Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

AFCON 2027: Mpira Utapiwa Uwanjani, Fursa Zitakuwa Mitaani

September 18, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Mwaka 2027, macho ya Afrika na dunia yataelekezwa Afrika Mashariki wakati Tanzania, Kenya na Uganda zitakapokuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Kwa Tanzania, tukio hili ni zaidi ya dakika 90 za mchezo uwanjani; ni jukwaa kubwa la biashara, utalii, uwekezaji na kuitangaza nchi kwa mamilioni ya watu duniani.

Kuanzia Dar es Salaam, Arusha hadi Zanzibar, ujio wa mashabiki, watalii na wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani ni wazi kwamba utaongeza mahitaji ya malazi, usafiri, chakula, burudani, bidhaa na huduma nyingine, na hapo ndipo fursa kwa Watanzania zinapojitokeza, na ukubwa wa manufaa ya fursa hizo utategemea namna wafanyabiashara na watoa huduma watakavyojiandaa mapema.

AFCON 2027 inatoa nafasi ya Tanzania kutumia tukio la michezo kutengeneza shughuli za kiuchumi zinazoweza kuendelea hata baada ya mashindano kumalizika. Hoteli zinaweza kupanua huduma, sekta ya utalii inaweza kuongeza bidhaa na vifurushi vipya, huku wafanyabiashara wadogo na wakubwa wakitengeneza bidhaa na huduma zinazolenga mahitaji ya wageni.

Kupitia Podcast ya Idara ya Habari-MAELEZO, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuanza maandalizi mapema ili fursa zitakazotokana na AFCON 2027 ziwafikie wazawa na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Msigwa anaeleza kuwa uzoefu wa nchi nyingine zilizowahi kuwa wenyeji wa AFCON unaonyesha ukubwa wa fursa zinazoweza kujitokeza. Anatoa mfano wa Morocco, iliyokuwa mwenyeji wa AFCON iliyofanyika Desemba 2025 hadi Januari 2026, ambapo zaidi ya wageni milioni 1.6 walifika nchini kutoka maeneo mbalimbali.

Takwimu hiyo inaonyesha kwa nini maandalizi hayawezi kusubiri hadi mashabiki waanze kuwasili. Fursa inaanza kabla ya mpira kuanza. Mfanyabiashara anayejipanga leo ana nafasi ya kuwa tayari wakati mahitaji yatakapoongezeka.

Kwa wafanyabiashara wa hoteli, utalii, usafiri na chakula, AFCON 2027 inaweza kuwa soko jipya lenye mahitaji makubwa. Msigwa anawataka watoa huduma kutumia muda uliopo kuboresha huduma zao na kujiandaa kukidhi mahitaji ya wageni.

Kama wewe unafanya biashara ya utalii, jiandae kuwasafirisha wageni kuwapeleka maeneo mbalimbali. Kama wewe ni mfanyabiashara wa hoteli, jiandae kushawishi wageni wafikie kwenye hoteli yako, na kama wewe ni mfanyabiashara wa chakula, jiandae kuandaa chakula kizuri ili wageni wakija wajisikie kuweka kambi na kuja kula kwako.

Ujumbe wa Msigwa unaweka jukumu kubwa kwa sekta binafsi: kutazama AFCON si kama tukio la kutazama mpira wa miguu pekee, bali kama soko la kutengenezwa na kutumiwa katika kukuza uchumi w mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mbali na biashara za moja kwa moja wakati wa mashindano, AFCON 2027 inaweza kuwa kichocheo cha uwekezaji katika maeneo yenye mahitaji ya muda mrefu. Makazi, hoteli, usafirishaji, kilimo, teknolojia na huduma mbalimbali ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuhitaji uwekezaji zaidi.

Msigwa anawataka Watanzania na sekta binafsi kuanza kuwasiliana na wadau ndani na nje ya nchi ili kuvutia uwekezaji na kutumia tukio hilo kama mlango wa kuonyesha fursa zilizopo Tanzania.

Rais ametuletea tukio kubwa, sisi tulitumie kufanya uwekezaji mkubwa, mfano kwenye makazi. Kwenye kilimo tukaribishe wadau wazuri wenye teknolojia na mitambo ya kisasa kuja kuwekeza.

Hii ina maana kwamba faida ya AFCON haipaswi kuishia katika mapato yatakayopatikana wakati wa mashindano. Tanzania inaweza kutumia wageni watakaofika kama daraja la kufungua masoko mapya, mitandao ya biashara na uwekezaji wa muda mrefu.

AFCON 2027 pia ni fursa ya Tanzania kujitangaza kupitia michezo. Wageni watakapofika nchini watapata nafasi ya kuona zaidi ya viwanja vya soka. Wataona utamaduni, vivutio vya utalii, bidhaa na mazingira ya biashara na uwekezaji.

Kwa mtazamo huo, mashindano yanaweza kuwa jukwaa la kuitambulisha Tanzania kama eneo la utalii, biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika.

Wakati fursa hizo zikitarajiwa, maandalizi ya miundombinu ya michezo yanaendelea. Kwa mujibu wa Msigwa, viwanja vitakavyotumika katika mashindano pamoja na viwanja vya mazoezi vimekamilika kwa kiwango kikubwa.

Tanzania pia inaendelea na maandalizi ya kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika mashindano hayo na kuunga mkono Taifa Stars, huku mikakati ya hamasa ikitarajiwa kulenga Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha.

Hatimaye, thamani ya AFCON 2027 kwa Tanzania haitapimwa kwa idadi ya mechi zitakazochezwa pekee, bali pia kwa fursa zitakazobaki baada ya mashindano.Tukio hilo linaweza kuwa kichocheo cha biashara mpya, uwekezaji, ajira, utalii na masoko mapya ikiwa maandalizi yatafanyika kwa wakati.

Kwa Watanzania, ujumbe ni mmoja: AFCON 2027 isiwe mashindano ya kutazama mpira tu uwanjani au kupitia Televisheni; iwe fursa ya kufanya biashara, kuwekeza, kuzalisha na kujenga. Mpira utakapigwa uwanjani, fursa zitakuwa mitaani, kwenye hoteli, mashamba, viwanda, usafiri na biashara mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *