ikichangia katika maendeleo ya Taifa. Katika hatua nyingine, Waziri Makonda amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), huku ikilenga kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa fursa ya kiuchumi kwa Watanzania katika sekta mbalimbali. Amesema maandalizi hayo yanahusisha miundombinu na huduma muhimu, zikiwemo usafiri, malazi, utangazaji, ujenzi wa chapa, huduma za lugha, upigaji picha, uzalishaji wa maudhui ya televisheni, huduma za matibabu na huduma za kiufundi. Amesema fursa zitakazotokana na AFCON 2027 zinapaswa kutumiwa ipasavyo na Watanzania kwa kujiandaa na kushiriki katika huduma mbalimbali zitakazohitajika kabla na wakati wa mashindano hayo. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali2 katika maandalizi ya matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa yanayotarajiwa kufanyika nchini katika kipindi cha mwaka 2026/2027, kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi, ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89.02, huku ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.37 na kazi mbalimbali za ukamilishaji zikiendelea kwa kasi. Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo Septemba 24, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27. Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, jengo la kituo kikuu cha umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa (MTO) asilimia 87. Mhandisi Besta amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na kukamilisha majengo, kufunga mifumo ya mitambo ya uendeshaji wa uwanja, umeme na mabomba, mifumo ya mawasiliano na ukaguzi wa mizigo, pamoja na kufunga madaraja ya kupita abiria, mifumo ya hali ya hewa na magari ya zimamoto. Mradi huo pia umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania. Mhandisi Besta amesema hadi sasa jumla ya ajira 9,059 zimezalishwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi. Amefafanua kuwa kati ya ajira hizo, 3,571 zimehusisha ujenzi wa miundombinu na 5,488 ujenzi wa majengo, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47. Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, ujenzi wa miundombinu ya mradi unatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, wakati ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026. Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo, na kuimarisha nafasi ya Dodoma katika shughuli za kitaifa na kimataifa.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Tanzania imeweka wazi azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, ikiwa na dhamira ya kupeleka katika chombo hicho sauti ya Afrika na kusukuma mbele ajenda ya amani, maendeleo na mageuzi ya mfumo wa kimataifa. Azma hiyo imetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika jijini New York, Marekani. Mhe. Ndejembi amesema endapo Tanzania itachaguliwa, itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani. Dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi wa nafasi hiyo ukitarajiwa kufanyika Juni 2028. Kwa Tanzania, safari ya kuwania nafasi hiyo inakwenda sambamba na hoja pana ya kutaka mfumo wa kimataifa uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi na kutoa nafasi kubwa kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika maamuzi yanayogusa mustakabali wa dunia. Katika hotuba yake, Mhe. Ndejembi amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi, hususan wakati dunia ikikabiliwa na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi moja. Migogoro na vita, mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya akili mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati ni miongoni mwa masuala ambayo Tanzania imesema yanahitaji ushirikiano wa kimataifa na taasisi zenye uwezo wa kuitikia mahitaji ya dunia ya sasa. Katika kueleza msingi wa msimamo wake, Tanzania imeonyesha pia uzoefu wake katika kushughulikia changamoto za maendeleo na ustawi wa jamii. Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imepiga hatua katika kuboresha afya ya mama na mtoto, ambapo kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kiliongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Tanzania pia imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba, hatua ambayo imehusishwa na uwekezaji katika huduma za afya na kuweka ustawi wa wananchi kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo. Uzoefu huo umeendelea kupewa nafasi katika ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekubali jukumu la kuwa kinara wa masuala hayo kwa niaba ya Umoja wa Afrika. Chini ya ajenda ya “Sifuri Tatu” (Three Zeros), Tanzania inalenga kufikia kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Mhe. Ndejembi amesema kufikia malengo hayo kunawezekana, lakini kunahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali za kutosha na ushirikiano imara wa kimataifa. Pamoja na afya, Tanzania imeunganisha azma yake ya kidiplomasia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana. Hata hivyo, Tanzania imesema utekelezaji wa malengo ya maendeleo katika nchi zinazoendelea unaendelea kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha, gharama za mikopo na mazingira ya mfumo wa fedha wa kimataifa huku ikitoa wito wa kuongezwa kwa mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasishwa kwa uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi, pamoja na nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya kifedha duniani. Mabadiliko ya tabianchi nayo yamepewa nafasi katika ujumbe wa Tanzania, huku nchi ikieleza wasiwasi kuhusu pengo lililopo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake. Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika kueleza hatua zake za mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi. Tanzania pia imeeleza uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034. Katika masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa, Tanzania imeeleza msimamo wake dhidi ya matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mengine. Kwa mujibu wa Tanzania, hatua hizo zinaweza kuathiri maendeleo, mamlaka ya nchi na uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao. Nchi hiyo imetaja mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti. Kuhusu migogoro inayoendelea ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kulindwa kwa raia, misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na diplomasia kurejeshwa kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu. Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha masuala ya amani na usalama na ajenda ya maendeleo ya nchi zinazoendelea. Azma ya kuwania nafasi katika Baraza la Usalama imekuja ikiwa imejengwa juu ya hoja za kuimarisha diplomasia ya kuzuia migogoro, kutafuta suluhu za amani, kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika amani na usalama, pamoja na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa. Kwa Tanzania, mjadala wa nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa hauishii kwenye uwakilishi pekee. Unaenda sambamba na masuala ya maendeleo, fedha, tabianchi, afya, nishati na amani ambayo yanaathiri moja kwa moja maisha ya watu.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Sekta ya Kilimo kwa miaka mingi imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania na inayotoa uhakika wa usalama wa chakula, kutoa ajira kwa mamilioni ya wananchi na kuchechemua biashara, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji. Hivyo, kumuwezesha mkulima kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha kipato si jukumu la sekta moja pekee, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika uchumi na mustakabali wa Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, uwekezaji katika sekta ya kilimo umeongezeka. Mathalani Bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi trilioni 1.19 mwaka 2025/2026. Ongezeko hilo linaonesha uzito wa sekta ya kilimo katika ajenda ya maendeleo na juhudi za kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kuongeza uzalishaji. Miongoni mwa hatua zinazomgusa mkulima moja kwa moja ni mfumo wa ruzuku za pembejeo, hususan mbolea na mbegu bora. Lengo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija shambani. Taarifa zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 360,000 kabla ya mfumo wa ruzuku hadi tani 840,000 katika msimu uliofuata, huku lengo likiwa kufikisha matumizi hadi tani milioni moja. Lakini kuongeza uzalishaji kunahitaji pia uhakika wa maji. Kutegemea mvua pekee kunaendelea kuwa changamoto katika uzalishaji wa kilimo, hivyo uwekezaji katika umwagiliaji ni hatua muhimu ya kumuwezesha mkulima kuzalisha kwa uhakika zaidi. Kufikia mwaka 2024/2025, Serikali ilikuwa ikitekeleza miradi 780 ya umwagiliaji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 543,000, huku kukamilika kwa miradi hiyo kukitarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji hadi zaidi ya hekta milioni 1.27. Pamoja na miundombinu hiyo, ushiriki wa wakulima katika usimamizi wa umwagiliaji nao umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imepanda kutoka 19 mwaka 2020/2021 hadi 912 mwaka 2024/2025. Hii inaashiria nafasi inayoongezeka ya wakulima katika kusimamia rasilimali muhimu kwa uzalishaji wao. Kilimo pia kinafungua ukurasa mpya kwa vijana. Kupitia programu kama Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), vijana wanahamasishwa kukiona kilimo kama biashara na fursa ya uwekezaji. Mtazamo huu ni muhimu kwa kizazi kinachoweza kutumia teknolojia, ubunifu na maarifa ya kisasa kubadilisha kilimo kutoka shughuli ya kutegemea nguvu kazi pekee na kuwa biashara yenye tija. Hata hivyo, kumuwezesha mkulima hakumaanishi kumuwezesha kuzalisha pekee. Mkulima anahitaji kuwezeshwa kuzalisha, kuhifadhi, kusindika na kuuza kwa thamani inayostahili. Bila soko la uhakika na uwezo wa kuongeza thamani, ongezeko la uzalishaji linaweza lisitafsiriwe moja kwa moja kuwa ongezeko la kipato. Hapa ndipo nafasi ya viwanda inakuwa muhimu. Mazao yanayotoka mashambani yanapaswa kuwa malighafi ya viwanda vya ndani. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, nafaka zikachakatwa kuwa bidhaa mbalimbali, maziwa yakaongezwa thamani na mazao mengine yakahifadhiwa na kusindikwa. Kwa kufanya hivyo, thamani inayotokana na kilimo hubaki zaidi ndani ya nchi, huku ikifungua nafasi za ajira na biashara. Kwa mtazamo huo, Agenda 10/30 inaleta umuhimu wa kuongeza tija, thamani ya mazao, mauzo ya nje, ushiriki wa vijana na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda. Kilimo kinapounganishwa na viwanda na masoko, mkulima haonekani tena kama mzalishaji wa malighafi pekee, bali anakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani unaozalisha utajiri. Hata hivyo, kipimo cha mwisho cha mafanikio ya uwezeshaji kinapaswa kuwa maisha ya mkulima. Bajeti inaweza kuongezeka na miradi inaweza kujengwa, lakini mafanikio halisi yataonekana pale mkulima atakapoweza kuzalisha kwa gharama nafuu, kupata mavuno bora, kuhifadhi mazao, kupata soko na kulipwa kwa thamani inayolingana na jasho lake. Tanzania ina ardhi, maji, nguvu kazi, masoko na malighafi nyingi zinazoweza kuifanya kilimo kuwa injini kubwa zaidi ya uchumi. Kinachohitajika ni kuendelea kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kutumia fursa hizo kikamilifu na kuwahamasisha vijana, wafanyabiashara na wawekezaji kuingia katika kilimo kwa mtazamo wa biashara. Tanzania yenye mkulima mwenye uwezo wa kiuchumi ni Tanzania yenye msingi imara wa chakula, viwanda, ajira na uchumi shirikishi. Kumuwezesha mkulima si kumsaidia mkulima pekee ni kuijenga Tanzania yenye uwezo wa pato la Taifa lenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola za Marekani 7000 kwa mwaka.

Sekta ya Madini inapozidi kuwa muhimu katika uchumi wa dunia, ushindani wa kimataifa haupimwi tena kwa wingi wa rasilimali pekee, bali pia kwa namna zinavyosimamiwa, uwekezaji unaovutwa na manufaa yake kwa wananchi. Mabadiliko haya yanaifanya Sekta ya Madini ya Tanzania kuzidi kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa, kupitia maboresho ya sekta, ukuaji wa uwekezaji na ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Kwa mujibu wa Tathmini ya Taasisi ya Fraser ya Canada ya mwaka 2025, Tanzania imeendelea kuimarika katika Sekta ya Madini kwa kushika nafasi ya nne barani Afrika na ya 34 duniani katika Kiashiria cha Kuvutia Uwekezaji (Investment Attractiveness Index). Aidha, Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 15 duniani katika kipengele cha upatikanaji wa rasilimali madini, ikiwa na alama 75, jambo linalothibitisha utajiri mkubwa wa rasilimali za madini zilizopo nchini. Hata hivyo, nafasi hizi hazielezi tu uwepo wa madini mengi nchini. Zinadhihirisha pia kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji, usimamizi wa sekta, uwazi wa sera na ongezeko la imani ya wawekezaji kwa Tanzania. Kwa maneno mengine, Tanzania haitajwi katika tathmini hizi kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kwa jinsi inavyoendelea kujenga mazingira yanayowezesha rasilimali hizo kuchangia maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi. Mwelekeo huo unaonekana pia katika upande wa uwekezaji. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025, Sekta ya Madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia Uwekezaji wa Mtaji wa Nje, ambapo mtaji uliongezeka kutoka dola bilioni 8.64 mwaka 2022 hadi dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024. Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anasema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na mageuzi yanayoendelea chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa sekta ya madini. Ongezeko hili ni matunda ya uhamasishaji wa uwekezaji, mazingira wezeshi kwa wawekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo, uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta na uunganishaji wa mitaji. Katika miaka ya hivi karibuni, Sekta ya Madini Tanzania imeendelea kuvutia kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi ambazo zimeingia katika ushirikiano na Serikali katika maeneo ya utafutaji, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini. Mwelekeo huu unaonesha kuwa ukuaji wa sekta si wa bahati mbaya, bali ni matokeo ya sera zilizo wazi, mifumo iliyoboreshwa na imani inayoongezeka kwa mazingira ya uwekezaji nchini. Mbali na kuvutia uwekezaji, Tanzania pia imekuwa ni sehemu ya rejea katika mijadala ya maendeleo ya sekta ya madini barani Afrika. Nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Uganda, Kenya, Burkina Faso, Sudani ya Kusini, Malawi, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari zimefika nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maeneo ya usimamizi wa sekta, ushirikishwaji wa wananchi, uendeshaji wa masoko ya madini na namna ya kuongeza mchango wa Sekta katika uchumi wa taifa. Hali hiyo inaonesha kuwa Tanzania si mnufaika wa mageuzi ya sekta ya madini pekee, bali pia imeanza kuwa chanzo cha uzoefu na maarifa kwa nchi nyingine zinazotafuta namna bora ya kuendeleza rasilimali zao za madini kwa manufaa ya wananchi. Kupitia hotuba yake ya bajeti aliyoisoma bungeni, Waziri Mavunde anaeleza kuwa, mwelekeo wa siku zijazo utaendelea kujikita katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji, kuongeza shughuli za uongezaji thamani wa madini pamoja na kuhakikisha sekta inachangia zaidi katika ajira, mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi wa taifa. Fauka ya hayo, Tanzania inaendelea kutajwa katika tathmini mbalimbali za kimataifa si kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kutokana na mchanganyiko wa rasilimali, sera zinazoendelea kuimarishwa, ongezeko la uwekezaji, ushiriki wa wananchi na usimamizi unaojenga imani kwa wadau wa sekta. Huu ndio msingi unaoifanya Tanzania kuendelea kujijengea nafasi muhimu zaidi katika ramani ya madini duniani na kuifanya sekta ya madini kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa nchi.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Mwaka 2027, macho ya Afrika na dunia yataelekezwa Afrika Mashariki wakati Tanzania, Kenya na Uganda zitakapokuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Kwa Tanzania, tukio hili ni zaidi ya dakika 90 za mchezo uwanjani; ni jukwaa kubwa la biashara, utalii, uwekezaji na kuitangaza nchi kwa mamilioni ya watu duniani. Kuanzia Dar es Salaam, Arusha hadi Zanzibar, ujio wa mashabiki, watalii na wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani ni wazi kwamba utaongeza mahitaji ya malazi, usafiri, chakula, burudani, bidhaa na huduma nyingine, na hapo ndipo fursa kwa Watanzania zinapojitokeza, na ukubwa wa manufaa ya fursa hizo utategemea namna wafanyabiashara na watoa huduma watakavyojiandaa mapema. AFCON 2027 inatoa nafasi ya Tanzania kutumia tukio la michezo kutengeneza shughuli za kiuchumi zinazoweza kuendelea hata baada ya mashindano kumalizika. Hoteli zinaweza kupanua huduma, sekta ya utalii inaweza kuongeza bidhaa na vifurushi vipya, huku wafanyabiashara wadogo na wakubwa wakitengeneza bidhaa na huduma zinazolenga mahitaji ya wageni. Kupitia Podcast ya Idara ya Habari-MAELEZO, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuanza maandalizi mapema ili fursa zitakazotokana na AFCON 2027 ziwafikie wazawa na kuchochea shughuli za kiuchumi. Msigwa anaeleza kuwa uzoefu wa nchi nyingine zilizowahi kuwa wenyeji wa AFCON unaonyesha ukubwa wa fursa zinazoweza kujitokeza. Anatoa mfano wa Morocco, iliyokuwa mwenyeji wa AFCON iliyofanyika Desemba 2025 hadi Januari 2026, ambapo zaidi ya wageni milioni 1.6 walifika nchini kutoka maeneo mbalimbali. Takwimu hiyo inaonyesha kwa nini maandalizi hayawezi kusubiri hadi mashabiki waanze kuwasili. Fursa inaanza kabla ya mpira kuanza. Mfanyabiashara anayejipanga leo ana nafasi ya kuwa tayari wakati mahitaji yatakapoongezeka. Kwa wafanyabiashara wa hoteli, utalii, usafiri na chakula, AFCON 2027 inaweza kuwa soko jipya lenye mahitaji makubwa. Msigwa anawataka watoa huduma kutumia muda uliopo kuboresha huduma zao na kujiandaa kukidhi mahitaji ya wageni. Kama wewe unafanya biashara ya utalii, jiandae kuwasafirisha wageni kuwapeleka maeneo mbalimbali. Kama wewe ni mfanyabiashara wa hoteli, jiandae kushawishi wageni wafikie kwenye hoteli yako, na kama wewe ni mfanyabiashara wa chakula, jiandae kuandaa chakula kizuri ili wageni wakija wajisikie kuweka kambi na kuja kula kwako. Ujumbe wa Msigwa unaweka jukumu kubwa kwa sekta binafsi: kutazama AFCON si kama tukio la kutazama mpira wa miguu pekee, bali kama soko la kutengenezwa na kutumiwa katika kukuza uchumi w mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Mbali na biashara za moja kwa moja wakati wa mashindano, AFCON 2027 inaweza kuwa kichocheo cha uwekezaji katika maeneo yenye mahitaji ya muda mrefu. Makazi, hoteli, usafirishaji, kilimo, teknolojia na huduma mbalimbali ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuhitaji uwekezaji zaidi. Msigwa anawataka Watanzania na sekta binafsi kuanza kuwasiliana na wadau ndani na nje ya nchi ili kuvutia uwekezaji na kutumia tukio hilo kama mlango wa kuonyesha fursa zilizopo Tanzania. Rais ametuletea tukio kubwa, sisi tulitumie kufanya uwekezaji mkubwa, mfano kwenye makazi. Kwenye kilimo tukaribishe wadau wazuri wenye teknolojia na mitambo ya kisasa kuja kuwekeza. Hii ina maana kwamba faida ya AFCON haipaswi kuishia katika mapato yatakayopatikana wakati wa mashindano. Tanzania inaweza kutumia wageni watakaofika kama daraja la kufungua masoko mapya, mitandao ya biashara na uwekezaji wa muda mrefu. AFCON 2027 pia ni fursa ya Tanzania kujitangaza kupitia michezo. Wageni watakapofika nchini watapata nafasi ya kuona zaidi ya viwanja vya soka. Wataona utamaduni, vivutio vya utalii, bidhaa na mazingira ya biashara na uwekezaji. Kwa mtazamo huo, mashindano yanaweza kuwa jukwaa la kuitambulisha Tanzania kama eneo la utalii, biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika. Wakati fursa hizo zikitarajiwa, maandalizi ya miundombinu ya michezo yanaendelea. Kwa mujibu wa Msigwa, viwanja vitakavyotumika katika mashindano pamoja na viwanja vya mazoezi vimekamilika kwa kiwango kikubwa. Tanzania pia inaendelea na maandalizi ya kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika mashindano hayo na kuunga mkono Taifa Stars, huku mikakati ya hamasa ikitarajiwa kulenga Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha. Hatimaye, thamani ya AFCON 2027 kwa Tanzania haitapimwa kwa idadi ya mechi zitakazochezwa pekee, bali pia kwa fursa zitakazobaki baada ya mashindano.Tukio hilo linaweza kuwa kichocheo cha biashara mpya, uwekezaji, ajira, utalii na masoko mapya ikiwa maandalizi yatafanyika kwa wakati. Kwa Watanzania, ujumbe ni mmoja: AFCON 2027 isiwe mashindano ya kutazama mpira tu uwanjani au kupitia Televisheni; iwe fursa ya kufanya biashara, kuwekeza, kuzalisha na kujenga. Mpira utakapigwa uwanjani, fursa zitakuwa mitaani, kwenye hoteli, mashamba, viwanda, usafiri na biashara mbalimbali.