Msigwa: Maafisa Habari Toeni Taarifa Zinazowagusa Wananchi
Na Baraka Messa – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali na Taasisi za Umma kuongeza ubunifu na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuangazia zaidi uwekezaji unaofanywa na Serikali na matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi.
Msigwa ametoa wito huo Septemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwakaribisha na kuwapa maelekezo Maafisa Habari wapya walioajiriwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba.
Amesema wajibu wa Maafisa Habari ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kwa wakati hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, maji, nishati, usafiri, teknolojia na sekta nyingine zinazogusa maisha yao.
Kazi yetu ni kuhabarisha wananchi. Tueleze Serikali imefanya nini, inafanya nini na inatarajia kufanya nini, kwa sababu hayo ndiyo mambo yanayowagusa wananchi.
Amesema katika kutekeleza wajibu huo, Maafisa Habari wanapaswa kuwasilisha taarifa zinazoonesha kwa uwazi uwekezaji uliofanyika, miradi inayotekelezwa, thamani ya uwekezaji huo, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, ili wananchi waweze kutambua namna rasilimali za Serikali zinavyotumika katika kuleta maendeleo.
Msigwa amesema taarifa za utekelezaji wa Serikali zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza tukio, badala yake zioneshe maana ya mradi kwa mwananchi, ikiwemo huduma zitakazopatikana, fursa zitakazozalishwa, ajira zitakazoongezeka na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema Maafisa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mipango na vipaumbele vya Serikali, pamoja na kutambua hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Taarifa nzuri si ile inayosema tu mradi umejengwa, bali ieleze mradi huo umejengwa kwa gharama gani, unahudumia wananchi wangapi na umeleta mabadiliko gani katika maisha yao.
Aidha, amewataka Maafisa Habari kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa na majukwaa ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, katika kufikisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto na inayoeleweka kwa makundi mbalimbali.
Amesema matumizi ya teknolojia yanatoa fursa ya Serikali kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo Maafisa Habari wanapaswa kutumia ubunifu katika kuandaa maudhui yanayowapa wananchi uelewa wa shughuli, miradi na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Vilevile, Msigwa amewataka Maafisa Habari hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji na maslahi mapana ya umma.
Amesema Maafisa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinajenga uelewa kuhusu maendeleo yanayotekelezwa na Serikali na kuwasaidia wananchi kutambua fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo.
Msigwa amesisitiza kuwa, kupitia taarifa sahihi, zenye ushahidi na zinazoonesha matokeo, Maafisa Habari wanaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa na mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.