Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Kituo Cha Habari

Na Mwandishi Wetu Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, amewaomba Watanzania kuendelea kulinda na kuitunza amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa wapo baadhi ya watu wanaotumika kuhamasisha vurugu nchini, hivyo ni muhimu kuwakataa kwani ustawi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya Taifa hayawezekani pasipokuwa na amani na utulivu. Msigwa amebainisha hayo leo Jumapili Mei 10, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Njombe kwenye shamba la muwekezaji wa zao la Parachichi pembezoni mwa Mji wa Njombe, akiwapongeza pia Watanzania kwa kuwakataa wale wanaohamasisha vurugu Nchini na kusisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kujielekeza katika habari zenye kuleta maendeleo na kuhamasisha umuhimu wa amani Nchini. “Najua maneno yapo mengi na wahamasishaji wamekuwa wengi. Mwalimu Nyerere alishatuambia kuwa mabeberu hawajalala na pia wakati mwingine wanawatumia miongoni mwa Watanzania kufikia malengo yao. Tuamke, hakuna nchi iliyofanikiwa kupata maendeleo ikiwa watu wake wanavurugana, wanagombana, wapo kwenye maandamano kila siku na kuhamasishana kuchoma miundombinu au kuharibu uchumi. Tukifika huko hatutatoboa.” “Nawaombeni ndugu zangu Watanzania tulinde amani yetu kwa wivu mkubwa, tukatae hamasa zozote zinazoashiria fujo na vurugu kwenye Nchi yetu. Tuwakatae wanaohamasisha vurugu na ninajua Watanzania wengi wamekataa na niwapongeze sana kwa hilo.”amesema Msigwa. Katika hatua nyingine, Msigwa pia amewataka Maafisa habari kote nchini kutenga muda na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania kama msingi wa kuweza kutekeleza Dira 2050 pamoja na hatua nyingine za maendeleo na ustawi wa jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto mchanga wa kike leo tarehe 11 Machi, 2026, katika makazi yake, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma. Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu, alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai. Akizungumza wakati wa kumkabidhi mtoto huyo, Mkuu wa Wilaya Tukai alisema mtoto huyo aliokotwa tarehe 17 Januari, 2026 akiwa ametelekezwa katika eneo jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, Nzega Mjini. Alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio. Rais Dkt. Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo. “Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” alisema Rais Dkt. Samia.