Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, amesema kuwa ujio wa wanamichezo wa kimataifa nchini Tanzania akiwemo mchezaji na nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand unashawishi wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo. Bw. Msigwa ameeleza hayo Mei 20, 2026 wakati akiwa safarini na mwanamichezo huyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia treni ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini. Ameongeza  kuwa wachezaji wa kimataifa wanapokuja nchini wanaongeza macho ya wadau mbalimbali wa michezo kuitazama nchi ya Tanzania na kuona ni namna gani wataweza kuwekeza  na nchi itaweza kunufaika kwa kupata mitaji ya kuwekeza kwenye michezo, wataalam wa kushirikiana nao pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na fursa ziliozopo duniani kupitia sekta hiyo. “Ujio wa mwanamichezo huyu, unapeleka ujumbe duniani kwamba Tanzania imejidhatiti kufanya mambo makubwa kwenye sekta ya michezo hivyo kupitia wao, nchi itafanikiwa kushawishi uwekezaji katika sekta ya michezo kwani nchi yetu ina changamoto kubwa kwenye eneo la uwekezaji hasa kwenye miundombinu ya michezo pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo jezi za wachezaji, viatu, mipira ambavyo tunaagiza kutoka nje. Vile vile, tunahitaji wataalam wa michezo ambao wataleta ujuzi wa namna ya kutengeneza viwanja.” Amesema Msigwa. Kwa upande wake, Mchezaji na Nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand amesema kuwa mpira wa miguu ukitumika vizuri unaweza kufungua fursa mbalimbali pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.  Amesema kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda pamoja na wadau wa sekta ya utalii ili kuongeza hamasa na ufuatiliaji wa sekta hiyo.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), linatarajia kuanza safari za ndege kuelekea nchini Urusi mnamo Juni, 2026. Ameyasema hayo Mei 15, 2026 jijini Arusha wakati aliposhiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi linaloendelea jijini humo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Waziri Mahmoud ameeleza kuwa, nchi ya Urusi inapendelea kupata mazao yenye viwango vya hali ya juu kutoka nchini Tanzania lakini huenda ni ngumu wafanyabiashara kukidhi kigezo hicho kutokana na uhaba wa usafiri wa haraka wa kufikisha bidhaa zikiwa na ubora wake. “Tunalishukuru shirika letu la ndege nchini kwa kukamilisha mikataba yote ambapo ifikapo Juni 2026, safari zitaanza kutoka Tanzania kwenda jijini Moscow na baadaye Saint Petersburg. Wakati ndege hizo zinarudi kutoka kwenye maeneo hayo, tunategemea zitabeba watalii watakaokuja kufanya utalii nchini katika maeneo ya Zanzibar, Kilimanjaro na Dar es Salaam”. Ameongeza kuwa, shirika hilo litakuwa na ndege itakayobeba mizigo hivyo, ametoa rai kwa wafanyabiashara wanaohitaji kusafirisha bidhaa kwa haraka kutumia usafiri huo. Ametaja baadhi ya fursa ambazo Tanzania na Urusi wanaweza kushirikiana ikiwemo ujenzi wa viwanda vya mbolea, vifaa vya kilimo, shughuli za ufungashaji, usindikaji na uhifadhi wa bidhaa, TEHAMA pamoja na dawa za binadamu.

Na Mwandishi Wetu Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, amewaomba Watanzania kuendelea kulinda na kuitunza amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa wapo baadhi ya watu wanaotumika kuhamasisha vurugu nchini, hivyo ni muhimu kuwakataa kwani ustawi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya Taifa hayawezekani pasipokuwa na amani na utulivu. Msigwa amebainisha hayo leo Jumapili Mei 10, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Njombe kwenye shamba la muwekezaji wa zao la Parachichi pembezoni mwa Mji wa Njombe, akiwapongeza pia Watanzania kwa kuwakataa wale wanaohamasisha vurugu Nchini na kusisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kujielekeza katika habari zenye kuleta maendeleo na kuhamasisha umuhimu wa amani Nchini. “Najua maneno yapo mengi na wahamasishaji wamekuwa wengi. Mwalimu Nyerere alishatuambia kuwa mabeberu hawajalala na pia wakati mwingine wanawatumia miongoni mwa Watanzania kufikia malengo yao. Tuamke, hakuna nchi iliyofanikiwa kupata maendeleo ikiwa watu wake wanavurugana, wanagombana, wapo kwenye maandamano kila siku na kuhamasishana kuchoma miundombinu au kuharibu uchumi. Tukifika huko hatutatoboa.” “Nawaombeni ndugu zangu Watanzania tulinde amani yetu kwa wivu mkubwa, tukatae hamasa zozote zinazoashiria fujo na vurugu kwenye Nchi yetu. Tuwakatae wanaohamasisha vurugu na ninajua Watanzania wengi wamekataa na niwapongeze sana kwa hilo.”amesema Msigwa. Katika hatua nyingine, Msigwa pia amewataka Maafisa habari kote nchini kutenga muda na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania kama msingi wa kuweza kutekeleza Dira 2050 pamoja na hatua nyingine za maendeleo na ustawi wa jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto mchanga wa kike leo tarehe 11 Machi, 2026, katika makazi yake, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma. Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu, alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai. Akizungumza wakati wa kumkabidhi mtoto huyo, Mkuu wa Wilaya Tukai alisema mtoto huyo aliokotwa tarehe 17 Januari, 2026 akiwa ametelekezwa katika eneo jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, Nzega Mjini. Alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio. Rais Dkt. Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo. “Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” alisema Rais Dkt. Samia.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kutekeleza ahadi za Mhe. Samia Suluhu Hassan la utoaji ufadhili wa masomo kwa wanasayansi kupitia “Samia Scholarship” ili kuongeza wigo wa wanasayansi nchini ikiwemo sayansi ya Data na Akili unde. Prof. Mkenda amesema kuwa katika eneo hilo vijana 50 wanaenda katika vyuo vikuu bora nje ya nchi. Kati yao vijana 16 wanaondoka tarehe 1 Februari kwenda Chuo Kikuu cha Johannesburg kusomea shahada ya kwanza katika sayansi ya data na akili unde na Vijana wengine 34 wanatarajiwa kwenda Ireland mwezi Machi. Amesema vyuo wanavyo kwenda kusoma pamoja na kuwa kuwa vina mfumo mzuri wa kupeleka vijana katika makampuni makubwa katika nchi hizo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Dodoma. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kufikia lengo kuu la kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, la haki na linalojitegemea. Rais Dkt. Samia aliyasema hayo Alhamis, Julai 17, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa Dira uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC)—tukio ambalo pamoja na viongozi wengine lilihudhuriwa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu. Aidha, Rais Dkt. Samia alisema Dira 2050 ni matokeo ya mchakato jumuishi uliohusisha maoni ya wananchi na wadau wote na inalenga kufanikisha maendeleo jumuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Rais Dkt. Samia alisema Dira hiyo iliyozingatia matarajio ya Watanzania imejengwa juu ya msingi wa mafanikio na mafunzo ya historia ya maendeleo ya Tanzania tangu Uhuru, ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa Dira ya 2025. “Maudhui ya Dira 2050 yametokana na maoni na matakwa ya Watanzania wenyewe. Tumefikiri wenyewe, tumeandika wenyewe, tumepanga wenyewe na tutatekeleza wenyewe,” alisema Mhe. Rais. Rais Dkt. Samia alisema kuwa uandaaji wa Dira hii umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia. Aliongeza kuwa kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa $1 trilioni ifikapo mwaka 2050. alisema kuwa uandaaji wa Dira hii umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia. Aliongeza kuwa kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa $1 trilioni ifikapo mwaka 2050.