Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Bajeti Kuu ya Serikali Yapitishwa kwa Kishindo Bungeni

June 23, 2026

Na Baraka Messa – MAELEZO

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya Wabunge wengi kuunga mkono mapendekezo ya matumizi na makusanyo ya Serikali yaliyowasilishwa bungeni.

Akitoa matokeo ya kura zilizopigwa Juni 23, 2026, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema jumla ya wabunge 395 walihudhuria kikao hicho huku wabunge wanane wakikosekana.

Mhe. Zungu amesema kati ya wabunge waliohudhuria, wabunge 385 walipiga kura za ndiyo, sawa na asilimia 97.26 ya kura zote zilizopigwa, huku wabunge wanane wakipiga kura za hapana. Matokeo hayo yamedhihirisha uungwaji mkono mkubwa wa bajeti hiyo kutoka kwa wajumbe wa Bunge.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatoa idhini kwa Serikali kuendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo pamoja na shughuli za kawaida za kiutawala katika mwaka mpya wa fedha.

Bajeti hiyo imelenga kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kuendeleza miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mipango ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza ustawi wa wananchi.

Amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Prof. Mkumbo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochangia kuongezeka kwa uzalishaji na mapato ya taifa.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango na miradi iliyopangwa, ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania katika miaka ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *