Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Asilimia 87.2 Wasajiliwa na NIDA

September 6, 2026

 

 

 

 

Na Baraka Messa – MAELEZO

Utambulisho ni msingi muhimu katika maisha ya kila mwananchi, kwani humwezesha mtu kutambulika kisheria, kupata huduma za kijamii na kiuchumi, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutekeleza haki na wajibu wake kwa urahisi.

Kutokana na umuhimu huo, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Septemba 16, 2026, huku nchini maadhimisho hayo yakianza Septemba Mosi kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto ya mabilioni ya watu ambao hawana utambulisho rasmi, hali inayowakosesha fursa ya kupata baadhi ya huduma muhimu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Msigwa amesema tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu wasio na utambulisho wa kisheria.

Anasema hali hiyo imechochea juhudi za pamoja za mataifa ya Afrika na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtu anapata utambulisho rasmi unaomwezesha kutambulika na kupata haki pamoja na huduma muhimu za kijamii na kiuchumi.

Katika safari hiyo, Msigwa amesema Tanzania imejijengea nafasi muhimu kutokana na hatua ilizochukua mapema kuanzisha mfumo wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua ambayo imeendelea kuimarisha mifumo ya utambulisho nchini.

Anasema mchakato wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ulianza mwaka 2012 kwa majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Msigwa anasema, NIDA imepewa majukumu mbalimbali ya msingi, yakiwemo kuwatambua na kuwasajili watu wanaoishi nchini wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia na wageni wakazi, pamoja na kutunza takwimu za usajili na utambuzi wa watu na kushirikishana taarifa hizo na wadau kwa mujibu wa sheria.

Tanzania imepiga hatua kubwa katika usajili. Kufikia Julai 2026, jumla ya watu 27,455,882 wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.2 ya watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, ambao ni 31,477,938 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, anasema Msigwa.

Anasema katika kipindi hicho, jumla ya Vitambulisho vya Taifa 21,526,585 vilizalishwa, sawa na asilimia 92.2 ya namba za utambulisho 23,344,265 zilizotolewa, huku vitambulisho 20,935,351 vikiwa vimegawiwa kwa wananchi, sawa na asilimia 97.2 ya vitambulisho vilivyozalishwa.

Msigwa anasema mfumo wa utambulisho umeleta manufaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kusaidia taasisi zinazohusika na usalama kudhibiti uhalifu, kupunguza udanganyifu, kudhibiti utakatishaji fedha na kufuatilia shughuli mbalimbali zinazohitaji uthibitisho wa utambulisho wa mtu.

Anasema pia matumizi ya Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) yamewezesha usajili wa laini za simu 92,735,799, hatua inayosaidia kupunguza udanganyifu na kuimarisha usalama katika mfumo wa mawasiliano, huku mfumo huo ukiwezesha wananchi, wakiwemo wazee, wanawake na vijana, kufungua akaunti na kupata huduma za kifedha na mikopo.

Utambulisho pia umewezesha wananchi kutambuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kupata huduma za matibabu kwa urahisi, wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo na kuiwasilisha kwa urahisi, pamoja na TASAF kuhakiki walengwa na kufanya malipo kwa ufanisi zaidi, anasema.

Aidha, Msigwa amesema Serikali inaendelea na mpango wa kufanya maboresho katika mfumo wa Vitambulisho vya Taifa, hususan katika teknolojia ya uzalishaji na uchapishaji wa vitambulisho, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kubaini umuhimu wa kuendana na teknolojia za kisasa.

Anasema miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni kuhamia kutoka teknolojia inayotumika sasa kwenda teknolojia inayotumia mionzi katika uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua inayolenga kuongeza ubora na usalama wa vitambulisho hivyo.

Pamoja na hayo Msigwa, amesema Serikali inalenga kufanya Kitambulisho cha Taifa kuwa nyenzo pana zaidi ya utambulisho kwa kuunganisha taarifa muhimu za huduma anazopata mwananchi.

Kadi ya Kitambulisho cha Taifa itabeba taarifa za utambulisho wa mtu pamoja na taarifa muhimu za huduma, zikiwemo bima ya afya na leseni ya udereva, anasema Msigwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA, Edson Guyai, amefafanua matumizi ya Kitambulisho cha Taifa cha NIDA na Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar (ZAN ID), akisema NIDA ni taasisi ya Muungano hivyo Kitambulisho cha Taifa hutumika kumtambua mwananchi akiwa Tanzania Bara au Zanzibar.

NIDA ni taasisi ya Muungano, Kwa hiyo, huduma zote za Muungano Kitambulisho cha Taifa cha NIDA hutumika kumtambua mwananchi akiwa Zanzibar au Tanzania Bara, Hata hivyo, kuna huduma ambazo ni mahsusi kwa Zanzibar, hivyo katika huduma hizo hutumika Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar, amesema Guyai.

Guyai anawataka wananchi ambao Vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika, wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5, kwenda kuvichukua katika vituo husika ili waanze kuvitumia kupata huduma mbalimbali, Anasema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na mfumo wa utambulisho wa taifa.

Kwa ujumla, Mfumo huu, ambao umeanza kama njia ya kumtambua mtu, sasa unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, usalama, uchumi na utoaji wa huduma, huku Serikali ikiendelea kuboresha teknolojia ili kuhakikisha kila mwananchi anatambulika na anapata huduma kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *