TUWAKATAE WANAOTUMIKA ILI KUTUGOMBANISHA – GERSON MSIGWA

May 10, 2026

Na Mwandishi Wetu

Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, amewaomba Watanzania kuendelea kulinda na kuitunza amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa wapo baadhi ya watu wanaotumika kuhamasisha vurugu nchini, hivyo ni muhimu kuwakataa kwani ustawi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya Taifa hayawezekani pasipokuwa na amani na utulivu.

Msigwa amebainisha hayo leo Jumapili Mei 10, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Njombe kwenye shamba la muwekezaji wa zao la Parachichi pembezoni mwa Mji wa Njombe, akiwapongeza pia Watanzania kwa kuwakataa wale wanaohamasisha vurugu Nchini na kusisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kujielekeza katika habari zenye kuleta maendeleo na kuhamasisha umuhimu wa amani Nchini.

“Najua maneno yapo mengi na wahamasishaji wamekuwa wengi. Mwalimu Nyerere alishatuambia kuwa mabeberu hawajalala na pia wakati mwingine wanawatumia miongoni mwa Watanzania kufikia malengo yao. Tuamke, hakuna nchi iliyofanikiwa kupata maendeleo ikiwa watu wake wanavurugana, wanagombana, wapo kwenye maandamano kila siku na kuhamasishana kuchoma miundombinu au kuharibu uchumi. Tukifika huko hatutatoboa.”

“Nawaombeni ndugu zangu Watanzania tulinde amani yetu kwa wivu mkubwa, tukatae hamasa zozote zinazoashiria fujo na vurugu kwenye Nchi yetu. Tuwakatae wanaohamasisha vurugu na ninajua Watanzania wengi wamekataa na niwapongeze sana kwa hilo.”amesema Msigwa.

Katika hatua nyingine, Msigwa pia amewataka Maafisa habari kote nchini kutenga muda na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania kama msingi wa kuweza kutekeleza Dira 2050 pamoja na hatua nyingine za maendeleo na ustawi wa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

© 2026 Idara ya Habari-MAELEZO. 

Get the App

Get it on

Microsoft Store

Available on the

App Store