Tanzania Yapiga Hatua Kuelekea Kujitegemea Kugharamia Maendeleo
Na Josephina Lupasha – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kujitegemea katika kugharamia shughuli za maendeleo kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani huku akieleza kuwa mchango wa makampuni, mashirika na taasisi za umma unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo.
Rais Samia amesema hayo Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, Ikulu jijini Dar Es Salaam.

Rais Samia ameeleza kuwa mafanikio hayo yatachangia kupunguza pengo la kujitegemea katika bajeti ya mwaka huu na kwa miaka miwili ijayo jambo linaloonyesha kuwa mikakati ya kuongeza mapato ya ndani imeanza kuzaa matunda.
“Gawio na mchango uliotolewa na makampuni, taasisi na mashirika yetu ni sehemu ya lengo letu la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharamia shughuli za maendeleo” amesema Rais Samia
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa matumaini yataongezeka endapo kasi ya ukusanyaji wa mapato na ufanisi wa taasisi utaendelea kuimarika ndani ya miaka miwili ijayo, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kugharamia maendeleo yake kwa kutegemea vyanzo vya ndani pekee.

Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amewaelekeza viongozi na watendaji wote kutoridhika na pongezi wanazopata, bali amewasisitiza kuwa, pongezi hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii, ubunifu na maarifa ili kufikia matokeo makubwa zaidi katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa mapato.
Kadhalika, ameeleza kuwa maendeleo ya uchumi wa Taifa yanahitaji uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa rasilimali na juhudi endelevu kutoka kwa taasisi zote za umma ili kuhakikisha mchango wao unaendelea kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo.