Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Kituo Cha Habari

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, amesema kuwa ujio wa wanamichezo wa kimataifa nchini Tanzania akiwemo mchezaji na nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand unashawishi wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo. Bw. Msigwa ameeleza hayo Mei 20, 2026 wakati akiwa safarini na mwanamichezo huyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia treni ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini. Ameongeza  kuwa wachezaji wa kimataifa wanapokuja nchini wanaongeza macho ya wadau mbalimbali wa michezo kuitazama nchi ya Tanzania na kuona ni namna gani wataweza kuwekeza  na nchi itaweza kunufaika kwa kupata mitaji ya kuwekeza kwenye michezo, wataalam wa kushirikiana nao pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na fursa ziliozopo duniani kupitia sekta hiyo. “Ujio wa mwanamichezo huyu, unapeleka ujumbe duniani kwamba Tanzania imejidhatiti kufanya mambo makubwa kwenye sekta ya michezo hivyo kupitia wao, nchi itafanikiwa kushawishi uwekezaji katika sekta ya michezo kwani nchi yetu ina changamoto kubwa kwenye eneo la uwekezaji hasa kwenye miundombinu ya michezo pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo jezi za wachezaji, viatu, mipira ambavyo tunaagiza kutoka nje. Vile vile, tunahitaji wataalam wa michezo ambao wataleta ujuzi wa namna ya kutengeneza viwanja.” Amesema Msigwa. Kwa upande wake, Mchezaji na Nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand amesema kuwa mpira wa miguu ukitumika vizuri unaweza kufungua fursa mbalimbali pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.  Amesema kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda pamoja na wadau wa sekta ya utalii ili kuongeza hamasa na ufuatiliaji wa sekta hiyo.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), linatarajia kuanza safari za ndege kuelekea nchini Urusi mnamo Juni, 2026. Ameyasema hayo Mei 15, 2026 jijini Arusha wakati aliposhiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi linaloendelea jijini humo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Waziri Mahmoud ameeleza kuwa, nchi ya Urusi inapendelea kupata mazao yenye viwango vya hali ya juu kutoka nchini Tanzania lakini huenda ni ngumu wafanyabiashara kukidhi kigezo hicho kutokana na uhaba wa usafiri wa haraka wa kufikisha bidhaa zikiwa na ubora wake. “Tunalishukuru shirika letu la ndege nchini kwa kukamilisha mikataba yote ambapo ifikapo Juni 2026, safari zitaanza kutoka Tanzania kwenda jijini Moscow na baadaye Saint Petersburg. Wakati ndege hizo zinarudi kutoka kwenye maeneo hayo, tunategemea zitabeba watalii watakaokuja kufanya utalii nchini katika maeneo ya Zanzibar, Kilimanjaro na Dar es Salaam”. Ameongeza kuwa, shirika hilo litakuwa na ndege itakayobeba mizigo hivyo, ametoa rai kwa wafanyabiashara wanaohitaji kusafirisha bidhaa kwa haraka kutumia usafiri huo. Ametaja baadhi ya fursa ambazo Tanzania na Urusi wanaweza kushirikiana ikiwemo ujenzi wa viwanda vya mbolea, vifaa vya kilimo, shughuli za ufungashaji, usindikaji na uhifadhi wa bidhaa, TEHAMA pamoja na dawa za binadamu.