Rais Samia: Uongozi ni Dhamana, Watumikieni Wananchi

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanawasikiliza, wanatatua kero zao na kutoa huduma bora kwa ufanisi.
Rais Samia ametoa wito huo Septemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, akisisitiza kuwa nafasi walizopewa si fursa ya kujinufaisha, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi ya Taifa.
Amewakumbusha viongozi hao kuwa wao ni watumishi wa wananchi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi.
Rais Samia amewasisitiza viongozi hao kuwa utumishi wa umma ni kuwa tayari kuwatumikia wananchi waliokupa dhamana hiyo, kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya nchi.
Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za mikoa na wilaya zinapatiwa majibu na hatua stahiki kwa wakati.
Amesema uongozi wa aina hiyo utasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na kuhakikisha huduma za umma zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawahitaji viongozi wanaosubiri kero zifikishwe ofisini pekee bali wanahitaji viongozi wanaokwenda kwao, kusikiliza changamoto zao, kutafuta suluhisho na kusimamia utekelezaji ili matokeo yaonekane.