Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Kumuwezesha Mkulima ni Kuimarisha Uchumi wa Taifa

September 21, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Sekta ya Kilimo kwa miaka mingi imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania na inayotoa uhakika wa usalama wa chakula, kutoa ajira kwa mamilioni ya wananchi na kuchechemua biashara, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji. Hivyo, kumuwezesha mkulima kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha kipato si jukumu la sekta moja pekee, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika uchumi na mustakabali wa Taifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, uwekezaji katika sekta ya kilimo umeongezeka. Mathalani Bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi trilioni 1.19 mwaka 2025/2026. Ongezeko hilo linaonesha uzito wa sekta ya kilimo katika ajenda ya maendeleo na juhudi za kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kuongeza uzalishaji.

Miongoni mwa hatua zinazomgusa mkulima moja kwa moja ni mfumo wa ruzuku za pembejeo, hususan mbolea na mbegu bora. Lengo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija shambani. Taarifa zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 360,000 kabla ya mfumo wa ruzuku hadi tani 840,000 katika msimu uliofuata, huku lengo likiwa kufikisha matumizi hadi tani milioni moja.

Lakini kuongeza uzalishaji kunahitaji pia uhakika wa maji. Kutegemea mvua pekee kunaendelea kuwa changamoto katika uzalishaji wa kilimo, hivyo uwekezaji katika umwagiliaji ni hatua muhimu ya kumuwezesha mkulima kuzalisha kwa uhakika zaidi. Kufikia mwaka 2024/2025, Serikali ilikuwa ikitekeleza miradi 780 ya umwagiliaji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 543,000, huku kukamilika kwa miradi hiyo kukitarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji hadi zaidi ya hekta milioni 1.27.

Pamoja na miundombinu hiyo, ushiriki wa wakulima katika usimamizi wa umwagiliaji nao umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imepanda kutoka 19 mwaka 2020/2021 hadi 912 mwaka 2024/2025. Hii inaashiria nafasi inayoongezeka ya wakulima katika kusimamia rasilimali muhimu kwa uzalishaji wao.

Kilimo pia kinafungua ukurasa mpya kwa vijana. Kupitia programu kama Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), vijana wanahamasishwa kukiona kilimo kama biashara na fursa ya uwekezaji. Mtazamo huu ni muhimu kwa kizazi kinachoweza kutumia teknolojia, ubunifu na maarifa ya kisasa kubadilisha kilimo kutoka shughuli ya kutegemea nguvu kazi pekee na kuwa biashara yenye tija.

Hata hivyo, kumuwezesha mkulima hakumaanishi kumuwezesha kuzalisha pekee. Mkulima anahitaji kuwezeshwa kuzalisha, kuhifadhi, kusindika na kuuza kwa thamani inayostahili. Bila soko la uhakika na uwezo wa kuongeza thamani, ongezeko la uzalishaji linaweza lisitafsiriwe moja kwa moja kuwa ongezeko la kipato.

Hapa ndipo nafasi ya viwanda inakuwa muhimu. Mazao yanayotoka mashambani yanapaswa kuwa malighafi ya viwanda vya ndani. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, nafaka zikachakatwa kuwa bidhaa mbalimbali, maziwa yakaongezwa thamani na mazao mengine yakahifadhiwa na kusindikwa. Kwa kufanya hivyo, thamani inayotokana na kilimo hubaki zaidi ndani ya nchi, huku ikifungua nafasi za ajira na biashara.

Kwa mtazamo huo, Agenda 10/30 inaleta umuhimu wa kuongeza tija, thamani ya mazao, mauzo ya nje, ushiriki wa vijana na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda. Kilimo kinapounganishwa na viwanda na masoko, mkulima haonekani tena kama mzalishaji wa malighafi pekee, bali anakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani unaozalisha utajiri.

Hata hivyo, kipimo cha mwisho cha mafanikio ya uwezeshaji kinapaswa kuwa maisha ya mkulima. Bajeti inaweza kuongezeka na miradi inaweza kujengwa, lakini mafanikio halisi yataonekana pale mkulima atakapoweza kuzalisha kwa gharama nafuu, kupata mavuno bora, kuhifadhi mazao, kupata soko na kulipwa kwa thamani inayolingana na jasho lake.

Tanzania ina ardhi, maji, nguvu kazi, masoko na malighafi nyingi zinazoweza kuifanya kilimo kuwa injini kubwa zaidi ya uchumi. Kinachohitajika ni kuendelea kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kutumia fursa hizo kikamilifu na kuwahamasisha vijana, wafanyabiashara na wawekezaji kuingia katika kilimo kwa mtazamo wa biashara.

Tanzania yenye mkulima mwenye uwezo wa kiuchumi ni Tanzania yenye msingi imara wa chakula, viwanda, ajira na uchumi shirikishi. Kumuwezesha mkulima si kumsaidia mkulima pekee ni kuijenga Tanzania yenye uwezo wa pato la Taifa lenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola za Marekani 7000 kwa mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *