Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

MOI Yaokoa Bilioni 121.99, Rufaa za Wagonjwa Nje ya Nchi

September 1, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali takribani Shilingi bilioni 121.99 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi, baada ya kuwapatia wagonjwa 2,282 huduma za ubingwa na ubingwa bobezi katika mwaka wa fedha 2025/26.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Taasisi hiyo ilihudumia jumla ya wagonjwa 211,359, wakiwemo wagonjwa 202,000 wa nje na 9,359 waliolazwa.

Amesema kuimarishwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa, kumeiwezesha MOI kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97.

Huduma zilizoboreshwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa teknolojia za kisasa, upasuaji kupitia matundu, tiba ya maumivu, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, huduma za kiharusi, pamoja na upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua.

Katika huduma za ubingwa bobezi, wagonjwa 2,282 walipatiwa matibabu yakiwemo upasuaji wa nyonga, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa hydrocephalus na scoliosis, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za Serikali.

Aidha, amesema MOI imeendelea kuchangia ukuaji wa tiba utalii nchini, ambapo katika mwaka huo ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Balozi Dkt. Ulisubisya amesema uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na mifumo bora ya utoaji huduma umeifanya MOI kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Katika kuimarisha ubora wa huduma, asilimia 87.5 ya wagonjwa waliridhishwa na huduma walizopata, huku kiwango cha kuridhika kwa watumishi kikifikia asilimia 82 na ushughulikiaji wa malalamiko kufikia asilimia 90.

Aidha, katika kipindi hicho MOI ilifanya vipimo 83,847 vya radiolojia, ikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384, huku wagonjwa 71,819 wakipatiwa huduma za tiba kwa mazoezi (fiziotherapia).

Taasisi hiyo pia imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, zilizowafikia wagonjwa 18,455, ambapo 4,310 walifanyiwa upasuaji.

Mafanikio hayo yamekwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD lenye thamani ya Shilingi bilioni 13.8, ukarabati wa MOI Annex, maboresho ya vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa, ukarabati wa ICU ya watoto pamoja na ujenzi wa tenki la Hewa Tiba ya Oksijeni lenye ujazo wa tani 10.

Kuhusu mipango ya baadaye ya taasisi hiyo, Dkt. Ulisubisya amesema MOI itaendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Amesema pia Taasisi hiyo inaendelea kujiandaa kutoa huduma za afya kwa wanamichezo na wadau wengine wakati wa michuano ya AFCON 2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *