Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 wananchi wa maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo lakini bado yana mazingira ya vijijini, ili waendelee kunufaika na huduma hiyo kwa gharama nafuu. Akizungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, Oktoba 16, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja, Dkt. Mwigulu amesema kupandishwa kwa hadhi ya eneo kuwa mji mdogo hakumaanishi kuwa uwezo wa kiuchumi wa wananchi umeongezeka, hivyo gharama za kuunganishiwa umeme zinapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha yao. Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo, niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini. Kuhusu hadhi ya Bagamoyo, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya kurasimisha hadhi hiyo itapatikana wiki ijayo, akieleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kilichobaki ni kukamilisha taratibu. Katika kushughulikia kero za ardhi, amemwagiza Kamishna wa Ardhi kuongoza mwenyewe kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua migogoro ya wananchi wa Bagamoyo kuanzia Jumatatu inayofuata, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka makao makuu, mkoa na ofisi husika za Serikali kwa muda wa wiki nzima. Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe. Amesema migogoro ya ardhi inaweza kuhatarisha undugu na mshikamano wa wananchi. Ameeleza kuwa tayari amewaelekeza Waziri wa Ardhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia upya utaratibu wa kutatua migogoro hiyo. Pia, amesisitiza wananchi wanaopisha uwekezaji na miradi ya maendeleo kulipwa fidia stahiki bila kupunjwa. Katika sekta ya afya, Waziri Mkuu amekataza kutozwa kwa wananchi gharama za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa wanaopelekwa hospitali za rufaa, akizitaka mamlaka husika kuhakikisha magari hayo yana mafuta ya kutosha na yanatoa huduma kwa wakati. Aidha, amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya kutokuzuia miili ya marehemu hospitalini kwa sababu ya madai ya malipo. Vilevile, ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia ununuzi, usambazaji na matumizi ya dawa za Serikali ili kuhakikisha zinawafikia wananchi waliokusudiwa. Akizungumzia uchumi na ajira, Dkt. Mwigulu amesema sekta binafsi imara na viwanda vya kuchakata mazao ni muhimu katika kuongeza ajira na kipato cha wananchi. Amewahimiza kutumia fursa za uwekezaji na uzalishaji, huku wakizingatia matumizi bora ya ardhi na sheria za nchi.    

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kupanua usambazaji wa umeme, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi. Akizungumza Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini mkataba na uzinduzi wa mpango wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, , amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa uhakika na kwa urahisi zaidi. Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme ni kukamilika na kuanza kuzalisha kwa Bwawa la Julius Nyerere, lililopo katika Mto Rufiji, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema ongezeko la uzalishaji linaenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji ili umeme uwafikie walaji wa mwisho. Mhe. Ndejembi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme nchini, ikiwemo jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya Shilingi bilioni 231 zimetengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kuimarisha huduma hiyo. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vikubwa vya kusambaza umeme, ikiwemo Dege na Mabibo, pamoja na ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi, Kimara, Ilala, Ubungo na Ununio, hatua inayolenga kuongeza uwezo na uhakika wa huduma ya umeme jijini Dar es Salaam. Akizungumza kuhusu mwelekeo wa muda mrefu, Makamu wa Rais amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta ya nishati nafasi muhimu katika kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia tija, ushindani, ubunifu na matumizi ya teknolojia. Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na megawati 74,000 ifikapo mwaka 2050. Aidha, amesema Tanzania inaendelea kushiriki katika juhudi za kimataifa za kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika kupitia ‘Mission 300’, unaolenga kuwaunganisha takribani watu milioni 300 barani Afrika na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia iliandaa Mkutano wa Africa Energy Summit – Mission 300 jijini Dar es Salaam mwaka 2025. Mhe. Ndejembi ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zake na sekta binafsi katika kuharakisha uwekezaji wa nishati. Amesema umeme unaofikishwa kwa wananchi unapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, uzalishaji, biashara, teknolojia na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo jitihada za kuongeza uzalishaji zinapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa ufanisi.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa kufungua fursa mpya za maendeleo kwa Taifa linalolenga kuongeza uzalishaji, kukuza viwanda na kujenga uchumi shindani. Tanzania inapofikisha ziada ya Megawati 2,000 za umeme, hatua hiyo inaashiria uwezo mkubwa wa nchi katika kuzalisha nishati ambayo inapaswa kugeuzwa kuwa kichocheo cha uzalishaji, uwekezaji, viwanda, kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi. Uwepo wa megawati 2000 za ziada ni habari njema kwa Watanzania kuichangamkia fursa hiyo na kutumia nguvu ya umeme kujenga uchumi wenye tija na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa. Akiongea hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika Bariadi mkoani Simiyu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Tanzania kwa sasa ina ziada ya MW 2,000 za umeme, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya uzalishaji wa nishati ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, SADC na maeneo mengine ya Afrika. Ziada hiyo ya umeme inapaswa kutazamwa kama fursa ya uzalishaji. Wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kutumia mazingira hayo kuanzisha na kupanua viwanda, hasa viwanda vidogo na vya kati vinavyoweza kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao. Kilimo, mifugo, uvuvi na madini vinaweza kuongezewa thamani kupitia uchakataji unaotumia umeme, na hivyo kuongeza kipato na ajira. Mkulima, kwa mfano, hapaswi kuishia kuuza zao ghafi ikiwa anaweza kulichakata na kupata bidhaa yenye thamani zaidi. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, mazao ya nafaka yanaweza kuchakatwa, maziwa yanaweza kuongezwa thamani na mazao mengine yanaweza kuhifadhiwa au kusindikwa kwa kutumia teknolojia. Hapo ndipo umeme unapogeuka kuwa mtaji wa uzalishaji. Kwa wafanyabiashara na vijana, ongezeko la upatikanaji wa umeme linaweza kufungua milango ya shughuli mpya. Kuanzia karakana na mashine za uzalishaji hadi teknolojia, huduma za kidijitali na biashara zinazohitaji nishati ya uhakika. Fursa hiyo inahitaji ubunifu na hatua, si kusubiri. Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuifanya nguvu hiyo iwafikie wananchi. Kupitia Mradi wa Gridi Imara, unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bariadi, uwezo wa gridi unaendelea kuimarishwa ili kuongeza uhakika wa usambazaji wa umeme. Aidha, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 302 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, hatua iliyowezesha mkoa wa Simiyu kufikisha huduma hiyo katika vijiji vyote 478. Hii ni nafasi ya wananchi wa mijini na vijijini kuangalia umeme kwa jicho jipya. Si huduma ya kutumia majumbani pekee, bali ni rasilimali ya kuzalisha utajiri. Kila eneo lenye umeme linaweza kuwa eneo la uzalishaji ikiwa wananchi watatumia fursa hiyo kuanzisha biashara, viwanda na shughuli zinazoongeza thamani. Tanzania pia ina rasilimali nyingi zinazoweza kuunganishwa na nguvu hii ya nishati. Ardhi, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini vinaweza kutoa malighafi kwa viwanda vya ndani. Changamoto sasa ni kuongeza ubunifu, uwekezaji na uzalishaji ili nishati inayopatikana itumike kikamilifu katika kuongeza thamani ya rasilimali hizo. Kwa vijana, wajasiriamali na wawekezaji, ujumbe ni mmoja tu kwao: Fursa hii isitazamwe kama takwimu ya Serikali, bali kama nafasi ya kufanya biashara na kuzalisha. Badala ya kusubiri ajira, mazingira haya yanatoa nafasi ya kuanzisha shughuli zinazoweza kutengeneza ajira kwa wengine. Ziada ya Megawati 2,000 pia ina maana kwamba Tanzania ina nafasi ya kujiandaa kwa mahitaji makubwa zaidi ya nishati yatakayotokana na ukuaji wa viwanda, miji na shughuli za kiuchumi. Hivyo, hatua inayofuata ni kuhakikisha uwezo huo unabadilishwa kuwa uzalishaji halisi na thamani kwa wananchi. Nguvu ya umeme inakuwa nguvu ya uchumi pale inapogeuzwa kuwa uzalishaji. Na uzalishaji unaanza pale wananchi wanapochukua hatua. Megawati 2,000 za ziada ni mwaliko kwa Watanzania kuchangamkia fursa, kuanzisha viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza biashara na kujenga ajira. Tanzania ina umeme wa kuzalisha zaidi; sasa ni wakati wa wananchi kuzalisha zaidi.

Na Jacqueline Mrisho MAELEZO. Hatimaye Tanzania imeshuhudia kutimia kwa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kujenga bwawa katika eneo la Stiegler’s Gorge kwenye Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosha kwa maendeleo ya Taifa. Wazo hilo lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1976 liliendelea kuenziwa na viongozi waliomfuata, wakiwemo Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Licha ya kukabiliwa na changamoto na upinzani mbalimbali ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ilichukua hatua ya kutafuta fedha, kutatua changamoto na kuanza utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati. Leo, Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa sehemu muhimu ya jitihada za Tanzania kuhakikisha Taifa linakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii. Mradi huo una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Taifa kuzalisha umeme na kusaidia kuondoa changamoto ya upungufu na mgao wa umeme uliokuwa ukiathiri uzalishaji viwandani, huduma za jamii, biashara na matumizi ya majumbani. Umeme huo umefungua nafasi kubwa kwa uwekezaji, viwanda, biashara, utalii, uzalishaji na ajira, huku ukitoa fursa ya kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa. Akizindua mradi huo Agosti 22, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kukamilika kwa mradi huo ni fundisho kwamba mafanikio ya miradi ya kimkakati yanahitaji uthubutu, uthabiti na ufuatiliaji wa karibu. Tunapofanya maamuzi yenye maslahi kwa Taifa, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu njia ya kufanikisha ni ngumu bali tunapaswa kuwa na uthubutu na uthabiti wa kuyasimamia maono na maamuzi yetu ili kufikia malengo tuliyojiwekea na manufaa tunayoyatarajia, alisema Rais Samia. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Felischem Mramba, amesema mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, hali inayoashiria pia ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Amesema Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa msingi muhimu wa kuondoa mgao wa umeme na kuwezesha Tanzania kuendelea na uwekezaji katika uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji, kuimarisha utalii na kukuza shughuli nyingine za uzalishaji. Bwawa hili limetutoa kwenye mgawanyo wa umeme kama nchi, na linatuhakikishia sasa kwamba tunaweza kuendelea kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda, tunaweza kualika wawekezaji kutoka nje wakaja kuwekeza kwenye uchumi wetu, tunaweza kuboresha utalii na mambo mengine mbalimbali ambayo ndiyo hasa yanayokuza uchumi wetu, amesema. Kukamilika kwa bwawa hilo ni hatua moja katika kuhakikisha umeme unaowafikia wananchi wote. Serikali inaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa, ikiwemo kukamilisha njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Zuzu, Dodoma. Kupitia kituo hicho, umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unasafirishwa kwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini. Jitihada hizo zimepanua wigo wa upatikanaji wa umeme, ambapo hadi sasa vijiji vyote 12,318 na takribani asilimia 62.4 ya vitongoji Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha nchi nzima inapata umeme ifikapo mwaka 2030. Uwezo mkubwa wa uzalishaji umeifanya Tanzania kuwa na umeme wa ziada, unaoweza kutumika kwa mahitaji ya ndani na kuuzwa katika nchi jirani ili kuongeza mapato na upatikanaji wa fedha za kigeni. Tayari Tanzania imepokea maombi kutoka nchi mbalimbali. Zambia imeonesha hitaji la kati ya Megawati 500 na 600, Rwanda inahitaji Megawati 100, huku Kenya ikikubaliana na Tanzania kuhusu uwezekano wa kufanya mabadilishano ya umeme. Hii inaifanya Tanzania kuingia katika hatua mpya, ambapo umeme hauwi tu huduma muhimu kwa maendeleo ya ndani, bali pia bidhaa yenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani. Pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vingine vya nishati, ikiwemo jua, upepo na nishati ya jotoardhi (thermal), ili kuongeza uwezo wa Taifa kuzalisha umeme kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Hatua hizi zinaifanya Tanzania kujenga msingi wa nishati unaoweza kuhimili mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ukifungua milango zaidi kwa viwanda, uwekezaji, biashara na ajira. Kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya Tanzania yenye nishati ya kutosha, uchumi unaokua na fursa zinazoongezeka kwa wananchi.