Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema hali ya amani na usalama katika Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere. Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo leo Julai 7, 2026, Chalamila aliwapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki maonesho hayo, akisema ushiriki huo unaonesha wananchi wanatumia vyema fursa ya kujifunza, kufanya biashara na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na washiriki. Alisema Serikali inaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanatawala ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao bila hofu, huku akiwataka kupuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga kuwakatisha tamaa kushiriki maonesho hayo. Pokeeni salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tunaendelea kuhamasisha Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kuona teknolojia mpya, kununua bidhaa kwa bei nafuu na kujifunza ubunifu mbalimbali unaooneshwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Chalamila. Alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 25, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Jumanne Muliro alisema hali ya usalama katika jiji hilo inaendelea kuwa tulivu, huku akieleza kuwa tathmini ya maeneo mbalimbali, ikiwemo Kibamba, Kimara, Ubungo, Manzese, Tegeta, Bunju na Kigamboni, inaonesha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani. Aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika katika kipindi chote cha maonesho hayo, na kuwataka waendelee kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama. Muliro alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa, akiwahimiza Watanzania kuendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa utulivu na uzalendo.

Na Mwandishi Wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania duniani, kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na kuanzisha vituo vya utamaduni wa Kiswahili katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Ufaransa. Maelekezo hayo yamewasilishwa leo, Julai 7, 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASKIDU 2026) yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), jijini Paris, Ufaransa. Kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia, vituo hivyo vitakuwa kitovu cha kufundisha na kueneza lugha ya Kiswahili, kutangaza utamaduni wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla, pamoja na kuimarisha diplomasia ya utamaduni. Vilevile, vitafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kimataifa kupitia matumizi ya Kiswahili. Aidha, vituo hivyo vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuwawezesha wananchi wa mataifa mbalimbali kujifunza historia, urithi, mila, desturi na ustaarabu wa Afrika kupitia lugha ya Kiswahili, ambayo inaendelea kupata hadhi na kutambuliwa katika majukwaa ya kimataifa. Katika hatua nyingine, Rais Samia amewahimiza Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kuhakikisha wanawarithisha watoto wao lugha ya Kiswahili ili kudumisha utambulisho wa Taifa, kuimarisha mshikamano wa kizazi hadi kizazi na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa Tanzania. Amesisitiza kuwa kadri Kiswahili kinavyoendelea kupanua wigo wake duniani, ndivyo kinavyozidi kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushawishi wa Tanzania kimataifa, kukuza utamaduni wa Kiafrika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Na Baraka Messa- MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ( Sabasaba) yameendelea kuwa daraja muhimu linalowaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo ya 50 Julai 3,2026 jijini Dares Salaam amesema maonesho hayo yamekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania wengi, huku yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kukua na kuwa wawekezaji wakubwa kupitia upatikanaji wa masoko na mitaji. “Kwa karibu miaka 50, maonesho ya Sabasaba yamekuwa daraja la kuwaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji, huku yakiiunganisha Tanzania na dunia katika biashara na uwekezaji.” amesema. Amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku mafanikio hayo yakichangiwa na maboresho makubwa ya miundombinu na matumizi ya teknolojia yaliyofanywa na Serikali. Aidha, Rais Samia amesema diplomasia ya uchumi imeendelea kuzaa matunda ambapo katika mwaka uliopita mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yalifikia takribani dola za Marekani bilioni 17, sawa na ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na kipindi kilichopita. Pia, mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 35, yakionesha ukuaji wa sekta ya madini. Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, amesema Tanzania na Msumbiji zinapaswa kutumia historia yao ya ushirikiano kuimarisha uchumi wa kikanda kwa kubadilisha mipaka ya nchi hizo kuwa korido za maendeleo, biashara na uwekezaji badala ya kuwa vikwazo Amesema uchumi wa Tanzania na Msumbiji unakamilishana na una fursa kubwa ya kukuza minyororo ya thamani, biashara ya kikanda na uwekezaji kutokana na rasilimali nyingi, nguvu kazi ya vijana na nafasi ya kimkakati inayounganisha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitia Bahari ya Hindi. Aidha, Rais Chapo amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika waitazame Tanzania na Msumbiji kama washirika wa kuaminika wenye mazingira rafiki ya biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda, sayansi, ubunifu, uchumi wa kidijitali na akili Unde (AI).

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kujitegemea katika kugharamia shughuli za maendeleo kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani huku akieleza kuwa mchango wa makampuni, mashirika na taasisi za umma unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo. Rais Samia amesema hayo Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, Ikulu jijini Dar Es Salaam. Rais Samia ameeleza kuwa mafanikio hayo yatachangia kupunguza pengo la kujitegemea katika bajeti ya mwaka huu na kwa miaka miwili ijayo jambo linaloonyesha kuwa mikakati ya kuongeza mapato ya ndani imeanza kuzaa matunda. “Gawio na mchango uliotolewa na makampuni, taasisi na mashirika yetu ni sehemu ya lengo letu la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharamia shughuli za maendeleo” amesema Rais Samia Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa matumaini yataongezeka endapo kasi ya ukusanyaji wa mapato na ufanisi wa taasisi utaendelea kuimarika ndani ya miaka miwili ijayo, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kugharamia maendeleo yake kwa kutegemea vyanzo vya ndani pekee. Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amewaelekeza viongozi na watendaji wote kutoridhika na pongezi wanazopata, bali amewasisitiza kuwa, pongezi hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii, ubunifu na maarifa ili kufikia matokeo makubwa zaidi katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa mapato. Kadhalika, ameeleza kuwa maendeleo ya uchumi wa Taifa yanahitaji uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa rasilimali na juhudi endelevu kutoka kwa taasisi zote za umma ili kuhakikisha mchango wao unaendelea kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo.