Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Samia Aagiza Machinga Watengewe Maeneo ya Biashara

September 6, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Katika miji inayokua kwa kasi, biashara ndogo ndogo zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wananchi. Kwa maelfu ya Watanzania, biashara hizo ni chanzo cha ajira, kipato na mahitaji ya kila siku ya familia. Hata hivyo, ukuaji wa shughuli hizo unahitaji usimamizi wenye mipango unaozingatia maslahi ya wafanyabiashara, wananchi na ustawi wa miji.

Ni kwa kuzingatia umuhimu huo ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa umakini suala la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga, akieleza kuwa wameanza kurejea kwa kasi katika maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara wakubwa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Viongozi baada ya kuwaapisha Wakuu wa mikoa ya Mbeya, Geita, Pwani, Mwanza pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar tarehe 02 Septemba, 2026.

Amesema suala la wafanyabiashara wadogo lilikuwa likisimamiwa vizuri, lakini kwa sasa kumekuwa na kulegalega katika utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa.

Suala la wafanyabiashara wadogo wadogo, tulikuwa tunalisimamia vizuri, lakini kwa sasa tumepunguza usimamizi hasa katika Majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Dodoma, amesema Rais Samia.

Kwa Rais Samia, changamoto ya Machinga kurejea katika maeneo ya wafanyabiashara wakubwa haiwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu au kuwaondoa bila kuwa na mpango mbadala.

Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuweka mipango mizuri itakayowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao katika maeneo salama na yaliyopangwa.

Si kwa kuwapiga fimbo au kuwapeleka Askari Mgambo kwenda kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke, tuwapangie mipango mizuri, watoke walipo na warudi kwenye masoko, ameagiza.

Kauli hiyo inaweka msisitizo kwenye matumizi ya mipango badala ya nguvu, ili kutatua changamoto ya wafanyabiashara wadogo kwa njia inayolinda utu wao na wakati huo huo kuhakikisha miji inakuwa na mpangilio unaokubalika.

Biashara za Machinga zina nafasi kubwa katika uchumi wa wananchi kwa kuwa zinawawezesha watu wengi kujiajiri na kupata kipato bila kutegemea ajira rasmi.

Kwa baadhi ya wananchi, biashara hizi ni hatua ya kwanza ya kujenga mtaji, kukuza biashara na hatimaye kuingia katika shughuli kubwa zaidi za kiuchumi.

Hivyo, usimamizi wa wafanyabiashara hao unahitaji kuangalia zaidi namna ya kuwawezesha kukua kuliko kuwaona kama tatizo linalopaswa kuondolewa katika maeneo ya mijini.

Mipango mizuri ya upangaji wa maeneo ya biashara inaweza kuwasaidia Machinga kupata maeneo yenye wateja, mazingira salama na huduma muhimu, huku ikisaidia pia kupunguza msongamano na migongano kati ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Maelekezo ya Rais Samia kwa viongozi ya kuwarudisha wafanyabiashara wadogo katika masoko yanapaswa kutafsiriwa kama wito wa kuhakikisha maeneo hayo yana mazingira yanayoweza kuwawezesha kufanya biashara kwa tija.

Soko lenye mpangilio mzuri, usalama, usafi na mazingira rafiki kwa biashara linaweza kuwa zaidi ya sehemu ya kuuza bidhaa; linaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea huduma zao.

Kwa mtazamo huo, kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyofaa kunapaswa kuambatana na kuwaandalia maeneo mbadala yenye uwezo wa kuwasaidia kuendelea kujipatia kipato.

Ujumbe wa Rais Samia pia unawakumbusha viongozi kuwa utekelezaji wa sheria na mipango ya miji unapaswa kwenda sambamba na kuheshimu utu wa wananchi.

Viongozi wakila kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar tarehe 02 Septemba, 2026.

Wafanyabiashara wadogo wanapaswa kupewa maelekezo yanayoeleweka, kushirikishwa katika mipango inayowahusu na kupewa muda na mazingira yanayowawezesha kuhamia katika maeneo yaliyopangwa.

Kwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kufikia malengo mawili kwa wakati mmoja: kuweka miji katika mpangilio unaotakiwa na kulinda fursa za kiuchumi za wananchi.

Maelekezo ya Rais Samia yanaibua umuhimu wa kutafuta uwiano kati ya maendeleo ya miji na mahitaji ya wananchi wanaotegemea biashara ndogo ndogo.

Miji inahitaji kuwa na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara mbalimbali, huku wafanyabiashara nao wakihitaji mazingira yatakayowawezesha kufanya biashara bila kuvunja taratibu zilizowekwa.

Hivyo, suluhisho la changamoto ya Machinga si kuwafukuza kutoka eneo moja kwenda jingine, bali ni kuwa na mpango endelevu wa upangaji, ugawaji wa maeneo na usimamizi wa biashara ndogo ndogo.

Kwa kufanya hivyo, biashara ndogo zinaweza kuendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi, huku miji ikiendelea kuwa safi, salama na yenye mpangilio.

Hatua hiyo pia itaimarisha uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara wadogo kwa kujenga mazingira ambayo wananchi wanaona kuwa mipango ya Serikali inalenga kuwawezesha, badala ya kuwazuia kujitafutia maisha.

Ujumbe wa Rais Samia ni kwamba Machinga wanahitaji kupangwa na kuwezeshwa, si kubughudhiwa Wanahitaji maeneo yanayofaa kwa biashara, viongozi wenye mipango na utekelezaji unaozingatia utu.

No Next Post Available

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *