Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Afrika Ijenge Uwezo wake wa Kusimamia na kuzalisha Huduma za Afya

September 9, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani wa kugharamia, kusimamia na kuzalisha mahitaji muhimu ya huduma za afya, badala ya kuendelea kutegemea misaada na mifumo kutoka nje.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, ukishirikisha zaidi ya washiriki 2,700 kutoka mataifa 27.

Amesema wakati umefika kwa Afrika kubadili namna inavyoelewa na kutekeleza dhana ya kujenga uwezo, akisisitiza kuwa dhana hiyo haipaswi kuishia katika miradi midogo isiyojenga uwezo wa kudumu, bali ielekezwe katika uwekezaji wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia na wataalamu.

Enzi zile nikiwa Waziri wa Fedha nilikuwa nawaambia nchi za Afrika zimeshashuhudia muda mrefu sasa wa maisha ya misaada na misaada inayoelekezwa pengine katika maeneo ambayo yanatofautiana na malengo ya ndani ya nchi kwa jina la capacity building. Capacity building. Capacity building. Na ndio tunaishia chapati, mandazi, sambusa. Hatuwekezi kitu kitakachodumu na kikawa endelevu.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, malengo ya ndani ya nchi yanayokwenda sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuheshimiwa na washirika wa maendeleo, ili misaada na uwekezaji katika sekta ya afya viweze kuacha matokeo ya kudumu kwa wananchi wa Afrika.

Amesema Tanzania inaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza miundombinu, rasilimali watu pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambayo Serikali imeanza kuitekeleza mwaka 2026.

Tunapozungumza kuhusu afya ya msingi, tusizungumzie tu kujenga vituo vya afya. Tujenge pia uwezo wa nchi zetu kugharamia huduma hizo, kuzalisha mahitaji yake na kutumia teknolojia zetu wenyewe.

Ameongeza kuwa Tanzania imeanza kuwekeza katika uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa kwa lengo la kupunguza utegemezi wa misaada na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuwa wa uhakika, hususan wakati dunia inapokumbwa na changamoto zinazoathiri minyororo ya usambazaji.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza ajira katika sekta hiyo, hatua ambazo zitasaidia kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Mwigulu amesema mkutano huo unapaswa kuzaa hatua mahsusi zinazoweza kutekelezwa na kupimwa, badala ya kuishia katika mijadala na maazimio yasiyotekelezwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, amesema Afrika ya mwaka 2026 si Afrika ya mwaka 1960 na kwamba wakati umefika kwa washirika wa maendeleo kubadili namna wanavyoshirikiana na Serikali za Afrika.

Dkt. Kaseya amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuwa na umiliki na uelewa wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya afya, huku fedha za washirika wa maendeleo zikiendana na mipango na vipaumbele vya kitaifa.

Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohammed Janabi, amesema changamoto kubwa kwa Afrika si kukosa suluhisho katika sekta ya afya, bali ni kukosa ujasiri wa kuyafadhili, nidhamu ya kuyatekeleza na uwajibikaji wa kuyadumisha.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuwa ndiyo ngazi inayohudumia wananchi wengi zaidi nchini.

Amesema asilimia 95.6 ya wajawazito wanaojifungua nchini wanapata huduma katika ngazi ya afya ya msingi, huku asilimia 86 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma yakihudumiwa katika ngazi hiyo.

Profesa Shemdoe amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya afya ya msingi, hivyo kuongeza uwekezaji katika ngazi hiyo ni kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kwa wananchi wengi nchini.

Mkutano huo wa siku tatu unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kupitia ufadhili endelevu, ufanisi, ubora wa huduma, ubunifu, ushirikiano wa kikanda na kujenga mifumo ya afya inayostahimili majanga.

Kwa ujumla, mkutano huo unalenga kuhimiza Afrika kujenga mifumo ya afya inayojitegemea, yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, huku ikiweka mkazo katika uwekezaji wa muda mrefu, uzalishaji wa ndani, rasilimali watu na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *