Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Katika miji inayokua kwa kasi, biashara ndogo ndogo zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wananchi. Kwa maelfu ya Watanzania, biashara hizo ni chanzo cha ajira, kipato na mahitaji ya kila siku ya familia. Hata hivyo, ukuaji wa shughuli hizo unahitaji usimamizi wenye mipango unaozingatia maslahi ya wafanyabiashara, wananchi na ustawi wa miji. Ni kwa kuzingatia umuhimu huo ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa umakini suala la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga, akieleza kuwa wameanza kurejea kwa kasi katika maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara wakubwa. Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa. Amesema suala la wafanyabiashara wadogo lilikuwa likisimamiwa vizuri, lakini kwa sasa kumekuwa na kulegalega katika utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa. Suala la wafanyabiashara wadogo wadogo, tulikuwa tunalisimamia vizuri, lakini kwa sasa tumepunguza usimamizi hasa katika Majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Dodoma, amesema Rais Samia. Kwa Rais Samia, changamoto ya Machinga kurejea katika maeneo ya wafanyabiashara wakubwa haiwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu au kuwaondoa bila kuwa na mpango mbadala. Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuweka mipango mizuri itakayowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao katika maeneo salama na yaliyopangwa. Si kwa kuwapiga fimbo au kuwapeleka Askari Mgambo kwenda kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke, tuwapangie mipango mizuri, watoke walipo na warudi kwenye masoko, ameagiza. Kauli hiyo inaweka msisitizo kwenye matumizi ya mipango badala ya nguvu, ili kutatua changamoto ya wafanyabiashara wadogo kwa njia inayolinda utu wao na wakati huo huo kuhakikisha miji inakuwa na mpangilio unaokubalika. Biashara za Machinga zina nafasi kubwa katika uchumi wa wananchi kwa kuwa zinawawezesha watu wengi kujiajiri na kupata kipato bila kutegemea ajira rasmi. Kwa baadhi ya wananchi, biashara hizi ni hatua ya kwanza ya kujenga mtaji, kukuza biashara na hatimaye kuingia katika shughuli kubwa zaidi za kiuchumi. Hivyo, usimamizi wa wafanyabiashara hao unahitaji kuangalia zaidi namna ya kuwawezesha kukua kuliko kuwaona kama tatizo linalopaswa kuondolewa katika maeneo ya mijini. Mipango mizuri ya upangaji wa maeneo ya biashara inaweza kuwasaidia Machinga kupata maeneo yenye wateja, mazingira salama na huduma muhimu, huku ikisaidia pia kupunguza msongamano na migongano kati ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Maelekezo ya Rais Samia kwa viongozi ya kuwarudisha wafanyabiashara wadogo katika masoko yanapaswa kutafsiriwa kama wito wa kuhakikisha maeneo hayo yana mazingira yanayoweza kuwawezesha kufanya biashara kwa tija. Soko lenye mpangilio mzuri, usalama, usafi na mazingira rafiki kwa biashara linaweza kuwa zaidi ya sehemu ya kuuza bidhaa; linaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea huduma zao. Kwa mtazamo huo, kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyofaa kunapaswa kuambatana na kuwaandalia maeneo mbadala yenye uwezo wa kuwasaidia kuendelea kujipatia kipato. Ujumbe wa Rais Samia pia unawakumbusha viongozi kuwa utekelezaji wa sheria na mipango ya miji unapaswa kwenda sambamba na kuheshimu utu wa wananchi. Wafanyabiashara wadogo wanapaswa kupewa maelekezo yanayoeleweka, kushirikishwa katika mipango inayowahusu na kupewa muda na mazingira yanayowawezesha kuhamia katika maeneo yaliyopangwa. Kwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kufikia malengo mawili kwa wakati mmoja: kuweka miji katika mpangilio unaotakiwa na kulinda fursa za kiuchumi za wananchi. Maelekezo ya Rais Samia yanaibua umuhimu wa kutafuta uwiano kati ya maendeleo ya miji na mahitaji ya wananchi wanaotegemea biashara ndogo ndogo. Miji inahitaji kuwa na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara mbalimbali, huku wafanyabiashara nao wakihitaji mazingira yatakayowawezesha kufanya biashara bila kuvunja taratibu zilizowekwa. Hivyo, suluhisho la changamoto ya Machinga si kuwafukuza kutoka eneo moja kwenda jingine, bali ni kuwa na mpango endelevu wa upangaji, ugawaji wa maeneo na usimamizi wa biashara ndogo ndogo. Kwa kufanya hivyo, biashara ndogo zinaweza kuendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi, huku miji ikiendelea kuwa safi, salama na yenye mpangilio. Hatua hiyo pia itaimarisha uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara wadogo kwa kujenga mazingira ambayo wananchi wanaona kuwa mipango ya Serikali inalenga kuwawezesha, badala ya kuwazuia kujitafutia maisha. Ujumbe wa Rais Samia ni kwamba Machinga wanahitaji kupangwa na kuwezeshwa, si kubughudhiwa Wanahitaji maeneo yanayofaa kwa biashara, viongozi wenye mipango na utekelezaji unaozingatia utu.

        Na Baraka Messa – MAELEZO Utambulisho ni msingi muhimu katika maisha ya kila mwananchi, kwani humwezesha mtu kutambulika kisheria, kupata huduma za kijamii na kiuchumi, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutekeleza haki na wajibu wake kwa urahisi. Kutokana na umuhimu huo, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Septemba 16, 2026, huku nchini maadhimisho hayo yakianza Septemba Mosi kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto ya mabilioni ya watu ambao hawana utambulisho rasmi, hali inayowakosesha fursa ya kupata baadhi ya huduma muhimu. Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Msigwa amesema tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu wasio na utambulisho wa kisheria. Anasema hali hiyo imechochea juhudi za pamoja za mataifa ya Afrika na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtu anapata utambulisho rasmi unaomwezesha kutambulika na kupata haki pamoja na huduma muhimu za kijamii na kiuchumi. Katika safari hiyo, Msigwa amesema Tanzania imejijengea nafasi muhimu kutokana na hatua ilizochukua mapema kuanzisha mfumo wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua ambayo imeendelea kuimarisha mifumo ya utambulisho nchini. Anasema mchakato wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ulianza mwaka 2012 kwa majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Msigwa anasema, NIDA imepewa majukumu mbalimbali ya msingi, yakiwemo kuwatambua na kuwasajili watu wanaoishi nchini wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia na wageni wakazi, pamoja na kutunza takwimu za usajili na utambuzi wa watu na kushirikishana taarifa hizo na wadau kwa mujibu wa sheria. Tanzania imepiga hatua kubwa katika usajili. Kufikia Julai 2026, jumla ya watu 27,455,882 wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.2 ya watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, ambao ni 31,477,938 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, anasema Msigwa. Anasema katika kipindi hicho, jumla ya Vitambulisho vya Taifa 21,526,585 vilizalishwa, sawa na asilimia 92.2 ya namba za utambulisho 23,344,265 zilizotolewa, huku vitambulisho 20,935,351 vikiwa vimegawiwa kwa wananchi, sawa na asilimia 97.2 ya vitambulisho vilivyozalishwa. Msigwa anasema mfumo wa utambulisho umeleta manufaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kusaidia taasisi zinazohusika na usalama kudhibiti uhalifu, kupunguza udanganyifu, kudhibiti utakatishaji fedha na kufuatilia shughuli mbalimbali zinazohitaji uthibitisho wa utambulisho wa mtu. Anasema pia matumizi ya Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) yamewezesha usajili wa laini za simu 92,735,799, hatua inayosaidia kupunguza udanganyifu na kuimarisha usalama katika mfumo wa mawasiliano, huku mfumo huo ukiwezesha wananchi, wakiwemo wazee, wanawake na vijana, kufungua akaunti na kupata huduma za kifedha na mikopo. Utambulisho pia umewezesha wananchi kutambuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kupata huduma za matibabu kwa urahisi, wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo na kuiwasilisha kwa urahisi, pamoja na TASAF kuhakiki walengwa na kufanya malipo kwa ufanisi zaidi, anasema. Aidha, Msigwa amesema Serikali inaendelea na mpango wa kufanya maboresho katika mfumo wa Vitambulisho vya Taifa, hususan katika teknolojia ya uzalishaji na uchapishaji wa vitambulisho, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kubaini umuhimu wa kuendana na teknolojia za kisasa. Anasema miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni kuhamia kutoka teknolojia inayotumika sasa kwenda teknolojia inayotumia mionzi katika uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua inayolenga kuongeza ubora na usalama wa vitambulisho hivyo. Pamoja na hayo Msigwa, amesema Serikali inalenga kufanya Kitambulisho cha Taifa kuwa nyenzo pana zaidi ya utambulisho kwa kuunganisha taarifa muhimu za huduma anazopata mwananchi. Kadi ya Kitambulisho cha Taifa itabeba taarifa za utambulisho wa mtu pamoja na taarifa muhimu za huduma, zikiwemo bima ya afya na leseni ya udereva, anasema Msigwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA, Edson Guyai, amefafanua matumizi ya Kitambulisho cha Taifa cha NIDA na Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar (ZAN ID), akisema NIDA ni taasisi ya Muungano hivyo Kitambulisho cha Taifa hutumika kumtambua mwananchi akiwa Tanzania Bara au Zanzibar. NIDA ni taasisi ya Muungano, Kwa hiyo, huduma zote za Muungano Kitambulisho cha Taifa cha NIDA hutumika kumtambua mwananchi akiwa Zanzibar au Tanzania Bara, Hata hivyo, kuna huduma ambazo ni mahsusi kwa Zanzibar, hivyo katika huduma hizo hutumika Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar, amesema Guyai. Guyai anawataka wananchi ambao Vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika, wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5, kwenda kuvichukua katika vituo husika ili waanze kuvitumia kupata huduma mbalimbali, Anasema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na mfumo wa utambulisho wa taifa. Kwa ujumla, Mfumo huu, ambao umeanza kama njia ya kumtambua mtu, sasa unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, usalama, uchumi na utoaji wa huduma, huku Serikali ikiendelea kuboresha teknolojia ili kuhakikisha kila mwananchi anatambulika na anapata huduma kwa ufanisi.

Na Jacqueline Mrisho MAELEZO. Hatimaye Tanzania imeshuhudia kutimia kwa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kujenga bwawa katika eneo la Stiegler’s Gorge kwenye Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosha kwa maendeleo ya Taifa. Wazo hilo lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1976 liliendelea kuenziwa na viongozi waliomfuata, wakiwemo Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Licha ya kukabiliwa na changamoto na upinzani mbalimbali ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ilichukua hatua ya kutafuta fedha, kutatua changamoto na kuanza utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati. Leo, Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa sehemu muhimu ya jitihada za Tanzania kuhakikisha Taifa linakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii. Mradi huo una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Taifa kuzalisha umeme na kusaidia kuondoa changamoto ya upungufu na mgao wa umeme uliokuwa ukiathiri uzalishaji viwandani, huduma za jamii, biashara na matumizi ya majumbani. Umeme huo umefungua nafasi kubwa kwa uwekezaji, viwanda, biashara, utalii, uzalishaji na ajira, huku ukitoa fursa ya kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa. Akizindua mradi huo Agosti 22, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kukamilika kwa mradi huo ni fundisho kwamba mafanikio ya miradi ya kimkakati yanahitaji uthubutu, uthabiti na ufuatiliaji wa karibu. Tunapofanya maamuzi yenye maslahi kwa Taifa, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu njia ya kufanikisha ni ngumu bali tunapaswa kuwa na uthubutu na uthabiti wa kuyasimamia maono na maamuzi yetu ili kufikia malengo tuliyojiwekea na manufaa tunayoyatarajia, alisema Rais Samia. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Felischem Mramba, amesema mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, hali inayoashiria pia ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Amesema Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa msingi muhimu wa kuondoa mgao wa umeme na kuwezesha Tanzania kuendelea na uwekezaji katika uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji, kuimarisha utalii na kukuza shughuli nyingine za uzalishaji. Bwawa hili limetutoa kwenye mgawanyo wa umeme kama nchi, na linatuhakikishia sasa kwamba tunaweza kuendelea kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda, tunaweza kualika wawekezaji kutoka nje wakaja kuwekeza kwenye uchumi wetu, tunaweza kuboresha utalii na mambo mengine mbalimbali ambayo ndiyo hasa yanayokuza uchumi wetu, amesema. Kukamilika kwa bwawa hilo ni hatua moja katika kuhakikisha umeme unaowafikia wananchi wote. Serikali inaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa, ikiwemo kukamilisha njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Zuzu, Dodoma. Kupitia kituo hicho, umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unasafirishwa kwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini. Jitihada hizo zimepanua wigo wa upatikanaji wa umeme, ambapo hadi sasa vijiji vyote 12,318 na takribani asilimia 62.4 ya vitongoji Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha nchi nzima inapata umeme ifikapo mwaka 2030. Uwezo mkubwa wa uzalishaji umeifanya Tanzania kuwa na umeme wa ziada, unaoweza kutumika kwa mahitaji ya ndani na kuuzwa katika nchi jirani ili kuongeza mapato na upatikanaji wa fedha za kigeni. Tayari Tanzania imepokea maombi kutoka nchi mbalimbali. Zambia imeonesha hitaji la kati ya Megawati 500 na 600, Rwanda inahitaji Megawati 100, huku Kenya ikikubaliana na Tanzania kuhusu uwezekano wa kufanya mabadilishano ya umeme. Hii inaifanya Tanzania kuingia katika hatua mpya, ambapo umeme hauwi tu huduma muhimu kwa maendeleo ya ndani, bali pia bidhaa yenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani. Pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vingine vya nishati, ikiwemo jua, upepo na nishati ya jotoardhi (thermal), ili kuongeza uwezo wa Taifa kuzalisha umeme kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Hatua hizi zinaifanya Tanzania kujenga msingi wa nishati unaoweza kuhimili mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ukifungua milango zaidi kwa viwanda, uwekezaji, biashara na ajira. Kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya Tanzania yenye nishati ya kutosha, uchumi unaokua na fursa zinazoongezeka kwa wananchi.