Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Bilioni 67.9 Zatumika Kujenga Miundombinu, Kukuza Ujuzi na Ajira kwa Vijana TIA

September 7, 2026

Na Bupe Mwaiseje – Dodoma

Elimu ya juu ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye wataalamu, wabunifu na vijana wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi. Kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza fursa za elimu na kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na ujasiriamali.

Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imewekeza jumla ya Sh bilioni 67.9 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), uwekezaji unaolenga kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa elimu bora na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri.

Uwekezaji huo umeleta mabadiliko yanayoonekana katika ukuaji wa TIA, kuanzia upanuzi wa kampasi, ongezeko la wanafunzi, maboresho ya programu za masomo, uimarishaji wa rasilimali watu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za elimu.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa shughuli za TIA kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Palangyo, amesema uwekezaji huo umeelekezwa katika kuboresha miundombinu kwenye kampasi za Mtwara, Mbeya, Singida, Kigoma, Mwanza na Zanzibar.

Mbali na uwekezaji wa Sh bilioni 67.9, TIA imepata Sh bilioni 27.8 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo miundombinu, TEHAMA, samani, mafunzo ya wahadhiri, maboresho ya mitaala, tathmini na shughuli nyingine za mradi. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 22.6 zimetumika moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya Kampasi za Singida na Mwanza.

Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika upanuzi wa TIA kutoka kuwa na kampasi sita mwaka 2021/22 hadi kufikia kampasi nane mwaka 2025/26, baada ya kuongezwa kwa kampasi za Tanga na Zanzibar.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 07, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Ukuaji huo umeenda sambamba na ongezeko la idadi ya wanafunzi. Kutoka wanafunzi 24,494 mwaka 2021/22, idadi hiyo imefikia 37,397 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 52.7. Wakati huohuo, uwezo wa taasisi kuhudumia wanafunzi umeongezeka kwa asilimia 35.

Haya si mabadiliko ya miundombinu pekee; ni upanuzi wa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya juu na ujuzi unaohitajika katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya Taifa. Katika kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya uchumi wa sasa, TIA imeongeza programu za masomo kutoka 49 hadi 54.

Miongoni mwa programu hizo ni Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha, ambazo zinalenga kuwajengea vijana uwezo katika biashara, ujasiriamali, uchumi na usimamizi wa fedha.

Kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu, wanafunzi 19,342 katika kampasi za Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Mbeya, Kigoma na Mtwara wamenufaika na mikopo hiyo. Aidha, jumla ya wahitimu 62,680 wamehitimu na kuingia katika maeneo mbalimbali ya ajira, ujasiriamali na huduma za kitaaluma.

Prof. Pallangyo anasema ubora wa elimu hauwezi kutenganishwa na ubora wa walimu na wahadhiri. Kwa kutambua hilo, Serikali imeiwezesha TIA kupata maprofesa tisa na kugharamia watumishi 78 kusoma Shahada za Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi. Kati yao, watumishi 48 tayari wamehitimu, huku 30 wakiendelea na masomo.

Hatua hiyo imeongeza uwezo wa TIA katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na uzalishaji wa maarifa. Sambamba na hilo, taasisi imeanzisha programu za Shahada ya Uzamili katika kampasi za Zanzibar, Mbeya, Singida na Mwanza.
Hivyo, uwekezaji katika rasilimali watu unaendelea kuifanya TIA kuwa taasisi inayozalisha wahitimu pekee wenye maarifa na ubunifu unaoweza kutumika katika kutatua changamoto za jamii.

Moja ya mafanikio yanayoipa thamani zaidi elimu inayotolewa TIA ni juhudi za kuwaunganisha wanafunzi na fursa za ajira na ujasiriamali. Zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa. Wakati huohuo, zaidi ya wanafunzi 500 wamepatiwa mafunzo mahsusi ya ujasiriamali na takribani 100 wamewezeshwa kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Anasema mfano wa matokeo ya juhudi hizo ni Nicolaus Carol Mboya, mmoja wa wahitimu wa TIA ambaye ameanzisha kampuni ya STEAMORA inayotoa mafunzo ya teknolojia ya elimu kwa watoto na vijana. Kupitia STEAMORA, vijana wanapata mafunzo katika teknolojia mbalimbali ikiwemo roboti, upangaji programu (coding), ubunifu wa miundo ya pande tatu (3D) na akili bandia (AI).

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2026, kampuni hiyo imewafikia zaidi ya wanafunzi 600 kupitia ushirikiano na shule nane za kimataifa na vituo viwili vya kujifunzia vya kijamii jijini Dar es Salaam. Aidha, ina watumishi wanane na imezalisha zaidi ya Shilingi milioni 15 katika mapato jambo linalotoa taswira ya elimu inayokwenda hatua moja zaidi—elimu inayompa kijana si cheti pekee, bali pia uwezo wa kutengeneza fursa.

TIA pia imeendelea kukuza utamaduni wa ubunifu kupitia Shindano la Ubunifu linalowapa wanafunzi nafasi ya kubadilisha mawazo yao kuwa suluhisho na fursa za biashara. Mwaka 2025, jumla ya mawazo 376 yaliwasilishwa katika shindano hilo. Kati yake, washindi 57 walipatikana na mawazo 17 yalifikia hatua ya kuanzishwa kuwa biashara zinazofanya kazi.

Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA TIA imeendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma. Taasisi imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kusimamia taarifa za wanafunzi (SIMS), unaowawezesha wanafunzi kupata huduma mbalimbali kuanzia maombi ya kujiunga, udahili na usajili, malipo, matokeo, huduma za maktaba hadi kujifunza kwa njia ya mtandao. Maboresho hayo yanalenga kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuendana na mahitaji ya kizazi cha sasa kinachokua katika mazingira ya kidijitali.
Uwekezaji wenye matokeo kwa Taifa
Kwa ujumla, uwekezaji unaofanywa na Serikali katika TIA unaonesha namna fedha zinazowekezwa katika elimu zinavyoweza kubadilika na kuwa fursa kwa vijana na Taifa kwa ujumla. Kutoka kwenye majengo na miundombinu hadi kwenye taaluma, TEHAMA, utafiti, ubunifu na ujasiriamali, uwekezaji huo umeiwezesha TIA kupanua wigo wa elimu ya juu na kuongeza uwezo wa kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *