BMH Yaendelea na Harambee ya TZS Bilioni 7 kusaidia Matibabu ya Upandikizaji Figo, Uloto
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetoa rai kwa Watanzania, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kuunga mkono harambee maalumu ya kuchangia matibabu ya upandikizaji figo na uloto kwa wagonjwa wenye uhitaji, hususan watoto wenye ugonjwa wa selimundu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Prof Abel Makubi amesema harambee hiyo ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo mwaka 2015, ambapo lengo ni kukusanya shilingi bilioni saba ndani ya kipindi cha miaka miwili ili kusaidia kuwatibu wananchi wasioweza kumudu gharama za matibabu hayo.
Amesema hospitali hiyo imeendelea kukua na kuwa kituo kikubwa cha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini, ikiwa na wataalamu wa afya zaidi ya 100 na kutoa huduma 20 za ubingwa pamoja na huduma 18 za ubingwa bobezi.
Baadhi ya huduma zinazotolewa ni upasuaji wa moyo, upandikizaji figo, upandikizaji uloto, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, pamoja na huduma nyingine za kisasa zinazopatikana ndani ya nchi.
“Tangu kuanza kwa huduma za upandikizaji figo mwaka 2018, jumla ya wagonjwa 56 wamefanyiwa upandikizaji wa figo nchini hatua iliyookoa zaidi ya shilingi bilioni 1.7 ambazo zingetumika kama wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi”, amesema Prof. Makubi.
“Vile vile huduma za upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu zilianza mwaka 2023 ambapo hadi sasa watoto 30 wamefanyiwa upandikizaji huo kwa mafanikio ikiwemo mtoto mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo huduma hizo zimeokoa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya Tanzania”, amemalizia Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, gharama za matibabu ya upandikizaji figo na uloto bado ni kubwa kwa wananchi wengi jambo lililoifanya kuanzisha mfuko maalumu wa kusaidia wagonjwa wenye uhitaji kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Kwa niaba ya Hospitali hiyo, Prof. Makubi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya hususan katika kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hospitalini hapo.
Comment (1)
Malaika
June 4, 2026Hii nzuri sana. Watanzania tunatakiwa kushikana kwenye haya pia,