Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Makamu wa Rais Aagiza Hatua za Haraka Kushusha Bei ya Saruji

September 4, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini kutafuta suluhu ya haraka ya kurejesha bei ya saruji katika viwango vinavyomudu wananchi.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya 19 ya Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani, iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Amesema maono ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa muhimu kwa gharama nafuu, hivyo ni muhimu kuoanisha uzalishaji na upatikanaji wa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa saruji ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama.

Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Serikali kufanya tathmini ya ukuaji wa sekta ya viwanda nchini ili kubaini iwapo viwanda vilivyopo vina uwezo wa kushindana katika masoko ya kikanda, Afrika na kimataifa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati wa hafla ya utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), zilizofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa bandia na biashara haramu zinazokwepa kodi na tozo, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaathiri viwanda vya ndani, mapato ya Serikali na ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Makamu wa Rais amewataka wazalishaji kuongeza uchakataji wa malighafi ndani ya nchi na kuongeza thamani ya bidhaa, hatua itakayoongeza ajira, mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Pia ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakiki takwimu za idadi ya viwanda vilivyopo nchini ili kuweka mikakati ya kuimarisha uwakilishi wa wazalishaji kupitia Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).

Amesema sekta ya viwanda ni mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuwa inaongeza thamani ya malighafi, inazalisha ajira, inaongeza mapato ya Serikali na fedha za kigeni, huku ikichochea sayansi, teknolojia, ubunifu na uvumbuzi.

Kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ikiwemo misitu na madini, ni muhimu kuendelea kukuza sekta ya viwanda na kujenga uhusiano madhubuti kati ya viwanda na sekta nyingine ili kuongeza ufanisi na kipato cha Watanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Amesema Wizara imekamilisha Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la 2025, zinazolenga kwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Suphian Ally, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), bandari, barabara na nishati, akisema miradi hiyo imepunguza gharama za usafirishaji na kurahisisha biashara.

Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Hafla hiyo imewakutanisha wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *